*Arsenal wamo, Man City kilio
*Sunderland wamerudi mkiani
Chelsea wamerejea kwenye uongozi wa Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya
ushindi mwembamba dhidi ya West Bromwich Albion.
Ulikuwa ni ushindi wa tisa mfululizo na bao lilifungwa na Diego Costa
katika dimba lao la Stamford Bridge na kufikisha pointi 37 dhidi ya
Arsenal walioongoza tangu Jumamosi wakiwa na pointi 34.
Mshambuliaji huyo wa Hispania alifaidi makosa ya Gareth McAuley kwenye
dakika ya 76, akampokonya mlinzi huo mpira wakati akisita na kumshinda
kipa Ben Foster.
West Brom walielekea kana kwamba wangepata pointi moja kutokana na
ukakamavu wao walioonesha tangu mwanzo wa mchezo, lakini wakaishia kwa
maumivu hayo.
Kwenye mechi nyingine Jumapili hii Manchester United hatimaye
walicheka kwa kupata ushindi dhidi ya Tottenham Hotspur.
Hata hivyo, bado wana kazi kwani wapo nyuma ya mahasimu wa mji wao,
Manchester City wanaoshika nafasi ya nne, kwa pointi sita.
Katika mechi nyingine Southampton walizinduka na kuwafunga
Middlesbrough 1-0 wakati Liverpool wakibanwa nyumbani kwao na West Ham
wakaenda 2-2.
Jumamosi Arsenal walipanda hadi nafasi ya kwanza kutokana na ushindi
wao wa mabao 3-1 dhidi ya Stoke, ila sasa wapo nafasi ya pili, Watford
wakawashindilia Everton 3-2 na Burnley wakawashinda Bournemouth kwa
idadi hiyo hiyo ya mabao.
Kwingineko Hull walienda sare ya 3-3 na Crystal Palace, Swansea
wakawakandika Sunderland 3-0 na kuondoka mkiani huku Pep Guardiola
akidhalilishwa na Leicester waliowapiga Man Cit 4-2.
Mechi nyingine katika mwezi huu wa msimu wa sikukuu zinaanza Jumanne
hii na ilivyo sasa ni kwamba Liverpool wanashika nafasi ta tatu kwa
pointi 31, Man City wakifuatia na 30 huku Spurs wakiwa nazo 27 na Man
U 24.
Sunderland wamerudi mkiani kwa pointi zao 11, wakifuatiwa na Hull na
Swansea zenye 12 kila moja na West Ham wenye 13.