in , , ,

CAMEROON MABINGWA WAPYA AFRIKA

Cameroon wameibuka mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) baada ya kuwafunga Misri kwa mabao mawili kwa moja katika mchezo uliopigwa ndani ya dimba la d’Angondjé jijini Libreville usiku wa Jumapili.
Misri ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hii walikuwa wanajaribu kunyakua taji la nane na walitawala mno mchezo kwenye dakika za mwanzoni. El-Said alipata nafasi nzuri ya kufunga bao lakini shuti lake liliokolewa vyema kabisa na mlinda mlango wa Cameroon Fabrice Ondoa.

Mafarao wakapata bao la kuongoza kupitia kwa Mohamed Elneny anayekipiga katika Klabu ya Arsenal ya nchini Uingereza. Kiungo huyo alifunga ndani ya dakika ya 22 baada ya kuanzisha shambulizi na kuingia ndani ya eneo la hatari ambapo alipokea pasi nzuri na kupiga shuti lililomshinda Fabrice Ondoa na kuzama wavuni.

Cameroon wakapata pigo jingine dakika chache baadae baada ya mlinzi wao tegemeo Adolphe Teikeu wa Sochaux ya Ufaransa kupata majeraha yaliyomlazimisha kutolewa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Nicolas Nkoulou.
Vijana hao wanaonolewa na mwalimu Hector Cuper waliendelea kuutawala mchezo na kuonesha ubora wa hali ya juu kwenye eneo lao la ulinzi kila mara Cameroon walipopata mpira na kujaribu kupenyeza mashambulizi.

Cameroon walianza kurejea mchezoni kwenye kipindi cha pili na wakapata bao la kusawazisha ndani ya dakika ya 58 ya mchezo. Ni Nicolas Nkoulou aliyefunga bao hilo maridadi baada ya kuruka juu zaidi ya walinzi wa Misri na kuutia wavuni mpira ule ulioingizwa kwa krosi na Benjamin Moukandjo.

Bao hilo liliamsha ari ya kikosi hicho na wakapeleka mashambulizi zaidi kwenye lango la Misri wakichezea nafasi kadhaa za mabao. Dakika zilivyozidi kusogea kila upande ulicheza kwa tahadhari kuepuka kuruhusu bao ambalo lingeweza kuwakosesha ubingwa.

Mchezo ulionekana ukielekea kwenye dakika 30 za ziada. Lakini zikiwa zimesalia dakika chache kabisa Vincent Aboubakar alifunga bao safi kabisa lililowaangamiza Misri na kuwapa Cameroon ubingwa wao wa tano wa michuano hii.

Mshambuliaji huyo anayechezea Besiktas ya Uturuki alifunga bao la kukumbukwa baada ya kupokea kwa kifua mpira mrefu uliopigwa na Sebastien Siani na kisha kuuinua juu ya mlinzi wa Misri aliyejaribu kuuchukua na akamalizia kazi kwa shuti kali lililotinga wavuni moja kwa moja na kumuacha mlinda mlango Essam El-Hadary akitazama tu.

Bao hilo ndilo lililoipa ubingwa kikosi cha Cameroon kilichoonekana kuwa kikosi dhaifu zaidi cha Cameroon kikilinganishwa na vile vya miongo kadhaa ya nyuma. Huu ni ubingwa wa kwanza kwa Cameroon kwenye michuano hii tangu ule waliotwaa mwaka 2002.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KUELEKEA KWENYE MECHI YA CHELSEA NA ARSENAL

Tanzania Sports

NILCHOKIONA KWENYE BAADHI ZA MECHI ZA EPL ‘WEEKEND’ HII