Shirikisho la Soka la Algeria limetangaza kusitisha michuano ya Ligi Kuu hadi itakapotangazwa vinginevyo, kutokana na mchezaji kuuawa kwa kupigwa jiwe dimbani.
Mchezaji huyo wa Cameroon aliyekuwa akichezea klabu ya JS Kabylie, Albert Ebosse alipoteza maisha akiwa hospitalini Jumamosi baada ya washabiki wa timu yake kurusha vitu uwanjani kwa kutoridhishwa na mchezo wa wachezaji wao.
Wakicheza nyumbani Tizi Ouzou, Kabylie walifungwa 2-1 na USM Alger, na shirikisho lililokaa Jumapili hii limeamua kusitisha ligi pamoja na kuufunga uwanja huo kwa muda usiojulikana.
Kwa muda sasa pamekuwa pakitokea vurugu kwenye mechi na wakati mwingine kuendelea hadi mitaani kiasi cha kujenga mazingira ya woga na ukosefu wa usalama.
Shirikisho limesema hatua hiyo inalenga kuwanyamazisha wahuni wanaotaka kuchafua soka, na kwamba linafikiria kuchukua hatua zaidi, ikiwa ni pamoja na klabu itakayotiwa hatiani kufutwa kwenye mashindano yote.
Katika kuipoza familia ya Ebosse, shirikisho limesema kiasi cha dola za Marekani 100,000 kitapewa familia hiyo pamoja na kiwango ambacho angepata iwapo angecheza hadi kumaliza mkataba wake wote na pia wachezaji wa Kabylie wataichangia mshahara wa mwezi mmoja mmoja.
Wizara ya Mambo ya Ndani tayari imetangaza kuanza kwa uchunguzi wa kina juu ya matukio yaliyosababisha kifo hicho pamoja na matukio ya vurugu katika soka kote nchini kwa ujumla. Wakati wa mechi, uwanja huo ulikuwa katika matengenezo, hivyo ikawa rahisi kwa washabiki kuokota mawe yaliyokuwa yamezagaa na kuwarushia wachezaji.
Moja ya maswali muhimu katika uchunguzi huo ni kulikoni uwanja ukatumika wakati ulikuwa katika matengenezo. Mechi hiyo ilikuwa ya pili tu katika msimu mpya wa ligi.
Comments
Loading…