in , , ,

Arsenal watanua kileleni

*Man City, Man United tia maji tia maji
*Wafungwa kiaina na West Brom, Villa

 
 
Arsenal wamezidi kuongoza Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kupata ushindi, huku Manchester United na Manchester City wakipokea vichapo.

Vijana wa Arsene Wenger walifanikiwa kuibuka na ushindi ugenini baada ya kuwashinda Swansea kwa mabao 2-0 kwenye mchezo mkali na wa kukamiana katika dakika zote 90.
Kinda la Arsenal kutoka Ujerumani, Serge Gnabry (18) alichanua kwa kupata bao la kuongoza, akiwa mchezaji wa pili mdogo zaidi kufunga katika EPL, wa kwanza akiwa Cesc Fabregas aliyekuwa pia Arsenal.

Bao hilo lilitokana na jitihada za kiungo mpya kutoka Real Madrid, Mesut Ozil ambaye kabla ya mpira kumfikia mfungaji ulipitia kwa Bacary Sagna, Olivier Giroud, Jack Wilshere na Aaron Ramsey aliyempatia mfungaji.

Arsenal walipata bao la pili kupitia kiungo wake Mwingereza Ramsey aliyeendeleza kucheka kwake na nyavu msimu huu, lakini wenyeji nao walifuta machozi kwa bao la Davies.
Arsenal walicheza kwa umakini katika mechi hiyo ya mwisho kwa Jumamosi hii, baada ya kuwa wameona matokeo ya washindani wao awali, hivyo kumpa Wenger zawadi nzuri alipoadhimisha miaka 17 klabuni hapo.

KILIO MANCHESTER UNITED
 
Katika dimba la Old Trafford, Manchester United waliishia kulia, baada ya kufungwa na West Bromwich Albion, ukiwa ni ushindi wa kwanza wa timu hiyo dimbani hapo tangu 1978.
Kocha David Moyes anaelekea kuanza vibaya kazi yake hapo kwani wadau wengi walishawapa United ushindi hata kabla ya mechi kuanza.

West Brom wanaofundishwa na Steve Clark, kocha msaidizi wa zamani wa Liverpool, walitangulia kuwaliza washabiki wa Mashetani Wekundu kwa bao la Morgan Amalfitano aliyetupia mpira kambani akimwacha kipa David De Gea akiwa hana la kufanya.
Mshambuliaji wa Man U, Wayne Rooney alisawazisha kwa mpira wa ashabu, lakini West Brom walikomaa na kupata bao la ushindi kupitia kwa Berahino kabla ya jitihada za Marouane Fellaini kutupiliwa mbali kwa sababu ya kuotea.

Moyes alikiri kwamba timu yake haikucheza vizuri, ambapo wanaiweka klabu katika uanzaji mbaya zaidi wa ligi tangu msimu wa 1989/90.

Kichapo hiki kinakuja pungufu ya wiki moja tangu wachabangwe na Manchester City mabao 4-1 kwenye ligi hii, hivyo walihitaji sana pointi tatu, lakini sasa wamebakiwa na pointi saba baada ya mechi sita.

Baggies, kama wanavyoitwa West Brom hawajapata kuwafunga United tangu 1984 na katika dimba la Old Trafford walipata ushindi wa mwisho 1978.
 
MANCHESTER CITY NAO TIA MAJI
 
Kilio katika EPL hakikuishia kwa mabingwa watetezi Jumamosi hii bali kiliwahusisha pia miamba wenzao wa Manchester – Manchester City.

Vijana hawa wa Manuel Pellegrini, katika hali inayoshangaza pia, walikubali kipigo kutoka kwa Aston Villa ambao hawakuwa wakipewa nafasi yoyote ya kupata ushindi wala sare.
Wanazi wa Villa Park walijawa na furaha na pengine kocha wao, Paul Lambert hakuamini kilichotokea, hasa baada ya kutangulia kufungwa na Yaya Toure.

Hata hivyo, Karim El Ahmadi alifunga kwa mpira wa karibu na goli na kuwasawazishia Villa kabla ya Edin Dzeko kutikisa nyavu na kuwaweka mbele tena  City.

Villa walisawazisha kupitia kwa mpira wa adhabu ndogo wa Leandro Bacuna kabla ya Andreas Weimann kuwahakikishia wenyeji pointi tatu kwa kupachika bao muhimu la tatu.

Kocha Pellegrini alisema hawezi kuamini kwamba timu yake imefungwa wakati Villa umekuwa ushindi wa kwanza nyumbani msimu huu, wakifurahia zaidi kiwango kilichoonyeshwa na kiungo wao Bacuna aliyetoka FC Groningen.
 
UBABE CHELSEA, SPURS WATOA SARE
 
Katika mechi ya mapema Jumamosi hii iliyojaa ubabe ilishuhudia Chelsea wakiambulia pointi moja mikononi mwa Tottenham Hotspur.

Ilikuwa mechi ambayo wachezaji walikamiana, zaidi sana ikiwa baina ya Jan Vertonghen na Fernando Torres kwa muda mwingi wa mchezo kabla ya Torres kutolewa nje kwa kadi nyekundu alipokwenda angani sambamba na Mdachi huyo kuwania mpira na kudaiwa kumuumiza.

Ilikuwa mechi yenye hisia, ikimkutanisha Andre Villas- Boas nyumbani kwake na mwalimu wake, Jose Mourinho, huku Villas-Boas akiwa ameshasema kwamba hana urafiki na Mreno mwenzake huyo.

Villas-Boas amepata kuwafundisha Chelsea kabla ya kufukuzwa kazi na mmiliki Roman Abramovich kisha akapumzika kabla ya kuitwa Spurs kuchukua nafasi ya kocha Harry Redknapp aliyefutwa kazi.

Spurs walikuwa wa kwanza kupata bao Jumamosi hii katika dimba la White Hart Lane kupitia kwa Gylfi Sigurdsson ambalo lilikombolewa na Nahodha wa Chelsea, John Terry aliyefunga kwa kichwa.

Chelsea walionekana kupata nguvu baada ya kuingizwa kwa Juan Mata wakati wa mapumziko, ambapo Mourinho amekuwa akilaumiwa kwa kumwacha benchi Mhispania huyo. Bao la Chelsea lilitokana na mpira wake wa adhabu.
 
SAINTS, CARDIFF, HULL WASHINDA
 
Katika matokeo mengine, Southampton wanaojulikana kama Saints walifanikiwa kupata pointi tatu baada ya kuwakandamiza Crystal Palace mabao 2-0.

Cardiff City nao walitoka uwanjani wa ugenini kwa kicheko, baada ya kuwafunga Fulham kwenye dimba la Craven Cottage mabao 2-1.

Kocha Sam Allardyce ‘Big Sam’ alitoka uwanjani kwa masikitiko makubwa, baada ya timu yake ya West Ham United kukandikwa bao 1-0 na Hull waliopanda daraja msimu huu.

Kwa matokeo hayo, Arsenal wanaongoza ligi wakifuatiwa na Spurs, Chelsea, Saints, Man City, Liverpool, Hull, Everton, Villa, West Brom, Cardiff, Man United, Swansea, Stoke, Newcastle, West Ham, Norwich wakati tatu za mwisho ni Fulham, Crystal Palace na Sunderland.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

KOMBE LA LIGI ENGLAND, MZUNGUKO WA NNE….

Wakenya watamba Marathon Ujerumani