in , , , ,

Blatter, Platini wakwama lakini…

Rufaa za Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter na yule wa lile la Ulaya (Uefa), Michel Platini kupinga kusimamishwa kwao kujihusisha na masuala ya soka zimegonga mwamba katika hatua ya kwanza.

Blatter na Platini walikata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya Fifa baada ya Kamati ya Nidhamu ya shirikisho hilo kuwasimamisha kwa siku 90 huku wakichunguzwa juu ya kushiriki kwenye mlungula.

Platini amesema kwamba anawasilisha rufaa yake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS), ambapo wakili wake, Thibaud d’Ales, anasema kwamba wana imani chombo hicho ndicho kitamtendea mteja wake haki.

Platini anayetaka kuchukua nafasi ya Blatter kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari mwakani, anadaiwa kupewa hongo ya pauni milioni 1.35 na Blatter ili ajitoe kwenye uchaguzi wa rais wa Fifa miaka minne iliyopita.

Hata hivyo, wawili hao wanadai kwamba hawajafanya kosa lolote la jinai wala kuchepuka kimaadili, wakidai hayo yalikuwa malipo halali kwa Platini kutokana na kazi yake ya kuwa mshauri wa ufundi wa rais huyo.

Kinachotia ukakasi ni ukweli kwamba malipo hayo yalikuja muda mrefu baada ya Platini kuwa alishaacha kazi hiyo na muda mfupi kabisa kabla ya uchaguzi, ambapo baada ya malipo husika, Mfaransa huyo alijiondoa kugombea hivyo Blatter akapita kirahisi. Wakati kazi ilifanyika 1998 malipo yalitolewa 2011.

Platini anaumizwa zaidi na adhabu hiyo kwa sababu jina lake limesubirishwa katika mchakato wa uchaguzi wa Februari mwakani, na haijulikani mchakato utakapoendelea ikiwa siku hizo zitakuwa zimemalizika.

Mwanasheria wa Blatter kutoka Marekani, Richard Cullen, amesema kwenye taarifa yake kwamba Mswidi huyo amedhamiria kusafisha jina lake na anatumaini kwamba hata kama kutakuwapo ucheleweshaji, hatimaye haki itafanyika kwa chombo huru kumsikiliza.

Kamati ya Maadili inajiandaa kusikiliza mashitaka dhidi ya wawili hao kabla ya Krismasi, ambapo Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke naye alisimamishwa kazi Oktoba mwaka huu, lakini kwneye taarifa ya Fifa hapakuwa na chochote kilichoelezwa juu yake.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Soka yaunganisha Ulaya

Pongezi toka PSPF kwa Wabunge wetu….