in , , ,

Chelsea wagomea kileleni

*Southampton na ushindi wa kwanza, Everton safi

*Swansea wazidi kupepesuka, Reading sasa mkiani

Ligi Kuu ya England imechanua kivingine, ambapo Chelsea imebaki kileleni, lakini Southampton imepata ushindi wake wa kwanza.
Vijana wa Stamford Bridge wanaodaiwa kutomfurahisha mmiliki, Roman Abramovich kwa wanavyocheza, hasa kimataifa, walibanwa na Stoke City hadi dakika tano za mwisho wakaambulia bao.
Baada ya kupoteza mechi nne za mwanzo, Southampton wameipatia Astona Villa kwa kuikandika mabao 4-1.
Chelsea ilipata bao kupitia beki wake, Ashley Cole, baada ya washambuliaji wake, Eden Hazard, Juan Mata, Fernando Torres na Oscar kukwama kumtungua golikipa Jonathan Walters.
Chelsea hawajapoteza mchezo wowote wa ligi msimu huu na pia hawajapata kufungwa na Stoke tangu Oktoba 4, 1995. Stoke waliwashinda Chelsea mara ya mwisho kwenye ligi mwaka 1975.
Chelsea wamejikusanyia pointi 13 baada ya mechi tano, Stoke wakibaki hawajashinda mechi yoyote, bali sare nne.
Southampton watakuwa na mwisho wa wiki wa kufurahia, kwani washabiki na wadau walishaanza kujiuliza mfululizo wa kufungwa ungeisha lini.
Saints, kama wanavyojulikana zaidi, walianza kufungwa, kabla ya mshambuliaji wao mahiri, Rickie Lambert kukomboa na kuja kupachika bao la mwisho.
Baada ya mechi nne walikuwa hawana pointi, na sasa kwa pointi tatu wamechupa hadi nafasi ya 17. Wapo waliokwishaanza kujadili kumng’oa kocha Nigel Adkins aliyewapandisha madaraja mawili hadi walipo.
Swansea walioanza ligi kwa kasi na kukaa juu ya msimamo kwa muda, wamepata kipigo cha pili, safari hii kikiwa kutoka kwa wakali Everton, waliowanyoa mabao 3-0.
Swansea walimaliza wakiwa 10, baada ya Nathan Dyer kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano kutokana na mchezo mbaya, mwenyewe akiwa ameingia kipindi cha pili.
Everton wamechupa hadi nafasi ya pili, japokuwa wanaweza kukaa kwa saa 24 tu. Katika michezo 16 waliyokutana katika mashindano mbalimbali, Swansea hawajapata kuwashinda Everton, ambapo katika ligi Everton wameshinda yote.
West Bromwich Albion waliwanyong’onyeza wageni wengine kwenye ligi, Reading, kwa kuwafunga bao 1-0 na kuwashusha hadi kwenye sakafu ya msimamo wa ligi.
Romelu Lukaku aliyetolewa kwa mkopo na Chelsea ndiye alifunga bao. Amekuwa akisema anataka kucheza na kufunga kama nyota Didier Drogba aliyekuwa Chelsea, ambaye sasa anachezea Shanghai Shenhua.
Reading hawajashinda hata mechi moja msimu huu, japokuwa wapo nyuma mchezo mmoja, mkononi wakiwa na pointi moja pia. West Brom wanashika nafasi ya tatu, pengine kwa muda.
Katika mechi nyingine, West Ham United walitoshana nguvu na Sunderland kwa kufungana bao 1-1.
Nusura vijana wa Sam Allerdyice wazikose pointi zote, kwani Sunderland, au Paka Weusi, waliongoza hadi dakika zikiyoyoma.
West Ham wanashika nafasi ya nane kwa pointi nane baada ya mechi tano, huku Sunderland wakiwa wa 12 baada ya sare ya mechi zake zote.
Timu mbili zisizotabirika za Fulham na Wigan zimekutana na kuumana, ambapo ilikuwa zamu ya kocha Martin Jol wa Fulham kucheka kwa kumfunga Roberto Martinez kwa mabao 2-1.
Mchezo huu ulishuhudia mwamuzi, Lee Probert akihitaji matibabu, baada ya kuminywa pale Steve Sidwell wa Fulham na Ben Watson wa Wigan walipokabiliana. Kwa kutania alipunga kadi nyekundu wakati mchezo ukiwa umesimama.
Huu ni ushindi wa kwanza ugenini msimu huu kwa Fulham, na mwaka jana pia waliupata walipowatembelea Wigan.
Fulham wamepanda hadi nafasi ya nne, huku Wigan wakiwa mbali – wa 15 kwa pointi nne tu walizojikusanyia.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

KAMATI YATANGAZA MCHAKATO WA UCHAGUZI TWFA

Super Sunday kicheko Manchester United