KWA misimu minne sasa Yanga inapangua kikosi cha kwanza kwa madai ya baadhi ya wachezaji kukosa uwezo ama kushindwa kuonesha thamani yao kwenye ikosi vyao mbalimbali wakiwa chini ya makocha tofauti. Msimu iliopita Yanga iliwatupia virago takribani wachezaji 17 huku ikisajili wapya ambao walikuwa na matarajio makubwa.
Baadhi ya nyota walikuwa na uwezo mzuri kiufundi lakini hawakufanikiwa kuonesha cheche zao kwa vijana hao wa mitaa ya Twiga na Jangwani. Pili, takwimu zinaonesha kuwa Yanga wamekuwa zoa zoa pia kwa upande wa makocha kwa kuwafukuza kwa sababu mbalimbali hivyo kujikuta wakiwa na mwalimu mpya kila baada ya miezi 6.
Nasredine Nabil raia wa Tunisia ndiye kocha wa Yanga kwa sasa akiwa wa nne tangu kuanza msimu huu 2020/2021. Timu anayofundisha ameikuta, na sasa anapanga kuwaondoa baadhi ya wacheaji ambao hawamudu falsafa zake.
Nayo Kamati ya Usajili ya Yanga iko mawindoni kusaka huduma za wachezaji wapya watakaosajiliwa kwa maelekezo ya kocha huyo, hivyo kuwaondoa baadhi ya wale aliowakuta na ambao hawakidhi mahitaji ya mifumo yake.
Wakati huu kamati ya usajili ikiwa mawindoni watasingizia kujiweka tayari kwa mashindano ya kimataifa msimu ujao, lakini hali hiyo inakwaza mwendelezo wa timu yenyewe kwa kushindwa kukaa pamoja na kuanza kutoa matunda mazuri.
Simba wana takribani misimu mitano wachezaji wao asilimia 70 wamekaa pamoja na kutengeneza kombinenga muhimu inayowaleta matokea mazuri viwanjani ikiwemo hesabu za ubingwa msimu huu 2020/2021, ambao wameanza kuutwa tangu msimu wa 2017/2018 hadi sasa wakiwa mabingwa watetezi.
Taarifa kutoka klabu ya Yanga zinabainisha kuwa upo uwezekano wa kusajiliwa nyota wapya 8 watakaoingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza. Hebu fikiria wachezaji wapya 8 wanaingia kwenye kikosi cha kwanza, na kuanza upya mtiririko wao. Yaani kila msimu Yanga wanaanza upya.
Badala ya kujaza mapengo ya wachezaji wachache lakini unaona timu inataka kuingiza wachezaji 8 wapya, ikiwa na maana ya zoa zoa tu. Wakati tunashangilia soka la kimataifa hususani vilabu vya Uropa ni muhimu kujifunza mambo mazuri kutoka kwao kwenye masuala ya uendeshaji wa timu katika kusaka mafanikio, lakini tusisahau kutumia mbinu zetu kulingana na mazingira yetu. Zipo timu
zina wachezaji waliokaa pamoja kwa miaka 10, na kuleta matunda ya kuwa kwao pamoja.
Wakati mwingine wachezaji wanafeli katika klabu za Tanzania si kwa sababu hawana uwezo bali namna soka linavyoendeshwa oasipo ushirikiano na kumboresha mchezaji.
Kwamba mchezaji anajilea mwenyewe, timu badala ya kuhakikisha tathmini yake kuonesha anaweza kutumika katika mfumo wa aina fulani, badala yake tunamwacha kwa kisingizio haendani na kasi ya timu au ameshuka kiwango.
Mchezaji kushindwa kuna sababu nyingi ambazo zinakuwa ndani yake na nyingine nje yake. Mchezaji anaposhindwa katika timu fulani kwa sababu mbalimbali;
Kwanza, mfumo wa uchezaji wa timu huchangiwa mchezaji kutomudu. Pengine kocha anapenda mfumo wa kujihami,kumiliki mpira au mwingine ambao unakuwa kikwazo kwa mchezaji. Mateja Kezman alikuwa hatari katika Ligi ya Uholanzi lakini aliposajiliwa Chelsea chini ya Jose Mourinho mwenye timu ya kujihami alilazimika kuchezeshwa mfumo asiomudu na uawa mwanzo wa kuonekana hafai. Aliyesababisha hayo ni kocha wa Mourinho si kufeli kwa Kezman.
