in , , ,

Chelsea wamtumie nani kupachika mabao?

Kila msimu wa kiangazi Chelsea husaka wapachika mabao hawajabaki nyuma msimu huu katika kiu yao hiyo.
Hata majuzi Kocha Jose Mourinho alithibitisha kwamba wanataka kuongeza mchezaji mmoja hapo Stamford Bridge.
“Tutajaribu hadi siku ya mwisho ya dirisha la usajili kuongeza mchezaji mpya kwenye kikosi chetu. Mfungaji,” Mreno huyo alisema baada ya Chelsea kuwafyatua Hull City Tigers 2-0.
Kwamba ni nani huyo mgeni anayekuja limebaki kuwa swali na watu kuhisi, lakini Chelsea wamekataliwa ofa zao mbili kwa mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney anayetaka kuhama Old Trafford, lakini wenyewe hawataki kumuuza.
Nyota wa Cameroon, Samuel Eto’o amehusishwa pia na mipango ya kuhamia Stamford Bridge mara kadhaa, huku Demba Ba sasa akionekana kama mtu wa ziada tu hapo.
Kwa msingi huo, washambuliaji wa kati wanaotambulika rasmi ni Fernando Torres na Romelu Lukaku.
Nia ya kuimarisha eneo hilo ni kubwa, lakini nani kati ya wapachika mabao waliopo klabuni na wale wanaohusishwa na kuhamia hapo wanaofaa zaidi kwa mfumo wa Mourinho?

Fernando Torres

Huyu aliwahi kuwa mpachika mabao aliyeogopewa zaidi barani Ulaya, lakini kushuka kiwango sana katika siku zake za mwanzo Chelsea kulikuwa anguko kubwa kwake.
The Blues walimwaga pauni milioni 50 Januari 2011, rekodi ya aina yake lakini haielekei kwamba zinalipa japokuwa bado Roman Abramovich anataka Torres ‘afufuliwe’.
Msimu uliopita Mhispania mwenzake, Rafa Benitez alifanya kazi hiyo na kuelekea kufanikiwa, ambapo alifunga mabao 23 kwenye mashindano yote katika klabu hiyo na katika mashindano ya Kombe la Mabara alitwaa kiatu cha dhahabu.
Alicheza vyema mechi ya kwanza dhidi ya Hull, ambapo alisababisha penati ambayo Frank Lampard alikosa na adhabu ndogo iliyowapatia bao moja.

Romelu Lukaku

Chelsea walimpeleka Romelu Lukaku West Bromwich Albion kwa mkopo msimu uliopita, akang’ara vilivyo kiasi cha kufunga mabao 17 kwenye Ligi Kuu.
Washabiki wa Chelsea walianza kupiga kelele arudi Stamford Bridge, kocha wa West Brom Steve Clark akawaomba Chelsea abaki tena kwa mkopo msimumwingine, lakini akakataliwa, na sasa amerejea Stamford Bridge.
Lukaku (20) aliapa kwamba angejifua na kukuza kiwango chake, akisema ndoto yake ni kuwa kama mchezaji mwenzake hapo zamani, Didier Drogba, na anaelekea huko, akizinyanyasa safu za ulinzi kama raia huyo wa Ivory Coast.
Anaweza kucheza namba tofauti na alidhihirisha hivyo akiwa na The Baggies msimu uliopita. Anatumia akili, mpira haumtoki mguuni na ana kasi ya ajabu na nguvu pasipo kucheza rafu.

Samuel Eto’o

Ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa katika timu mbalimbali, zikiwamo Barcelona na Inter Milan, hivyo kwamba Ulaya yote inajua jinsi anavyotisha.
Mpachika mabao huyu kutoka Cameroon amefanikiwa kutwaa Kombe la Mabingwa Ulaya mara tatu, lakini tangu ahamie Anzhi Makhachkala ya Urusi mwaka 2011, ni kana kwamba ameshuka na wengi wamepoteza mvuto kwake.
Ameshindwa kufunga mabao mengi kama zamani, ambapo kwa misimu miwili iliyopita amefunga mabao 24 tu, ikilinganishwa na mabao 34 katika msimu wake wa mwisho Barca 2008/09 na mabao 29 mwaka wake wa mwisho Inter, yaani 2011, ni wazi si mchezaji yule yule.
Katika umri wake wa miaka 32 amekumbwa pia na majeraha ya mara kwa mara na hilo linatakiwa kutiliwa maanani na Mourinho ikiwa atamleta Stamford Bridge, atakakotakiwa kuasili aina ya mchezo wa nguvu na kasi zaidi wa England na Ulaya, tofauti na ule wa Urusi.

Wayne Rooney

Mwingereza huyu ana machungu mengi moyoni, akitafuta njia za kuondoka Old Trafford tangu enzi za Alex Ferguson hadi sasa za David Moyes lakini anaambiwa haendi popote.
Anadhani kwamba muda wake hapo umetosha, lakini Moyes alimnyanyua kutoka benchi katika fungua dimba ya ligi dhidi ya Swansea wikiendi hii, ambapo alichangia upatikanaji wa mabao mawili kwenye ushindi mnono wa 4-1 Liberty Stadium.
Uchezaji wake Jumapili ulidhihirisha kwamba akili yake imetulia kiasi, na hilo linaweza kumfurahisha Moyes, lakini na Mourinho pia anayemhitaji.
Anapokuwa fiti kabisa, Rooney ni mmoja wa wachezaji wazuri zaidi katika Ligi Kuu hii na amekuwa akifunga mabao kutoka upande wowote wa uwanja. Alisaidia upatikanaji mabao 13 msimu uliopita. Ni mfungaji mzuri akipewa nafasi yake ya namba tisa.
Kwa kujumuisha, Eto’o si chaguo jema sana kwa Chelsea, maana ataanzia benchi, na wanaye mtu wa aina hyo, Ba. Ama kwa kinda Lukaku, ni hazina kubwa kwa Chelsea, lakini ajue kufunga mabao hapa ni tofauti na kule West Brom, hivyo lazima awe mvumilivu hata akianzia benchi au kutocheza kabisa kwa muda.
Kwa msingi huu, chaguo kubwa lililopo mbele ya Mourinho kwenye upachikaji mabao ni kati ya Torres na Rooney, kama watampata. Wakimkosa Rooney, basi Lukaku atachukua nafasi yake na itategemea kama Torres ataendeleza mazuri yake au la.
Torres ana namna ya kutojiamini, tofauti na Rooney anayeona hakuna cha kumshinda. Imemchukua muda Torres kuasili aina ya mchezo wanaotaka Chelsea, na si yule aliyesajiliwa kutoka Liverpool.
Kule Anfield, Torres alifanikiwa zaidi na kulishwa mipira na akina Steven Gerrard na Xabi Alonso, mwenyewe akiwa mtu wa mwisho, akisababisha majanga kwenye ngome za maadui kwa kumalizia mipira moja kwa moja.
Chelsea hawachezi soka ya aina hiyo, maana yake ni kwamba wanapenda kumiliki mpira na kuzunguka hadi wakati mwafaka wa kupachika bao ufike, kitu ambacho Rooney amebobea, na ndicho amekuwa akifanya United kwa muongo uliopita.
Torres ni mshambuliaji na mpachika mabao mzuri, lakini Chelsea wakifanikiwa kumnyakua Rooney, kocha Mourinho atakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuchagua nani akae pale mbele, kulingana na timu wanayokabiliana nayo pia.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal wanajiandalia majanga

24 WAITWA TAIFA STARS KUIVAA GAMBIA