*Arsenal yang’ang’niwa na West Ham
*Chelsea yapigwa
*Man City safi
Ligi Kuu ya England iliendelea kutimua vumbi hapo jana ikiwa kwenye mzunguko wa 33 ambapo michezo saba ilipigwa kwenye viwanja tofauti.
Mchezo wa mapema zaidi kati ya West Ham na Arsenal ulizishuhudia nyavu zikitikiswa mara sita pale Arsenal walipotoa sare ya 3-3 dhidi ya wenyeji wao ndani ya dimba la Upton Park.
Andy Carroll ndiye aliyetumbukiza wavuni mabao yote matatu ya wenyeji huku yale ya Arsenal yakifungwa na Mesut Ozil, Alexis Sanchez na Laurent Koscielny aliyefunga bao la mwisho la kusawazisha mnamo dakika ya 70.
Manchester City wakawaongezea msiba Arsenal wikiendi hii baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya West Bromwich Albion kwenye mchezo wa baadae na kupunguza tofauti ya alama kati yao na Arsenal walio kwenye nafasi ya 3.
Manchester City waliandika mabao yao kupitia kwa Sergio Aguero na Samir Nasri huku lile la West Bromwich likitumbukizwa wavuni na Stephane Sessegnon. Sasa ni alama mbili pekee zinazozitenganisha Manchester City na Arsenal.
Kwingineko bao la Gylfi Sigurdsson liliwazamisha mabingwa watetezi Chelsea. Kipigo hicho kutoka kwa Swansea ni cha kwanza kwa Chelsea katika EPL tangu kuanza kunolewa na Guus Hiddink.
Chelsea sasa wana alama 44 wakiwa kwenye nafasi ya 10 nyuma ya Liverpool wenye alama 45 wakiwa na michezo miwili mkononi ambapo leo watakuwa uwanjani kukipiga na Stpke City kwenye dimba la Anfield.
Kwenye michezo mingine Aston Villa walipokea kipigo cha 2-1 kutoka kwa Bournemouth. Crystal Palace wakawalaza Norwich 1-0, Southampton wakipata ushindi wa 3-1 dhidi ya Newcastle huku Everton na Watford zikitoka sare ya 1-1.