in , , ,

Manchester United, Liverpool washinda

Manchester United na Liverpool wameshinda na kupata pointi muhimu katika kipindi hiki, baada ya kuwa kwenye wakati mgumu mwanzoni mwa msimu wa ligi.

United sasa wameshinda mechi ya nne mfululizo, kitu kinachompa matumaini kocha Louis van Gaal, japokuwa anendelea kupatwa na majeruhi, ambapo sasa nahodha Wayne Rooney anachunguzwa na matabibu juu ya ukubwa wa jeraha lake la goti.

United waliwafunga Stoke 2-1 katika mchezo mkali, ambapo nusura Stoke wasawazishe dakika za lala salama, ambapo walikosa nafasi mbili za wazi, Van Gaal akapumua na kuwasifu vijana wake kwa kupambana hadi mwisho.

Kwa ushindi huo United wamebaki ndani ya timu nne za kwanza, wakiwa na pointi 25, nyuma ya Chelsea, Manchester City na Southampton. United waliokuwa wenyeji walipata bao la kuongoza kupitia kwa Marouane Fellaini aliyepokea mpira kutoka winga ya kushoto ya Ander Herrera katika dakika ya 21.

Stoke walijibu mapigo na kulitia shinikizo lango la United na Steven N’Zonzi alifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 39 lakini mkwaju wa adhabu wa Juan Mata katika dakika ya 59 ulizama kwenye nyavu na kuwaangusha Stoke.

Mchezaji wa zamani wa United, Mame Biram Diouf alijaribu mara mbili katika dakika za mwisho kusawazisha, lakini kipa David De Gea alijipinda kwa aina yake kuokoa kichwa alichokuwa amekipeleka nyavuni, wakati baadaye kidogo Ashley Young aliokoa mpira kwenye mstari wa goli.

LIVERPOOL WAMPA MATUMAINI RODGERS

Liverpool wameamsha matumaini licha ya kwamba walicheza na timu ndogo ya Leicester, ambapo wamepanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi. Kadhalika Liverpool inabidi wasishangilie sana, kwa sababu walicheza mchezaji mmoja zaidi ya jamaa hao walio chini katika msimamo wa ligi.

Nahodha Steven Gerrard alirejesha kujiamini kwake kwa sababu alifunga bao baada ya kurejeshwa kikosini. Liverpool walikuwa nyuma kwa bao ambalo kipa wao anayeelekea kuwa garasa, Simon Mignolet kujifunga dakika ya 22, lakini dakika nne tu baadaye, Adam Lalana akatikisa nyavu za adui.

Gerrard alifunga katika dakika ya 54 kabla ya Jordan Henderson kukomelea msumari wa mwisho dakika ya 83. Mignolet alijifunga kwa mpira wa mshambuliaji hatari wa Leicester, Leonardo Ulloa uliogonga mwamba, kisha ukakikuta kichwa cha kipa cha kipa huyo, naye akaingiza golini mwake.

Gerrard (34)ameshaachwa mara kadhaa kwenye kikosi cha kuanzia, ikiwa ni pamoja na kwenye mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid na pia kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Stoke, ambapo Liverpool walishinda 1-0.

Mkataba wake unamalizika na pamekuwapo shaka iwapo atapewa au yeye kukubali mwingine kwani alipata kusema kwamba anaweza kuhamia klabu nyingine. Baada ya mechi hii amesema kwamba atafanya uamuzi wakati mwafaka utakapowadia.

Katika matokeo mengine, Burnley walikwenda sare ya 1-1 na Newcastle, Swansea wakawachapa QPR 2-0, Crystal Palace wakazidiwa nguvu na Aston Villa waliowafunga 2-1 huku West Bromwich Albion nao wakiangukia pua kwa West Ham kwa kufungwa 2-1.

Ligi inaendelea Jumanne hii kwa Arsenal kuwakaribisha Southampton, Chelsea ni wenyeji wa wana London wenzao Tottenham Hotspur, Hull ni wageni wa Everton huku Sunderland waliowazuia Chelsea wikiendi hii wakisafiri kuchuana na Manchester City.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Brahimi mwanasoka bora Afrika

Chelsea, Man City, Arsenal waua