*Afuata nyayo za Fergie, Ferdinand
Msimu wa Ligi Kuu ya England (EPL) unapoingia mwisho, habari za kustaafu zinaonekana kuwa nyingi.
Wakati wadau wakitafakari uamuzi uliochukuliwa kuwa wa ghafla na wa kushangaza wa kocha Sir Alex Ferguson wa Manchester United kujiuzulu, David Beckham naye ameachia ngazi.
Ni wakati ambao pia Rio Ferdinand aliyecheza chini ya Fergie United ametangaza kustaafu soka ya kimataifa ili aelekeze nguvu zake klabuni, baada ya kuongeza mkataba wa mwaka mmoja.
Kadhalika, ni msimu huu huu mmoja ambao aliyekuwa nahodha wa England, John Terry alitangaza kustaafu kuchezea timu ya taifa, lakini baada ya kashfa ya kutoa maneno ya kibaguzi kwa mchezaji mweusi, Anthony Ferdinand, mdogo wake Rio.
Ya Rio na Terry hayakuwashangaza wala kuumiza wengi, maana kwanza pamekuwa na upinzani mkali dhidi yao kutokana na tabia walizoonesha miaka au miezi ya karibuni.
Terry alipata kuonekana mara kadhaa aliumiza wachezaji na akaadhibiwa kwa kadi waamuzi walipomwona, kumtukana Ferdinand kuliwakasirisha wadau wengi, hivyo kwamba wanaona aheri akae pembeni.
Rio aliyesimama kidete na mdogo wake na pia kupiga kampeni dhidi ya ubaguzi, alijiharibia mwenyewe upenzi wa wadau kwa kukataa alivyoitwa timu ya taifa na kocha Roy Hodgson, baada ya kuwa amelalamika mwanzoni kwa kutoitwa na madai ya kocha kusema hatakaa aitwe.
Mbaya zaidi ni kwamba baada ya kukataa mwito kwa madai ya ugonjwa, Rio alipanda ndege na kusafiri hadi Ghuba ya Uajemi kuchambua moja kwa moja mechi ya England dhidi ya San Marino.
Lakini ya Fegie lilikuwa jambo la kushangaza, mtu aliyepata heshima ya kuwa kocha bora zaidi Uingereza, aliyeitumikia klabu hiyo ya Old Trafford kwa miaka karibu 27.
Leo hii David Robert Joseph Beckham (40) anayecheza Paris Saint-Germain (PSG) ametangaza kujiuzulu mwishoni mwa msimu, wakati bado PSG walikuwa wanataka aongeze mkataba juu ya ule wa miezi sita aliokuwa nao.
Beckham (38) anasema ametafakari na kuona kwamba baada ya mafanikio makubwa aliyopata kwenye soka katika klabu za nchi mbalimbali, ni wakati mwafaka kutundika daluga.
Beckham ni mtu maarufu duniani, anayeheshimika mno Uingereza, aliyetwaa ubingwa wa nchi tofauti nne akiwa na klabu ambazo ni Manchester United, Real Madrid, Los Angeles Galaxy na PSG.
Amechezea United mechi 356 na kufunga mabao 85 kati ya mwaka 1992 hadi 2003. Fergie alimpeleka kwa mkopo Preston North End kati ya 1994 na 1995, na huko alifunga mabao mawili baada ya kucheza mechi tano.
Nchini Hispania alitamba na Real alikofunga mabao 19 katika emchi 157 kati ya mwaka 2003 na 2007. Kuanzia hapo alikuwa Marekani akichezea Los Angeles Galaxy na amewafungia mabao 20 kwenye mechi 118.
Aliwafungia AC Milan mabao mawili alipowachezea kwa mkopo mechi 33 wakati sasa ndio kwanza alidhaniwa anapiga jaramba PSG ili asajiliwe upya.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ambaye ni shabiki wa kutupwa wa Aston Villa iliyonusurika kushuka daraja, amesema kwamba Beckham amekuwa mwanasoka mahiri katika kipindi kirefu.
Alipong’atuka Ferguson, Cameron alisema kwa utani kwamba huenda utakuwa wakati wa klabu yake hiyo kupumua dhidi ya kashikashi za Fergie na timu yake. Waliwafunga Villa majuzi na kuwaweka pabaya katika kushuka daraja, kabla ya Arsenal kuwahakikishia usalama kwa kuwashusha Wigan.
Comments
Loading…