Ni Chelsea vs Man City
HATIMAYE ratiba ya mechi za raundi ya tano kuwania Kombe la FA
imetoka, ambapo Chelsea watawakaribisha Manchester City.
Kombe hilo linashikiliwa na Arsenal kwa msimu wa pili mfululizo,
ambapo pia safari hii wamefuzu kwa raundi hii ya 16 bora.
Ratiba hii inamaanisha kwamba ama Chelsea au City watalikosa kombe
hili la pili kwa ukubwa nchini England baada ya lile la Ligi Kuu
(EPL).
Mechi hizi zitakazochezwa kati ya Februari 19 na 22, zinakuja wakati
Chelsea wakielekea kuanza kuimarika wakiwa na kocha Guus Hiddink,
baada ya kuanza msimu vibaya na kocha aliyefutwa kazi, Jose Mourinho.
Chelsea na City walikutana Agosti mwaka jana kwenye mechi ya EPL,
ambao City walishinda kwa 3-0.
Timu inayocheza kwenye League One, Shrewsbury Town, wanaochukuliwa
kuwa vibonde zaidi miongoni mwa klabu zilizofuzu watawakaribisha
Manchester United kwenye dimba la New Meadow.
Mabingwa watetezi, Arsenal, watapepetana na Hull, ikiwa ni kama
marejeo ya fainali ya 2014, ambapo Arsenal walishinda na kujifariji
sana kwa taji hilo.
Ratiba hiyo inaonesha kwamba Crystal Palace watakuwa wageni wa
Tottenham Hotspur, wakati Bournemouth watawakaribisha Everton katika
mechi zinazokutanisha timu za ligi kuu.
Mechi nyingine zitashuhudia Watford wakikamatana na Leeds United;
Reading watakabiliana na mshindi kwenye mechi ya marudiano baina ya
West Bromwich Albion.
Peterborough na Blackburn watacheza na ama Liverpool au West Ham
kulingana na matokeo ya mechi za marudio.
Mechi ya kuvuta wengi zaidi ni baina ya mabingwa wa karibuni zaidi wa
EPL, ambapo Hiddink ameshasema kwamba hiyo ni “huge game” –
itakayovuta watu wengi zaidi, akisema tayari ni kama fainali, maana
mmoja lazima aachie ngazi.
Hii ni droo ya tatu mfululizo dhidi ya timu ya EPL kwa kikosi cha
Manuel Pellegrini wakati Arsenal wanakutana na Hull kwa mara ya tatu
katika misimu mitatu. Mwaka jana Washika Bunduki wa London
waliwashinda Hull 2-0 katika raundi ya tatu mwaka jana.