in , , ,

ARSENE WENGER AAMBIWA:

*Unaua klabu yetu, ondoka*
*Nilishuhudia akitukanwa na wapenzi wenye hasira*
*Wamesahau mazuri yote aliyowafanyia ndani ya miaka 20*

Washabiki wenye ghadhabu wa Arsenal wamemwambia kocha wao, Arsene Wenger kwamba anawaulia klabu na hana budi kuondoka.

Kwenye mchezo ambao, niliushuhudia moja kwa moja toka uwanjani Emirates, hakika matusi yalikuwa mengi sana!!

Walishindwa kuvumilia baada ya kufadhaishwa nyumbani kwao Emirates walipopokea kichapo kingine cha 5-1 na kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa jumla ya mabao 10 -2 na Bayern Munich.

Kadiri ya washabiki 200 wa Arsenal waliandamana usiku nje ya dimba la Emirates wakiwa na mabango ya kutaka Mfaransa huyo aliyeshika usukani kwa miaka 21 sasa aondoke. Na hayo yametokea wakati nyota wao, Alexis Sanchez akidhaniwa kwamba ataondoka Arsenal kutokana na klabu kutotaka kumpa mshahara anaotaka wa karibu pauni 250,000 kwa wiki.

Ameahidiwa fedha nyingi nchini China, lakini pia klabu nyingine za ndani na nje ya England zinamhitaji kwa sababu yupo kwenye kiwango kizuri cha soka. Wananchi wa Chile walipata kuandamana kutaka mwana wao huyo aondoke Arsenal, wakidai amekuwa akiachiwa mzigo kuibeba timu hiyo tangu ajiunge.

katika hali ya kukata tamaa..

Sanchez aliyeondolewa kipindi cha pili kwenye mechi hiyo, alionekana akiwapungia washabiki wakati akitoka, na akifuatilia mechi hiyo kwenye benchi alionekana akicheka, kitendo kinachozua utata juu ya maana hasa ya yeye kufanya hivyo wakati timu walikuwa katika hali mbaya.

Huu ni msimu wa saba mfululizo kwa Arsenal kutolewa katika hatua hiyo wakati kwenye Ligi Kuu ya England nako wamepigwa mara kadhaa kiasi cha kuwashusha hadi nafasi ya tano. Kichapo cha karibuni kilikuwa cha 3-1 dimbani Anfield kutoka kwa Liverpool. Walifungwa pia na Chelsea, Watford na Everton. Liver waliwafunga mechi ya kwanza ya msimu kadhalika.

Wenger ambaye amekuwa mkuuhapo tangu Oktoba 1996 anaongoza England kwa kuwa kocha kwa muda mrefu zaidi kwenye klabu moja na alikuwa amepewa na uongozi muda hadi mwishoni mwa mwezi huu aweke msimamo wake juu ya kipi anakusudia kufanya baada ya mkataba wake kumalizika kiangazi hiki.

Inaelezwa kwamba tayari Arsenal wamepanga kumchukua kocha wa Juventus ya Italia, Massimiliano Allegri iwapo Wenger ataamua kuondoka. Licha ya Wenger, kuna dalili za kiungo Mesut Ozil – mchezaji ghali zaidi kwa Arsenal, kuondoka kwani naye anaingia kwenye kipindi cha mwisho cha mkataba wake na hakuna mazungumzo yaliyofanyika.

Wenger amepata kuwaambia washabiki na wadau wa Arsenal wasidhani kwamba akiondoka ndio watakuwa wakishinda kila mechi. Amesema ana uhakika wa kuwa kocha msimu ujao, iwe ndani au nje ya Arsenal, lakini ni Ulaya na kwamba amekataa dili kubwa nchini China.

Kabla ya mchezo kulikuwa na matumaini kidogo…

Mchezaji wa kikosi cha ‘The Invicibles’ chini ya Wenger 2003/4 ambacho hakikufungwa hata mechi moja msimu huo, Gilberto Silva amesema anaona kwamba ni wakati wa Wenger kuondoka Arsenal.

Hata hivyo, mlinzi wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amewaonya washabiki wa Arsenal kwamba ni hatari kwao Wenger kuondoka kuliko kubaki, akikumbukia hali mbaya United waliyokabiliwa nayo baada ya kuondoka kwa kocha mkongwe, Sir Alex Ferguson aliyeamua kung’atuka.

Beki wa kulia wa Arsenal, Hector Bellerin amewaomba washabiki msamaha rasmi kwa kadhia waliyowapa kwa kufungwa. Hata hivyo, Wenger amewapongeza wachezaji wake, akisema walionesha ujasiri wa aina yake kwenye mechi ambayo walinyimwa penati baada ya Theo Walcott kuangushwa na wapo kuadhibiwa penati na kutolewa nje nahodha Laurent Koscielny.

Katika mechi nyingine ya Ulaya, Real Madrid walifanikiwa kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Napoli na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 6-2.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE BAADHI YA MECHI WEEK-END HII

Tanzania Sports

NI MARA CHACHE KUSHUHUDIA USIKU USIO NA GIZA KAMA USIKU WA NOU CAMP