in

Barcelona kumuuza MESSI au kumnunua LA MASIA

Barca

Bado nalifikiria kaburi la Johan Cruyff. Natamani leo hii niende mpaka sehemu ambayo alizikwa  Johan Cruyff nina amini nitakutana na nyufa kubwa kwenye kaburi la mzee huyu mwenye heshima kubwa kwenye mpira wa miguu duniani.

Akili yangu inawaza namna ambavyo jana Johan Cruyff alivyopata mateso makubwa akiwa ndani ya kaburi lake. Mateso ambayo yalimfanya atamani kutoka mpaka nje ya kaburi lake kwa sababu ya matokeo ya jana ya kufungwa goli 8-2 na Bayern Munich, ndiyo maana natamani kwenda kwenye kaburi lake kushuhudia nikiamini kuna nyufa juu ya kaburi.

Nyufa ambazo zimetokana na hasira. Hasira ambayo imesababishwa na Barcelona kutokufuata musings yake ambayo aliwahi kuiweka kabla hajaondoka duniani. Misingi ambayo aliamini itawafanya Barcelona wawe watawala wakubwa wa mpira wa miguu duniani.

Misingi ambayo iliifanya Barcelona kwenye miaka ya 2000 kuwa moja ya timu ambazo ulikuwa hutamani kukutana nayo. Ungetamani kuiona Barcelona ikicheza mechi dhidi ya kikosi cha pili cha Barcelona kuliko kuiona ikicheza mechi dhidi ya timu yako.

Barcelona ambayo ingekufanya mtumwa muda wote wa mchezo. Barcelona ambayo ingekufanya usiwe na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira , wao ndiyo walikuwa wanatamani kuwa na mpira muda wote.

Miguu yao waliiaminisha kuwa inastahili kuwa na mpira muda wote. Hii ndiyo Barcelona ambayo Johan Cruyff alikuwa anatamani kuiona kwenye maisha yake. Hii ndiyo Barcelona ambayo Johan Cruyff alitamani iwe hivi muda wote wa maisha.

Kalamu yake ya wino wa dhahabu ilitumika vyema kuandika ramani ambayo ingekuwa na nafasi kubwa ya kujenga nyumba imara ya Barcelona. Ramani hiyo iliitwa jina la La Marcia.

Ndiyo ramani ambayo Johan Cruyff aliamini itawafanya Barcelona kuwa watawala wa mpira wa miguu duniani. Alichokuwa anakiwaza Johan Cruyff wakati anachora ramani ndiho kilichotokea mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Barcelona ilikuwa haikamatiki kwa sababu ilikuwa na wachezaji wengi wazuri ambao walikuwa wametoka kwenye chuo cha La Masia. Wachezaji ambao walikuwa wanajua utamaduni wa Barcelona. Wachezaji ambao walikuwa na mapenzi ya dhati na Barcelona,  ndiyo wachezaji ambao walifundishwa kuupenda mpira wa miguu.

Walichukua kila aina ya kombe ambalo walishiriki. Ndicho kipindi ambacho dunia ilishuhudia mwanafunzi wa kwanza kutoka La Masia,  akishinda Ballon D’oo.

Ndicho kipindi ambacho dunia ilishuhudia wanafunzi watatu kutoka La Masia wakiingia kwenye tatu bora ya tuzo ya Ballon D’oor na tatu bora ya tuzo ya mchezaji bora wa FIFA.

Dunia ilishuhudia Lionel Messi , Xavi na Andres Iniesta wakiwa kwenye tatu bora ya tuzo hizi kubwa duniani. Wachezaji wote hawa walikuwa wahitimu wa chuo cha kuzalisha vipaji cha La Masia.

Dunia ilishuhudia mwaka 2010 Hispania ikicheza fainali ya kombe la dunia dhidi ya Germany michuano ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Africa nchini Afrika Kusini.

Hispania walishinda goli 1-0 dhidi ya Barcelona. Kushinda kwa Hispania kombe la dunia kilikuwa kitu kikubwa sana lakini kitu kizuri cha kuvutia ni kuona wachezaji 7 kutoka La Masia wakiwa kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona na mfungaji wa goli hilo alikuwa Andres Iniesta mchezaji kutoka La Masia.

Haya ndiyo maono ambayo Johan Cruyff alikuwa nayo. Barcelona walianza kutembea nje ya maono ya Johan Cruyff, badala ya kuwa klabu ya kuzalisha vipaji ikawa klabu ya kununua vipaji. Kitu ambacho kimekuwa kigumu kwao.

Wachezaji ambao wamekuwa wakinunuliwa ni aina ya wachezaji ambao hawajui utamaduni wa Barcelona. La Masia wameitelekeza.  Wachezaji nyota wameshaanza kuzeeka. Hawana nguvu tena.

Huu ndiyo muda sahihi ya kuachana na kina Lionel Messi , Gerard Pique , Luis Suarez , Rakitic na kufikiria namna gani ya kurudi kwenye maono ya Johan Cruyff, maono ambayo yalikuwa yanaonesha La Masia ndiyo kila kitu kwa Barcelona.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Fei Toto

Ikiwezekana ‘tumfukuze’ Fei Toto Ligi Kuu Bara

Eymael

Eymael Aponda Usajili Yanga