Ligi Kuu ya England (EPL) imeendelea kwa vinara Chelsea, wa pili wao Manchester City na Arsenal kupata ushindi.
Chelsea waliowafunga Tottenham Hotspur 3-0 wanabaki kwenye kiti cha uongozi kwa tofauti ya pointi sita. Spurs hawakutarajia kushinda mechi hiyo, kwani hawajapata kushinda Stamford Bridge katika mechi 23 zilizopita.
Spurs walipoteza nafasi mbili nzuri za kufunga mapema mchezoni, ambapo Harry Kane alifyatua shuti lililogonga mwamba na baadaye akiwa kwenye nafasi nzuri akapiga mpira ulioishia kuwa mwingi na kutoka nje.
Chelsea walianza makeke kwa Eden Hazard kumalizia kazi nzuri waliyofanya kwa kugongeana na Didier Drogba aliyecheza badala ya Diego Costa aliyezuiliwa kucheza baada ya kuoga kadi tano za njano. Kipa wa Spurs, Hugo Lloris atalaumiwa kwa bao hilo.
Drogba alifunga bao la pili na mshambuliaji mwingine, Loic Remy, aliyeingia kipindi cha pili, akamaliza kazi na kuwafanya Chelsea sasa kutamba kwa kutofungwa katika mechi zao 23 kwenye mashindano yote, rekodi ambayo walipata kuiweka kabla.
MANCHESTER CITY WAWARARUA SUNDERLAND
Manchester City wameendeleza wimbi la ushindi kwa kuwchakaza Sunderland 4-1, wakifunga mabao mawili kila kipindi, na mawili yakitiwa kimiani na Sergio Aguero ambaye sasa amefikisha mabao 19 msimu huu. Hiki ni kipigo cha kwanza kwa Sunderland katika mechi tano za ligi.
Sunderland ndio walioanza kupata bao, pale Connor Wickham alipowazidi maarifa kipa Joe Hart na beki wake, Pablo Zabaleta. Hata hivyo, Aguero alisawazisha kwa kiki kali kutoka yadi 16, Stevan Jovetic naye akampiga tobo kipa wao wa zamani, Costel Pantilimon kabla ya Zabaleta kusawazisha makosa yake kwa kufunga kwa kichwa mpira wa Aguero
ARSENAL WAPAMBANA KUPATA USHINDI
Arsenal wamefanikiwa kupata ushindi dhidi ya timu ngumu ya Southampton, bao likitiwa kimiani na Alexis Sanchez, kuwafikisha Washika Bunudki wa London katika nafasi ya sita, wakiwa pointi tatu nyuma ya Saints wanaoshika nafasi ya tatu. Saints hawajapata kushinda nyumbani kwa Arsenal kwenye mechi ya EPL na Jumatano hii walifanikiwa kupiga shuti moja tu kulenga lango.
Arsenal walipata bao dakika mbili tu kabla ya mechi kumalizika, baada ya kipa Fraser Forster kuwazuia Arenal kwa muda mwingi, licha ya mashambulizi mengi na aliokoa mabao ambayo yangefungwa na Danny Welbeck na Olivier Giroud. Alishindwa kumzuia Sanchez aliyefunga kutokana na majalo ya kiungo Aaron Ramsey. Sanchez amefikisha mabao 14 msimu huu kwa Arsenal.
Comments
Loading…