Alexander Hleb alikuwa nyota wa Arsenal, lakini alipohamia Barcelona ikawa kama ‘makapi’, mfumo ulimtoa jasho na hakupata muda wa kutosha kuonesha umahiri wake. Hiyo ni mifano namna makocha wanavyoweza kuharibu viwango cha wachezaji kutokana na mifumo yao, ingawa wanakuwa hawajashindwa kusakata kandanda. Mshambuliaji Yikpe alifeli Yanga lakini anawika huko Urabuni.
Pili, imani ya kocha kwa wachezaji wapya huchelewa mno hali ambayo inashusha ari kwa baadhi yao hivyo ni kama wanaanza ypya kila siku. Kuaminiwa na kocha katika timu ni jambo linamwimarisha mchezaji kwa kiasi kikubwa.
Kocha asipomwamini mchezaji humnyima muda, na hata akihojiwa na viongozi wake anaweza kusingizia chochote lakini ukweli huchangia matatizo ya wachezaji, lakini viongozi wetu kibongo bongo wanadhani tatizo ni mchezaji peke bila kuangalia mambo yanayojumuisha kutokea hayo.
Tatu, kuibuka kwa wachezaji wengine ambao humzidi kiwango mchezaji mgeni. Mara nyingi kwenye timu kuna wachezaji wanaibuka bila kutarajiwa, ambao wanaweza kuziba mwanya wa mchezaji mpoya kutamba kwenye kikosi. Mtazame Deus Kaseke pale Yanga ndipo utajua kuwa na mchezaji kama huyo akikaa na wengine muda mrefu wanatengeneza kombinenga nzuri.
Nne,mazingira mapya yana mchango kwa mchezaji kufanya vizuri au kuboronga. Baadhi ya wachezaji huwachukua msimu mzima kuweza kujiweka sawa, lakini kwenye soka la Tanzania mchezaji anahukumiwa ndani ya mechi 3 au mwezi mmoja tu, pasipo wao kutafuta namna ya kumtumia kulingana na aina yake ya uchezaji. Ni kwamba hatuna mfumo wa kumtengeneza mchezaji ila tunazoa zoa tu.
Tano, muda anaopewa kucheza na matarajio yaliyoko kwake huwa hayaoani na ikiwa yanaoana basi sababu nyingine za hapo juu huchangia kushindwa kwake.
Sita, kuumia mara kwa mara kunachangia kuporomosha kiwango cha mchezaji husika na kuharibu saikolojia yake. wapo wachezaji ambao tangu waumie viwanjani iwe mazoezini au kwenye mechi wanapotea moja kwa moja.
Hivi karibuni Eden Hazard kwa mara ya kwanza amecheza mechi yote yaani kamaliza dakika 90 akiwa timu ya taifa Ubelgiji kwenye mashindano ya Euro tangu alipoumia Novemba mwaka 2020 hajawahi kurudi kwenye kiwango chake, lakini anavumiliwa. Ingelikuwa anacheza timu za kwetu Tanzania huyu angetupiwa virago msimu mmoja tu kwa kisingizio ameshindwa kuendana na mazingira mapya.
Kifupi hatutunzi wachezaji ambao wana uwezo mkubwa kiufundi pale wanapokutana na majeraha. Simba walikuwa na utamaduni huo huo kutotunza wachezaji, mfano halisi ni Shaban Nditi wakati akitokea Mtibwa Sugar.
Nditi alikuwa ana kiwango bora kabisa ambacho kiliwavutia Simba, na wakati huo alikuwa kinara wa kiungo Taifa Stars ya Marcio Maximo. Lakini kilichotokea ni majeraha ya mara kwa mara kabla ya kuamua kuondoka kurudi tena Mtibwa Sugar.
