in , , ,

BUSARA YA MATUMIZI IMEWAWEKA MAN CITY MAHALA WALIPO

Mara ya mwisho Manchester City kuzidiwa kiasi cha matumizi ya pesa za usajili na klabu za Ligi Kuu ya England kwenye dirisha kubwa la usajili ilikuwa ni kipindi cha majira ya joto ya mwaka 2014. Vipindi vya dirisha kubwa la usajili vya miaka mitatu iliyopita vimewashuhudia matajiri hao wa Etihad wakiongoza kwa matumizi ya pesa dhidi ya klabu zote za Ligi Kuu ya England.

Walitumia jumla ya paundi milioni 153.5 kwenye majira ya joto ya 2015 wakifuatiwa na Manchester United waliotumia kiasi cha paundi milioni 108. Vinara hao wa Ligi Kuu ya England wakatoa mfukoni jumla ya paundi milioni 174 kwenye majira ya joto 2016 mbele ya Manchester United waliotumia takribani paundi milioni 150.

Kiasi cha paundi milioni 212 kiliteketezwa na matajiri hao kwenye dirisha kubwa lililofuata la mwaka 2017.
Wakati mwingine yanaweza kuonekana kuwa ni matumizi ya hovyo ya pesa. Lakini Pep Guardiola juzi alisema kuwa kuna viwango fulani vya pesa ambavyo hutumika na klabu kubwa nyingine kwa ajili ya mchezaji mmoja lakini Manchester City hawawezi kuvitumia kusajili mchezaji mmoja kwa sasa. Alisema City kwa sasa hawawezi kusajili mchezaji mmoja kwa paundi milioni 80. Hapa anastahili kurekebishwa. Si kweli kuwa hawawezi. Ni kwamba hawataki kufanya hivyo.

Paundi milioni 55 ndicho kiasi kikubwa zaidi cha pesa kilichowahi kulipwa na klabu hiyo kwa ajili ya mchezaji mmoja. Manchester United wanao Paul Pogba, Angel Di Maria na Romelu Lukaku waliowahi kuwasajili kwa zaidi ya kiasi hicho cha pesa. Liverpool wamemsajili Virgil van Dijk kwa pesa nyingi zaidi. Alvaro Morata wa Chelsea pia amesajiliwa kwa zaidi ya paundi milioni 55 za De Bruyne.

Ukitazama vizuri namna Manchester City ilivyotumia vyema pesa kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu huu unaoendelea utagundua kuwa matumizi yaliyofanywa na klabu hiyo chini ya Guardiola yalikuwa ya busara mno. Manchester City walikuwa wakipigania kuimarisha eneo la walinzi wa pembeni wakati klabu nyingi kubwa zikihangaika kupigania saini za wachezaji aina ya Neymar, Coutinho, Morata, Lukaku, Kane na wengine.

Guardiola alifahamu vizuri namna alivyotakiwa kutumia pesa za mafuta. Isingekuwa busara Manchester City kutumia paundi milioni 80 kwa mchezaji mmoja aliye wa moto sokoni kutokana na namna anavyoshindaniwa na vilabu vikubwa na pia kupambwa na vyombo vya habari wakati klabu hiyo ilikuwa na mahitaji ya muhimu zaidi. Wengi tunaligundua hili sasa lakini ni wazi Pep Guardiola na bodi ya Manchester City ililiona tangu mwanzo.

Takribani paundi milioni 130 zilitumika na Manchester City kwa ajili ya walinzi wa pembeni tu kwa ajili ya kujiandaa na msimu huu. Pesa hizo ziliwasajili mlinzi wa kushoto Benjamin Mendy kutoka Monaco aliyelipiwa paundi milioni 52, mlinzi wa kulia Kyle Walker kutoka Spurs aliyesajiliwa kwa paundi milioni 50 na Danilo aliyejiunga akitokea Real Madrid kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 27.

Siku za ubora za walinzi wa pembeni Bacary Sagna, Pablo Zabaleta, Gael Clichy na Aleksandar Kolarov zilishapita na hawakuwa tena kiwango kinachotosha kuibeba klabu ya hadhi ya Manchester City. Pep alilijua hili na ndio maana hakusita kutumia kiasi cha paundi milioni 130 kuimarisha eneo la walinzi wa pembeni lililokuwa dhaifu na kuwa moja ya sababu kuu zilizomfanya ashindwe kung’ara kwenye msimu wake wa kwanza ndani ya Ligi Kuu ya England.

Kyle Walker, Benjamin Mendy na Danilo wameongeza kitu kikubwa kwenye klabu. Kasi walizo nazo kutokana na kuwa na umri mdogo zinawawezesha kupandisha vyema mashambulizi na kuwahi mara moja eneo la nyuma kila wanapohitajika. Wameifanya Manchester City kucheza kama timu ya Guardiola kweli kweli. Busara ya kutumia pesa imewafanya City kuwa hapa.

Klabu yako inapokuwa ndio kinara wa kufunga mabao mengi zaidi mbaka sasa kwenye ligi tano kubwa za Ulaya ukiwatoa PSG pekee bado unahitaji kutumia mapesa mengi kukidhi ada ya uhamisho na madai ya kipuuzi ya mshahara ya Alexis Sanchez? Unazo pesa nyingi mno lakini busara ya matumizi ya pesa inakataza jambo hili. Busara hiyo imewafanya vinara hawa wa Ligi Kuu ya England wamkose Alexis Sanchez. Lakini ni vyema na salama zaidi kusema kuwa Alexis Sanchez ndiye aliyeikosa Manchester City.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SANCHEZ KURUDISHA HESHIMA YA JEZI NAMBA 7?

Tanzania Sports

Pierre- Emerick Aubameyang: alikaribia kutua Newcastle Utd