JUMANNE ya mwisho wa mwezi wa Januari imekuja na mechi za Ligi Kuu ya
England (EPL) ambapo matokeo yalikuwa mchanganyiko.
Mechi kubwa ilikuwa baina ya Liverpool na Chelsea uwanjani Anfield
ambapo Liver walikuwa wametoka kuchezea vichapo vitatu vibaya.
Antonio Conte wa Chelsea alikuwa akihofia hasira za Jurgen Klopp na
vijana wake, na kweli haikuwa kazi rahisi usiku ule.
Chelsea walitangulia kupata bao kupitia kwa mpira wa adhabu ndogo wa
David Luiz, Diego Costa akakosa penati iliyopanguliwa na Simon
Mignolet huku Georginio Wijnaldum akisawazisha bao.
Bado Chelsea wamekaa kwenye usukani wa EPL kwa tofauti ya pointi tisa,
wa pili wakiwa ni Tottenham Hotspur waliowavuka Arsenal Jumanne hii.
Spurs walikwenda suluhu na Sunderland na hivyo kufikisha pointi 47
sawa na za Arsenal ambao walipokea kichapo cha 2-1 kutoka kwa timu
ndogo ya Watford waliopata mabao yao mapema kabla ya Arsenal kufuta
machozi dakika ya 60 hivi.
Kazi ipo kwa Arsenal kwa hakika, maana wakati huu ambapo bado kocha
Arsene Wenger amefungiwa kuwa eneo la ufundi, wanakabiliana na Chelsea
muda wa mchana Jumamosi hii Stamford Bridge.
Ni wenger huyu huyu anasema kwamba kisaikolojia wachezaji wake
hawakuwa tayari kwa gemu dhidi ya Watford, kitu ambacho kwa wengi
hakieleweki, maana ndivyo ratiba ilivyo, na wengine wamecheza na
wanaendelea kucheza.
Arsenal wamejiweka pia hatarini kuondoka kwenye nne bora, maana sare
ya Liverpool imewaweka piointi moja tu nyuma yao na bado wanakuja
Manchester City wenye pointi 43 na Man United japo wana 41, huwezi
kujua kasi itakuwaje, ukizingatia wote wawili wa Manchester wana mechi
moja mkononi.
Wa katikati tuachane nao, twende mkiani ambako tunawakuta Hull na
Sunderland wote wakiwa na pointi 16 na hatarini kushuka daraja. Rafiki
yao ni Crystal Palace – pointi 19 huku Swansea Leicester na
Middlesbrough kila mmoja akiwa na pointi 21.
Kazi ipo huko kujinasua kushuka daraja.
Jumanne hii, Bournemouth aliangukia pua nyumbani kwa 0-2 dhidi ya
Crystal Palace wanaofundishwa na Sam Allerdyce, ikiwa ni mechi ya
kwanza kushinda.
Burnley wamewakandika mabingwa watetezi Leicester 1-0, Middlesbrough
na West Bromwich Albion wametoshana nguvu 1-1 na Swansea amempiga
Southampton 2-1.
Jumatano hii EPL inaendelea baina ya West Ham na Manchester City;
Manchester United na Hull na Stoke dhidi ya Everton.