*Ni za kuwanasa Pogba na John Stones
*Real Madrid bado wamuwinda De Gea
*Nicolas Otamendi rasmi Man City
Baada ya Chelsea kuanza vibaya msimu wa 2015/16 wa Ligi Kuu ya England (EPL), mmiliki wa klabu hiyo, bilionea Roman Abramovich ameamua kutenga pauni milioni 100 ili kocha Jose Mourinho aimarishe kikosi.
Chelsea walioanza kwa sare ya 2-2 na Swansea kisha kuchapwa 3-0 na Manchester City wamejaribu mara tatu kumsajili mlinzi wa Everton na England, John Stones lakini ofa zao zilizopanda hadi pauni milioni 30 zilikataliwa, Everton wakidai hawamuuzi.
Hata hivyo, sasa wameamua kumfungia kazi, ambapo kwa ujumla zimetengwa pauni milioni 100 ili pia kumpata mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa, Paul Pogba ambaye awali Mourinho alidai hana uwezo wa kumsajili, akimfananisha na Mnara wa Eiffel ulioko Paris, usioweza kuingia nyumbani kwake.
Kadhalika hivi karibuni kocha huyo alinukuliwa akifananisha ukimya wa Chelsea katika kusajili na mtu anayechezea shilingi katika tundu la choo, akisema ingeweza kuwa ngumu kutetea ubingwa wao msimu huu.
Hadi sasa wamemsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Monaco, Radamel Falcao, ambaye alicheza pia kwa mkopo Manchester United msimu uliopita.
Kadhalika wamewapiku United na kumsajili Pedro kutoka Argentina sambamba na Baba Rahman wa Augsburg na kipa Asmir Begovic kutoka Stoke.
Chelsea wanafikiria kwamba Juventus watapokea pauni milioni 60 ili wamwachie Pogba aingie Stamford Bridge. Pogba alipata kucheza Manchester United, lakini kocha Sir Alex Ferguson alimtupia virago akidai hana kiwango, ila kwa sasa anasifika kote duniani kwa ubora wake kwenye kiungo.
Kiasi kilichobaki au pungufu kinatarajiwa kuelekezwa Everton, kwa ajili ya kumpata Stones. Kadiri dau linavyopandishwa ndivyo uwezekano wa kumnasa unakua, kwani litawashawishi Toffees kumuuza ili wanunue mchezaji mwingine na pia kubaki na faida kibindoni.
Inatarajiwa kwamba Stones ameshawishiwa awaambie Everton kwamba anataka kuondoka, hatua itakayosaidia kuongeza shinikizo kwa uongozi wa klabu hiyo kukubali dau la Chelsea.
Chelsea walimwachia kipa wao, Petr Cech kujiunga na mahasimu wao wa London, Arsenal na sasa wanatarajiwa kumuuza mchezaji waliyemsajili kiangazi kilichopita tu, Juan Cuadrado na Oscar ambaye huenda akahamia Italia.
REAL MADRID BADO WAMUWINDA DE GEA
Katika hatua nyingine, Real Madrid waliowakatalia Manchester United kumpata beki wa kati Sergio Ramos, wanakuja kivingine kutaka kumsajili kipa namba moja wa Old Trafford, David De Gea.
Madrid wanataka kutoa kiasi cha fedha, lakini pia kuwapa United kipa wao, Keylor Navas, ambaye pia ni wa kimataifa wa Costa Rica, kabla ya mwisho wa dirisha hili la usajili kufungwa.
De Gea hakucheza mechi mbili za mwanzo msimu huu, baada ya kocha Louis van Gaal kudai kwamba alibadilika na kwamba alimwambia kocha wa makipa hakuwa na shauku ya kucheza, japokuwa kipa huyo amekanusha kudai hivyo.
Badala yake, kipa wa kimataifa wa Argentina, Sergio Romero ndiye alidaka mechi zote mbili na hakuruhusu bao.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ambaye tayari amemsajili nyota Mateo Kovacic kutoka Inter Milan, anataka kuwakonga nyoyo washabiki kwa kusajili nyota mwingine kiangazi hiki.
Navas alicheza vyema kwenye mechi za kujiandaa na msimu huu, lakini anajua wazi kwamba atauzwa iwapo De Gea atasajiliwa, kwani Madrid wanaye kipa mwingine, Kiko Casilla aliyesajiliwa wakati nahodha na kipa mkongwe wa Bernabeu Santiago, Iker Casillas akiondoka. Ramos ameshafungwa kwa mkataba mpya klabuni hapo.
Baada ya kupigwa bao kwenye matumaini ya kumsajili Pedro, sasa Manchester United wamemgeukia mchezaji wa Southampton, Saido Mane, na wanasema kwamba watatoa zaidi kidogo ya pauni milioni 20 kumnasa.
Bayern Munich wanafikiria kumsajili kiungo kinda wa United, Adnan Januzaj wakati Tottenham Hotspur wanamtaka Victor Wanyama wa Southampton na wameandaa dau la pauni milioni 16.
OTAMENDI AAHIDI UBINGWA MAN CITY
Manchester City wamekamilisha usajili wa mlinzi wa kimataifa wa Argentina na Valencia, Nicolas Otamendi kwa dau la pauni milioni 32. Otamendi ndiye alikuwa mchezaji bora wa La Liga msimu uliopita na aliiwakilisha nchi yake kwenye fainali ya michuano ya Copa America.
Mchezaji huyu wa zamani wa Porto anasema kwamba anaona kama ndoto kuingia kwenye klabu aliyosema ni maarufu sana. Kocha Manuel Pellegrini alimsifu mlinzi huyo, akisema kwamba ana nguvu na anajua vyema kukaba, akiwa na utaalamu wa hali ya juu.
Anasema kwamba mchezaji huyo hatakuwa mgeni, kwani atakutana na watu kama Eliaquim Mangala na Fernando aliokuwa akicheza nao Ureno.
Otamendi ni mchezaji mkubwa wa tatu kusajiliwa City kiangazi hiki, baada ya wale wa kimataifa wa England, Raheem Sterling aliyetoka Liverpool na aliyekuwa nahodha wa Aston Villa, Fabian Delph