Arsenal na Chelsea wamepoteza mechi muhimu za makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), huku Arsenal wakiwekwa katika wakati mgumu zaidi wa kufuzu.
Wakicheza nyumbani Emirates, Arsenal walifungwa na Olympiakos 3-2, likiwamo bao la kujifunga mwenyewe la kipa David Ospina aliyeanza badala ya Petr Cech aliyesajiliwa kwa matarajio ya kusaidia Arsenal kwenye mechi kubwa kama hii.
Wamepoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kufungwa na Dinamo Zagreb ugenini kwenye mechi ya kwanza ya kundi lao, na bado wana mtihani wa mechi mbili baina yao na Bayern Munich.
Ulikuwa usiku mgumu kwa vijana wa Arsene Wenger, ambapo Ospina alijikuta akitumbukiza wavuni mwake kona iliyochongwa na Kostas Fortounis, dakika saba tu baada ya mshambuliaji Theo Walcott kusawazisha bao la Felipe Pardo. Alexis Sanchez alitia matumaini kwa bao la dakika ya 65 lakini Alfred Finnbogason akaongeza bao la tatu.
Wenger amedai kwamba bado wana nafasi ya kufuzu hatua ya mtoano ya mashindano haya makubwa Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia kwa Arsenal kupoteza mechi mbili za mwanzo.
“Matokeo haya yametuacha kwenye nafasi mbaya lakini bado tupo kwenye mchuano. Lazima tushinde mechi yetu ijayo dhidi ya Bayern Munich,” alisema Wenger aliyeonesha wazi kusononeshwa na matokeo hayo.
Katika mechi nyingine, Chelsea wakicheza ugenini nchini Ureno walichapwa 2-1 na Porto, timu aliyopata kufundisha Jose Mourinho, na pia huko ndiko nyumbani alikozaliwa kocha huyo mwenye tambo.
Chelsea walionesha kwamba bado wana tatizo kubwa, kwani wameendelea na kupwaya kwao tangu kuanza msimu huu. Waliruhusu bao la kwanza kupitia kwa Andre Andre aliyetia mpira kimiani baada ya kipa Asmir Begovic kuugonga mpira wa Yacine Brahimi.
Kiungo wa Chelsea, Willian alisawazisha wakati timu zikikaribia kwenda mapumziko lakini dakika saba ndani ya kipindi cha pili, Maicon akafunga bao la ushindi kabla ya Diego Costa kufyatua shuti lililogonga mwamba.
Cesc Fabregas na Pedro walimpa kazi ya ziada mchezaji mwenzao wa kimataifa wa Hispania, Iker Casillas aliyekuwa golini lakini akazuia jitihada zao. Casillas ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika mashindano hayo, baada ya kufikisha michezo 152.
Mourinho alishangaza kwa kumwacha benchi mchezaji bora wa mwaka jana aliyetangazwa na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), Eden Hazard, wakati yule aliyesajiliwa kwa mkopokutoka Monaco baada ya kushindwa kazi Manchester United, Radamel Falcao hakuwa hata kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.
Branislav Ivanovic alikuwa na wakati mgumu kwenye ulinzi, akipelekeshwa na Yacine Brahimi. Wachezaji wawili walioingizwa kipindi cha pili na kusawazisha dhidi ya Newcastle wikiendi iliyopita, Wabrazili Willian na Ramires – walicheza tangu mwanzo wa mchezo.
Katika matokeo ya mechi nyingine, Barcelona waliwapiga Bayern Leverkusen 2-1 kwa mabao ya Luis Suarez na Sergi Roberto, katika mechi ya kwanza kwa mabingwa hao kumkosa Lionel Messi anayetarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane baada ya kuumia.
Bayern Munich waliwakandika Dinamo Zagreb 5-0 na kutuma salamu kwa Arsenal watakaokabiliana nao kwenye mechi ijayo. Mabao ya Bayern yalitiwa kimiani na Robert Lewandowiski aliyepiga hat trick, Douglas Costa na Mario Gotze. Lewandowiski amefikisha mabao 10 katika mechi tatu za mashindano tofauti.
BATE Boir wakicheza nyumbani walifanikiwa kuwafunga Roma 3-2 wakati Maccabi Tel Aviv walipoteza mechi ya pili mfululizo walipolala nyumbani kwao kwa kufungwa mabao 2-0 na Dynamo Kiev. Lyon walishindwa kutumia vyema uwanja wa nyumbani walipofungwa 1-0 na Valencia wakati Zenit St Petersburg walishinda 2-1 dhidi ya KAA Gent.