Sikumbuki mara ya mwisho wadau wa soka kuacha kutoa lawama kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) juu ya maendeleo mbalimbali ya michezo.
Ilikuwa tangu zamani Taasisis hii ikiitwa ‘FAT’ na sasa imebadilika na kuwa TFF, viongozi wengi wamepita hapo kila mmoja akifanya yake, lengo la kila mmoja kuusogeza soka mbele ila mipango haipo thabiti ndio maana lawama zipo nyingi.
Nimeitaja bodi ya ligi kwakuwa nao wanahusika katika kupanga ratiba hivyo wanaweza kutoa ushauri kwa wahusika.
Tuanzie na hili la sasa ambalo linajadiliwa na aliyelianzisha kocha wa Ruvu Shooting Charles Boniface Mkwasa juu ya ratiba ya kucheza saa nane mchana wachezaji wanachoka kwa maoni yake hakulalamika.
Ifahamike kuwa Mkwasa hakulalamika ila ametoa maoni sasa mie natambaa naye humo humo.
RATIBA YA BODI YA LIGI
Bodi ya ligi kupanga ratiba inayowapendelea Yanga na Simba hili jambo limekuwa sugu japo katika ratiba hata mdhamini wa kurusha matangazo anahusika kuangalia biasara yake kwa timu hizo mbili.
Siku moja nilisema ukizaliwa Tanzania utakuwa Simba au Yanga hilo halina ubishi na hata upangaji ratiba hizi unaashiria dhahiri kuwa wapenzi wengi wa soka wanazipenda timu mbili tu, ndio maana ratiba yao inakuwa raha mustarehe!
Mjadala uliopoa kwanini Yanga na Simba hazichezi muda wa saa nane mchana kama zilivyo timu nyingine ambazo zinafanya hivyo?
Wengine wanaenda mbali zaidi wanasema kwanini Yanga na Simba zinapoendaa viwanja vya Mtibwa Sugar, Azam FC, Ruvu Shooting na Mwadui FC uwanja unabadilishwa ?
Zamani ilikuwa Mwadui Complex zinapoenda hizi timu mbili mechi zinarudi uwanja wa Kambarage ila timu nyingine zote zinachezwa Mwadui Complex.
Zinapoenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar zinabadilishiwa uwanja kutoka Turiani au Gairo zinapelekwa Jamhuri uliopo Morogoro mjini ila timu zilizobaki inacheza huko huko Turiani au Gairo ambapo ndiko maskani ya Mtibwa Sugar.
Huku mchezo wa Azam ambao Wanarambaramba wana uwanja wao kule Azam Complex ila inapokuja swala la Simba na Yanga ngoma inapigwa Uwanja wa Mkapa.
Ukiachalia hayo hii ratiba ya saa nane imekuaje wacheze wengine hawa watani wajadi wanacheza saa kumi.
Kama kigezo wafanyakazi wanatoka saa tisa hivyo wakicheza saa nane watakosa watu kwani Ruvu Shooting hawana mashabiki watakaotaka kuangaliampira wao.
Japo ukweli ni kwamba Yanga na Simba ndio kila kitu katika soka lakini wanashindwaje kuweka mambo sawa.
Ratiba za saa nane mchana kule wanakotazama au kuiga mambo timu zote zinacheza muda huo.
Sasa iweje hawa wenzetu washindwe kufikia maamuzi sahihi, ukiwauliza watakwambia Azam TV anataka ‘viewers’ wengi kutokana na muda huo kwa Yanga na Simba.
Arsenal katika mechi ya kufungua msimu huu walicheza saa sita na nusu kwa saa za kwao England huku kwetu ilikuwa saa nane na nusu, ni kweli kabisa utaratibu wao uko tofuati kutokana na ‘Fan base’ ya timu zao Fulham na Arsenal zote zipo London lakini kila timu ina mashabiki wake.
Kupendelea timu
Hii wala sijaithibitisha wala sijaiona ila walio wengi wanasema kuwa katika kila kipindi cha uongozi wanakuwa na timu zao, wanavyosema kipindi cha Jamal Malinzi aliipendelea sana Yanga kwakuwa ana mapenzi nayo na inafahamika kuwa anaipenda Yanga.
Kipindi cha Wallace Karia wengi wanasema kuna kaupendeleo kwa Simba kwakuwa naye anapenda Simba japo hajawahi kuweka wazi sehemu yoyote kama anapenda Simba, japo kuna wakati ilifanyika tamasha la viongozi na alioneka akiwana jezi za Simba akishiriki tamasha hilo akiwa upande huo.
Karia anapenda Coastal Union na Simba hilo liko wazi, ila katika kupendelea timu moja au nyingine hayo mawazo tu ya wadau wa soka ila kwa upande wangu naona anafanya vizuri.
Ila ndio ishakuwa malalamiko ya wadau wa soka juu ya kuboronga kwa michezo mbalimbali, wanatakiwa wajitathimini na warudi katika njia kama kweli iko hivyo.
Kuchelewesha adhabu
Kumekuwa na ucheleweshwaji wa kutoa adhabu pindi wachezaji wanapofanya makosa, kamati ya masaa 72 inapoteza maana yake halisi kutokana na tatizo la kutochukua maamuzi haraka.
Kamati hii inaweza kutoa maamuzi hata wiki mbili baada ya tukio, tena kama mchezaji wa Simba au Yanga anapokosea wakiangalia mbele kunamechi gani timu hizo zinacheza basi maamuzi yanaweza kukaa hata mwezi mmoja.
Mfano msimu uliopita Benard Morrison akichezea Yanga alimpiga mchezaji mwenzake kiwiko, huku Jonas Mkude wa Simba akifanya tukio kama hilo, adhabu zao zilikuja kutolewa baada ya mwezi kupita.
Tatizo hili linatakiwa likomeshwe haraka iwezekanavyo ili kila kitu kiende sawa.
Maoni ya Mwandishi
TFF inatakiwa kufanya maamuzi haraka iwezekavyo huku wajipange kuweza kupangua mambo mbalimbali yanayoendelea huku chini.
Uongozi wa juu ukianzia na Karia pamoja na Kidao wanatakiwa wajitathimini na wasichukulie poa maoni yanayotolewa na wadau ili kuangalia kama yana msingi wayaboreshe.
Naamini kila kiongozi anatamani mpira uende mbele wasife moyo juu ya maoni au kashfa mbalimbali zinazoendelea wazifanye kama changamoto kazini watamaliza vizuri kipindi chao.
Comments
Loading…