Dunia imeshawahi kuwa na makipa wengi ambao macho yenu yalifurahia kuwatazama. Makipa ambao wana sanaa kubwa sana wakiwa langoni.
Kwa bahati mbaya hawa watu huwa hawathaminiwi kwa kiwango kikubwa kama wachezaji wa ndani.
Lakini ukweli unabaki pale pale kuwa golikipa ni mtu muhimu sana ndani ya timu husika. Hispania wanamtambua golikipa ndiye mshambuliaji wa kwanza.
Kwao wao yeye ndiye anayeanzisha mashambulizi. Yeye ndiye anayejua eneo gani muhimu ambalo linafaa kuanzisha mashambulizi ya timu.
Kwa kifupi yeye ndiye mtu ambaye anauona uwanja wote, anaona jinsi ya wachezaji wanavyojipanga wakati wa kujizuia na wakati wa kushambulia.
Ndiyo maana kuna wakati mwingine golikipa huonekana kama kiongozi wa kwanza kwenye timu. Kwa macho ya nyama ni ngumu sana kumtambua golikipa kama ndiye mtu wa muhimu kwenye timu.
Hawa ni watu muhimu sana kwenye timu. Watetezi wa mwisho wa timu. Kuna wakati timu inaweza ikawa imezidiwa kila eneo, mtu pekee ambaye anabaki anatazamwa kama mwokozi wa mwisho ni golikipa.
Ndipo hapo dunia inapomtambua Lev Yashin kama golikipa bora kuwahi kutokea duniani, golikipa mwokozi wa timu. Ndiyo maana anabaki kuwa kama golikipa pekee kushinda ballon d’or.
Italia imewahi kuwa na golikipa ambaye atakumbukwa sana tena sana kwa sababu ya alama ambazo amewahi kuziandika akiwa katika soka la Italia.
Italia inamtambua na kumheshimu sana Buffon kwa sababu alikuwa shujaa kwenye milingoti mitatu. Alijua kuilinda milingoti hiyo. Alijua kusimama kama mtu wa mwisho wa kubeba tumaini kwenye timu.
Kuna wakati timu inaweza kukosa tumaini, lakini yeye alikuwa anaibuka kama mtu wa mwisho kwa kuleta tumaini jipya ndani ya timu.
Ndipo hapo unaweza kuwakumbuka watu kama kina Iker Casillas golikipa bora kuwahi kutokea katika jiji la Madrid.
Katumia muda wake mwingi sana kuitetea Real Madrid, alisimama kwa ushupavu mkubwa sana. Mikono yake ilihakikisha kuna usalama mkubwa sana ndani ya kikosi cha Real Madrid.
Ndiyo maana anabaki kuwa golikipa bora kuwahi kutokea katika timu ya Realmadrid. Golikipa bora wa kizazi cha sasa ambaye aliwahi kuwavutia vijana wengi.
Leo hii David De Gea anaonekana kama mhimili katika timu ya Manchester United lakini Iker anabaki kama kioo ambacho David De Gea alikuwa anakitumia kujitazama.
Alimwangalia sana Iker, akawa anatumia muda mwingi kufikiria namna ambavyo anaweza kufika sehemu ambayo alipo Iker. Leo hii yuko Manchester United.
Klabu kubwa duniani, klabu ambayo anasimama kama mtetezi mkuu. Misimu mitano tangu atoke Sir Alex Ferguson. Timu imekuwa haina umbo la ushindani mkubwa kama kipindi ambacho yeye alikuwa anafundisha.
De Gea amebaki kama mchezaji ambaye anaitetea sana Manchester United kwenye nyakati zote ngumu. Huyu ndiye mchezaji ambaye ameipa Manchester United alama nyingi sana kwenye nyakati ngumu.
Kuna kipindi timu inakuwa haina uwiano mzuri, inaruhusu mashambulizi mengi . Mashambulizi ambayo huonekana ni hatari katika timu ya Manchester United, lakini David De Gea husimama imara kutetea jahazi la Manchester United.
Kwa kifupi huyu ndiye huwa mtetezi wa mwisho kwenye timu baada ya watetezi wengine kushindwa kuitetea timu ya Manchester United.
Sifa zake hubaki katika eneo la juu na inawezekana ni mmoja ya wachezaji wanaopendwa sana na mashabiki wa Manchester United kwa sababu hutumia muda mrefu kuitetea timu yake katika nyakati ngumu.
Nyakati ambazo Yanga walikumbana nazo katika mechi dhidi ya Simba. Walishambuliwa muda mwingi wa mchezo.
Waliruhusu mashambulizi mengi langoni mwao na kuna wakati wachezaji wa Simba walipata nafasi nyingi za wazi.
Tumaini la Yanga lilikuwa dogo sana lakini Beno Kakolanya aliibuka na kubaki kuwa mchezaji pekee wa Yanga aliyetoa tumaini jipya ndani ya kikosi cha Yanga.
Mikono yake iliilinda vizuri Yanga, ikahakikisha kuwa hakuna ambaye anaweza kuiangamiza ngome ya Yanga kwa sababu ya ulinzi wake imara uliokuwa unapatikana kwenye mikono yake.
Leo hii anabaki kuwa mchezaji ambaye amesemwa sana na kuandikwa sana tangu mechi ya Simba na Yanga ilipomalizika kwa sababu tu mikono yake ilisimama kama wakili msomi katika kesi ngumu mahakamani.