*Ni kupisha kujengwa upya Stamford Bridge
*Uwanja utatanuliwa kuchukua watu 60,000
*Wawazidi dau Spurs waliotoa pauni milioni 8
Mabingwa wa England, Chelsea wameomba kuhamia Uwanja wa Wembley kwa misimu mitatu kwa ajili ya kupisha upanuzi wa ule wao wa Stamford Bridge.
Matajiri hao wa London wametoa ofa ya pauni milioni 11 kwa Bodi ya Wembley ili kuwaruhusu kuhamia hapo kwa mechi kuanzia 2017 na kuwapiku Tottenham Hotspur waliotoa ofa ya pauni milioni nane.
Kwa kutoa ofa kubwa zaidi ya wenzao wa London, Chelsea wana nafasi kubwa zaidi ya kuhamia Wembley na Bodi ya Ligi Kuu imekuwa ikiishinikiza ile ya Wembley kutoa uwanja huo kwa moja ya klabu hizo.
Chelsea wanajenga upya uwanja wao ili uweze kuchukua watu 60,000 kwa gharama ya pauni zaidi ya milioni 500, ambapo Septemba mwaka huu wanatarajia kufanya mashauriano rasmi ya wazi juu ya mipango yao hiyo.
The Blues wanatarajia kuwasilisha maombi rasmi mbele ya Baraza la Halmashauri ya Hammersmith & Fulham ili wapate ruhusa kwenda na mpango wao.
Inatarajiwa kwamba ruhusa hiyo itatolewa kiangazi cha mwaka kesho, ujenzi uanze baada ya hapo na ifikapo 2020 watarejea tena Stamford Bridge.
Bilionea Roman Abramovich amepania uwanja wake huo mpya uwe bora kuliko yote nchini akiuita ‘Cathedral of Football’.
Uwanja wa Wembley unachukuliwa kuwa wa taifa na una uwezo wa kuchukua washabiki 90,000 lakini klabu itakayopangishwa hapo haitatakiwa kuvuka washabiki 50,000 kutokana na masharti yaliyowekwa.
Wembley hutumiwa kwa shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na matamasha ya muziki. Uwanja mpya wa Chelsea utakuwa na vitu kama minara na usanifu mithili ya Kanisa la Westminster Abbey.
Katika kutafuta uwanja wa kuchezea misimu hiyo mitatu, Chelsea wamepata kuwasiliana na Umoja wa Rugby ya Soka kwa ajili ya kutumia uwanja wao wenye kuchukua watu 82,000 ulioko Twickenham.
Hata hivyo, kulikuwa na vikwazo kadhaa ikiwa ni pamoja na kutakiwa kuwasilisha kwanza kibali cha mpango wao wa Stamford Bridge lakini pia wakazi wa eneo hilo walipinga suala hilo.
Ikiwa watapewa Wembley kwa misimu hiyo mitatu, patakuwa pazuri zaidi licha ya kwamba upo nje ya eneo lao la asili.
Kutoa kwao ofa kubwa kunawafanya Spurs kusawajika, kwani ndio walitangulia kutoa ofa ya pauni milioni nane bila kujua wenzao walikuwa wakiwasubiri.
Spurs walipewa ruhusa ya kukarabati uwanja wao wa White Hart Lane ili uchukue watu 56,000 lakini sasa wanataka kuomba kibali kipya ili waongeze viti hadi 61,000, ambapo pia utatumika kwa ajili ya mechi za ‘American football’.
Hivi sasa Spurs chini ya Mwenyekiti Daniel Levy wanakuna vichwa juu ya wapi pa kucheza, moja ya maeneo ambayo yangewezekana ni kutumia Uwanja wa Olimpiki pamoja na West Ham kwa miaka miwili.
Uwezekano mwingine ulikuwa kuzungumza na West Ham kwa ajili ya kutumia uwanja wao wa Upton Park kwani wanatarajia kuondoka hapo kwenda huo mkubwa wa Olimpiki.
Hata hivyo, mipango yote hiyo imeelezwa kwamba haitawezekana na sasa linaloonekana huenda likawa ni kutumia uwanja mmoja na Milton Keynes Dons, maarufu zaidi kama MK Dons.