in , , ,

YALIYOJIRI VIWANJANI LIGI YA MABINGWA

 

Ligi ya Mabingwa Ulaya hapo jana iliingia kwenye raundi ya pili ya hatua za makundi. Jumla ya michezo nane kutoka kwenye makundi manne ambayo ni Kundi E, F, G na H ilipigwa hapo jana kwenye viwanja tofauti. Haya hapa ni matokeo ya michezo hiyo nane ya hapo jana.

 

TIMU ZA ENGLAND ZAENDELEA KUCHEMSHA

Jose katika majonzi
Jose katika majonzi

 

Arsenal na Chelsea zote ziliambulia vipigo hapo jana. Arsenal ambao waliwakaribisha Olympiakos kutoka Ugiriki kwenye mchezo wa Kundi F walifungwa mabao matatu kwa mawili na kujikuta mkiani mwa kundi hilo wakiwa na alama sifuri.

Arsenal walifungwa bao la kwanza kwenye dakika ya 33 ambapo Felipe Pardo aliukusanya mpira wa kona na kupiga shuti lililomgonga Oxlade Chamberlain na kumpoteza golikipa David Ospina kabla ya kuingia wavuni.

Hazikupita dakika tatu Theo Walcott akasawazisha bao hilo baada ya kupokea mpira mzuri kutoka kwa Alexis Sanchez. Hata hivyo Olympiakos wakapata bao lingine la kuongoza dakika tano kabla ya kwenda mapumziko ambapo golikipa wa Arsenal David Ospina aliusukuma mpira ndani ya lango lake alipojaribu kudaka mpira huo uliotokana na krosi ya Kostas Fortounis.

Dakika ya 65 kwenye kipindi cha pili ilimshuhudia Alexis Sanchez akirejesha matumaini ndani ya uwanja wa Emirates baada ya kuwapatia Arsenal bao la kusawazisha akimalizia krosi ya Theo Walcott. Ni Alfred Finnbogason aliyefunga bao lililowazamisha Arsenal usiku huo wa jana akimalizia krosi ya Felipe Pardo kwenye dakika ya 66.

Kwingineko Bayern Munich wakiwa nyumbani waliendelea kujikita kileleni mwa kundi hili baada ya kuwazamisha Dinamo Zagreb kwa mabao matano kwa sifuri. Lewandowski alifunga hat-trick na mengine mawili yaliwekwa wavuni na Douglas Costa na Mario Gotze.

Chelsea wao wakiwa ugenini walifunzwa adabu kwa kipigo cha mabao mawili kwa moja kwenye mchezo wa Kundi G dhidi ya FC Porto. Porto walipata bao la kuongoza kupitia kwa Andre Andre aliyemalizia mpira ambao golikipa Asmir Begovic alijaribu kuuokoa kutokana na shuti lililopigwa na Yacine Brahimi.

Kiungo Willian ndiye aliyewasawazishia Chelsea zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kupitia mpira wa adhabu aliouweka wavuni moja kwa moja. Dakika saba baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Maicon akawafungia Porto bao la ushindi.

Kwenye mchezo mwingine wa kundi hili Dynamo Kyiv wakiwa ugenini waliwafunga Maccabi Tel Aviv mabao mawili kwa sifuri na kuwa vinara wa kundi hili wakiwa na alama nne sawa na FC Porto wanaoshika nafasi ya pili huku Chelsea wenye alama tatu wakikamata nafasi ya tatu.

 

HISPANIA KAMA KAWA

Suarez
Suarez

 

Klabu za Hispania zimeendelea kutesa kwenye michuano ya Ulaya baada ya Barcelona kutoka Kundi E na Valencia ya Kundi H kuibuka na ushindi kwenye michezo yao hapo jana. Barcelona ambao walikuwa wakikipiga bila ya nyota wao tegemeo Lionel Messi ambaye ni majeruhi walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Bayer Leverkusen kwenye dimba la Nou Camp.

Mabingwa hao watetezi walitanguliwa kwenye dakika ya 22 kupitia bao la kichwa lililofungwa na Kyriakos Papadopoulas. Sergi Roberto akawasawazishia kwenye dakika ya 82 kabla ya Luis Suarez kuwafungia bao la ushindi kwenye dakika ya 84.

Mchezo mwingine wa kundi hili ulikuwa kati ya BATE Borisov na AS Roma ambapo BATE waliibuka na ushindi wa 3-2. Kwa matokeo hayo Barcelona wanaongoza kundi hili wakiwa na alama nne wakifuatiwa na Leverkusen kisha BATE kila moja ikiwa na alama tatu. Roma wanaburuza mkia wakiwa na alama moja.

Valencia wao wakiwa nyumbani walishinda dhidi ya Lyon kupitia bao pekee la mchezo lililofungwa na Sofiane Feghouli. Wamepanda mbaka nafasi ya pili kwenye Kundi H nyuma ya  vinara Zenit St. Petersburg ambao jana waliwafunga Gent mabao mawili kwa moja.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MAWAKALA WA FORODHA TANZANIA WAJIUNGA NA PSPF

Tanzania Sports

Arsenal, Chelsea hoi Ulaya