Hii ina maana wachezaji ni wafanyakazi ambao wanaweza kukuonesha mambo mazuri na yenye ufanisi ikiwa wana afya njema, lakini wanapotekelezwa wakiwa wagonjwa maana yake mifumo ya uendeshaji wa timu imejaa ubabaishaji. Lakini Simba wa sasa wamebadilika.
Saba, wakati mwingine mchezaji hushindwa kuchezea tiu mpya kwa sababu shinikizo kubwa lililopo, yaani presha. Zipo timu zina presha kubwa kwa mchezaji ambaye anategemewa kuonesha cheche zake. kwahiyo presha inapokuwa kubwa na kumzidi mchezaji huwa chanzo cha kushuka kiwango.
Suluhisho la hilo si kumtupia virago bali kuhakikisha timu kama Yanga au Simba zinakuwa na wataalamu wa saikolojia ambao watafanya kazi ya kushughulikia afya ya akili ya mchazaji na kuhakikisha anakuwa kwenye hali nzuri kiakili na kuituikia timu. Kinyume cha hapo tutambebesha lawama nyingi mno.
Nane, timu kutokuwa wazalishaji wa ipaji yake vinayoweza kuitumiwa ni sababu nyingine inayochangia kuwapoteza wachezaji wazuri. Hivi karibuni kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen aliwaita wacheji wanne aliowafundisha zamani katika kikosi cha Vijana cha Serengeti Boys, ambao baadhi wapo nje ya nchi wakisakata kandanda na wengine wakiwa hapa nchini.
Uamuzi wa Kim Poulsen umetuumbua kama taifa jinsi ambavyo hatuna mipango wa kusimamia wachezaji wetu na kuwaendeleza ili wawe nyota wakutumainiwa. Ni mambo kama hayao yanachangia kuzoa zoa wachezaji. Mfano halisi tazama mashindano ya vijana chini ya miaka 20 wa Ligi kuu, kila msimu wanapotea tu, halafu tunaanza upya. Tunaaibisha sana.
Ifahamike tathmini ya mchango wa mchezaji haitolewi tu kwa mechi anazocneza, bali hata ushindi anaoonesha mazoezini katika timu na kumfanya yule mchezaji anayepangwa kikosi cha kwanza kuwa na kiwango bora. Kwahiyo hilo linahitaji muda wa timu kumwandalia mchezaji mazingira ya kujifunza kwenye timu mpya,wachezaji wapya,makocha wapya,mbinu mpya na utamaduni mpya.
Ndiyo maana hadi leo baadhi ya watu wanashindwa kuelewa kwanini Calinhos alikuwa analalamikia vyakula vya Kitanzania na alitaka vile ya kwao Angola.
Si ajabu wachezaji barani Uropa hususani wale wanaotokea Amerika ya kusini huchagua kucheza La Liga au Serie A sababu ya mtiririko wa mafanikio ya waliotangulia,mazingira ya kazi yao,utamaduni na hali ya hewa. Ni wachache wanakubali kwenda England kwa sababu wanaepuka mambo niliyoorodhesha hapo juu.
Ligi Kuu Tanzania Bara inasifika hata kwa majirani zetu kuwa ina fedha nyingi za malipo kwa wachezaji lakini ukweli usemwe bado tuna safari ndefu ya kuifanya ligi yenyewe iwe katika kiwango bora.
Kwa kuhakikisha mifumo ya uendeshaji wa vilabu yetu unakuwa na kisasa ikiwemo kuhakikisha weledi wa viongozi kuhakikisha wachezaji wao wanakaa pamoja na kutengeneza timu tishio sio kuzoa zoa kila msimu kuingiza wapya kikosi cha kwanza. Yanga ya sasa inaonesha ina malengo ya muda mfupi tu katika vikosi vyao, inazoa zoa bila kutoa nafasi ya muda kwa wanaozolewa kuchezea timu hiyo na kuleta mafanikio.
Comments
Loading…