in , ,

Sterling aonesha jeuri

*Akataa kusafiri na Liverpool, City wachekelea
*Anfield wanawaendea Benteke na Lacazette
* Schneiderlin Man U, Casillas kwenda Porto

Mipango ya msimu mpya kwa Liverpool imechukua sura mpya baada ya mshambuliaji wao kati, Raheem Sterling kuwakatalia kwenda nao ziarani.

Sterling, 24, anayetakiwa na Manchester City amemwambia kocha Brendan Rodgers kwamba hatakwenda na timu ziarani Australia wala Asia ya Kusini Mashariki.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England amekataa kusaini mkataba mpya Anfield licha ya kupewa ofa ya mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki.

Alieleza nia yake ya kwenda kucheza katika klabu inayotwaa makombe, akikana kwamba ni mroho wa fedha na sasa anasema hayupo sawa kisaikolojia kusafiri na kikosi hicho.

Wakati Sterling amepanga kubaki nyumbani wakati wenzake wakijiandaa kwa safari ya mwisho wa wiki kwenda kujiandaa na msimu mpya, Manchester City wanadaka fursa hiyo kwa kutoa ofa mpya ya pauni milioni 50 ili wamsajili.

Man City walikataliwa ofa yao ya awali ya pauni karibu milioni 40, wakiambiwa kwamba mchezaji huyo hauzwi lakini kutokana na mwenyewe kuonesha jeuri na uwezekano wa kuja kuondokam kama mchezaji huru wanaweza kumuuza kwa bei kubwa.

Sterling alikutana na Rodgers kwa mazungumzo baada ya kurudi kutoka mapumziko. Alimwambia kocha kwamba si kwamba anataka kuondoka Anfield tu, bali pia hatasafiri na wenzake.

Liverpool watacheza na Thai All Stars jijini Bangkok Jumanne ijayo kabla ya kwenda Brisbane na Adelaide, kisha kucheza mechi moja nchini Malaysia wakati wakirudi nyumbani.

Kabla ya kwenda likizo, Sterling aliambiwa wazi kwamba anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaokwenda ziarani, lakini sasa huenda ikawa ngumu kumlazimisha.

Liverpool wanaendelea kutafuta mbadala wa Sterling iwapo ataondoka, na baada ya kuwasiliana na Aston Villa ili kumsajili Christian Benteke, 24, wameambiwa kwamba watatakiwa kulipa pauni milioni 32. Wanadhaniwa watakubaliana na Villa.

Liverpool pia wanafikiria kumsajili mshambuliaji wa Lyon, Alexandre Lacazette, 24. Tangu kumuuza Luis Suarez Barcelona Liverpool wamebaki kuteseka kwenye safu ya ushambuliaji.

Manchester United wanaamini kwamba watampata kiungo Mfaransa wa Southampton, Morgan Schneiderlin, 25, kabla ya safari yao ya Marekani Jumatatu ijayo. Walikataliwa ofa ya awali, ambapo kocha Ronald Koeman alisema ilikuwa kama utani kwao.

Aliwataka United kufanya uamuzi mapema kwa sababu vinginevyo atabaki kuwa mchezaji wao licha ya mchezaji mwenyewe kuonesha nia ya kuhamia Old Trafford. Koeman alisema ni hali ngumu kwa mchezaji katika mazingira ya sasa.

Manchester City wamewakubalia Roma ombi la kumnunua mshambuliaji wao raia wa Bosnia, Edin Dzeko, 29, lakini watatakiwa kutoa pauni milioni 20, suala ambalo Roma wanalitafakari bado.

Crystal Palace wamefikia makubaliano na Paris Saint Germain (PSG) ili kumchukua kiungo Yohan Cabaye, 29, lakini sasa ni juu ya Mfaransa huyo kuamua iwapo atakubali kuondoka wiki ijayo kwa ada ya pauni milioni 12.
Palace pia wanakaribia kumnasa mshambuliaji wa kati wa QPR, Charlie Austin, 26. 
Tetesi kutoka Hispania ni kwamba kipa Iker Casillas, 34, amekubali kuondoka Real Madrid na kujunga na Porto – ikionekana ni kuacha njia nyeupe kwa raia mwenzake wa Hispania anayekipiga Manchester United, David De Gea, 24, kuchukua nafasi yake Bernabeu. 

Real Madrid wameonesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa PSG kutoka Sweden, Zlatan Ibrahimovic, 33. 
Manchester United wamekubaki kulipa ada ya pauni milioni 12 kumsajili beki wa kulia wa Italia, Matteo Darmian, 25.) 

Mshambuliaji wa Fluminense, raia wa Brazil, Kenedy, 19, amefanyiwa vipimo vya afya jijini London tayari kujiunga na Chelsea kwa ada ya pauni milioni 6.3.

Tottenham wanakaribia kukamilisha usajili wa mchezaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Toby Alderweireld kwa pauni milioni 11.5 kutoka Atletico Madrid. Alikuwa Southampton kwa mkopo msimu uliopita.

Kuna utata juu ya sababu za Saints kunyimwa fursa ya kwanza ya kumchukua kulingana na mkataba wao. Walipanga kufungua kesi lakini sasa inaelekea watapewa sehemu ya fedha hizo za usajili.

Kocha wa zamani wa Chelsea, Claudio Ranieri, 63, amesema yupo tayari kujiunga na Leicester City ambao hawana kocha kwa sasa.

Winga wa Manchester United, Nani, 28, amewasili katika klabu yake mpya ya Fenerbahce kwa ada ya pauni milioni 4.25. alilakiwa na mashabiki wengi uwanja wa ndege wakiwa na maua kuonesha upendo wao kwake.
Mchezaji huyo wa Ureno amefunga mabao 40 katika mechi 229 alizochezea United tangu 2007 aliposajiliwa kutoka Sporting Lisbon.
 
Msimu uliopita alirudi huko kwa mkopo, lakini akakataa kubaki, akitaka kwenda United ambako hakupata nafasi zaidi ya kuuzwa. Huko Istanbul atakutana na Wareno wenzake, Raul Meireles na Bruno Alves.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Mayweather avuliwa ubingwa WBO

Chelsea kuhamia Wembley