in , , ,

AZAM NA YANGA WAMESHINDWA KUONESHA UZALENDO

wanakutana kwenye ngao ya jamii jumamosi hii

Jana nilikutana na habari kuwa kocha wa timu ya taifa Charles Mkwasa amezilaumu klabu za Azam na Yanga kwa kugoma kuwaruhusu nyota wao kujiunga na timu ya taifa mapema kwa ajili maandalizi ya mchezo wa kirafiki tutakaocheza dhidi ya Oman Jumatatau tarehe 24/08/2015.

Klabu hizo zimefanya hivyo kwa kuwa zinawahitaji nyota wao hao kwa ajili ya mchezo wa ngao ya jamii utakaofanyika hapo Jumamosi baina yao na hatimaye nyota hao watachelewa mno kujiunga na kambi ya timu ya taifa.

Kiuhalisia sheria za FIFA hazizilamishi timu hizi kuwaachia wachezaji hao kwa kuwa mchezo wa hapo Jumatatu haumo kwenye Kalenda ya Michezo ya Kimataifa (International Match Calendar) ya FIFA.

Hata hivyo ingawa sheria haziwalazimishi Azam na Yanga kuwaachia wachezaji hao mzalendo yeyote anayependa maendeleo ya timu yetu ya taifa hawezi kuunga mkono maamuzi ya timu hizo.

Ni kweli kuna mchezo mgumu hapo Jumamosi baina ya timu hizi. Lakini sidhani kama ni sahihi kukataa kuwaachia wachezaji wajiunge na timu ya taifa mapema kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa hapo Jumatatu.

Huenda mchezo huu wa Jumatatu haupewi uzito wowote kwa kuwa ni wa kirafiki. Lakini tukumbuke kuwa mchezo huu ni sehemu muhimu ya maandalizi yetu kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika tutakaocheza dhidi ya Nigeria baada ya wiki mbili.

Kikosi  cha timu ya Yanga
Kikosi cha timu ya Yanga

Tutakutana na Nigeria tukiwa tunaburuza mkia kwenye kundi kwa kuwa tulishapigwa 3-0 na Misri kwenye mchezo wa kwanza. Hivyo maandalizi ya mapema yanahitajika na ndio maana hatutakiwi kupuuza mechi zetu za kirafiki.

Azam na Yanga wameshindwa kuonesha uzalendo. Pengine ni kwa sababu ya umuhimu wa wachezaji wa klabu hizo ambao mwalimu Mkwasa amewahitaji wakiwemo manahodha wa timu zote mbili ambao ni John Bocco na Nadir Haroub.

Lakini nafikiri umuhimu wa wachezaji hawa ndio ungewafanya Azam na Yanga kukubali kuwaruhusu mapema kama ishara ya kumuunga mkono na kumtia nguvu mwalimu Mkwasa kwa kuwa wachezaji hao ni muhimu pia kwenye timu ya taifa.

Azam na Yanga hawajali. Wanachokijali ni maslahi ya klabu zao na hatimaye wachezaji wa timu hizo watachelewa mno kujiunga na wenzao. Huu ni ubinafsi na kutokujali ambako kunapelekea maandalizi mabovu ya timu ya taifa.

Mwalimu Mkwasa amelalamika kuwa hili limemuharibia ratiba zake za maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Jumatatu na michezo muhimu ya mbeleni.

Bado lawama na mashambulizi vitamuelemea mwalimu Mkwasa na kikosi chake ikiwa timu ya taifa itapoteza michezo muhimu ukiwemo ule wa dhidi ya Nigeria wa mapema mwezi ujao.

Naomba hili lisitokee. Lakini nikizingatia makali ya Nigeria, matokeo ya timu yetu ya hivi karibuni na kutokujali kwa timu za Azam na Yanga sioni namna ambavyo tunaweza kuambulia walau sare kwenye mchezo huo.

Inakuwaje mchezo wa Ngao ya Jamii unapewa uzito kuliko michezo muhimu ya timu ya taifa? Inaonekana tumeikatia tamaa kabisa nchi yetu kwenye soka la kimataifa. Kama wadau muhimu wa soka la nchi yetu kama vilabu hivi vikubwa hawaoneshi kujali chochote sitegemei kuona mwananchi wa kwaida anajali.

Ninavyoona mwananchi huyo anausubiri kwa hamu mchezo wa Jumamosi na hajali chochote kuhusu maandalizi ya timu yetu ya taifa. Anasubiri Nigeria waje kutusambaratisha kisha aanze kulaumu na kuibeza timu ya taifa.

Kwa hili sitamlaumu mwananchi huyu. Lawama zangu zitawaelekea Azam na Yanga kwa kushindwa kuonesha uzalendo.

advertisement
Advertisement

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Sunday Oliseh

Super Eagles vs Taifa Stars

Abramovich amwaga £100m