in

Yupo wapi refa bora wa dunia apewe tuzo yake?

Mwamuzi wa mpira wa wavu

MCHEZO wa soka unakamilika chini ya usimamizi wa mwamuzi. Waamuzi wapo kwenye michezo mbalimbali. Kwenye Volleyball, Kikapu, mpira wa pete, Ndondi. Kwenye mchezo wa Tennis wapo waamuzi pia.

Kila mchezo unakuwa na mwamuzi ambaye anasimamia sheria za mchezo husika. Mwamuzi huyu anaweza kukutana na mazingira magumu ya mchezo lakini anamudu au kumaliza akiwa salama. 

Kuna presha kutoka kwa timu shindani. Kuna presha kutoka kwa makocha na wamiliki wa timu zenyewe. Kuna presha kutoka serikali za nchi, mashabiki na wadau wengine wa mchezo husika. 

Halafu, presha ya mwisho kubwa inakuwa uwanjani. Wachezaji wanaweza kumzingira mwamuzi au kulalamikia maamuzi yake huku wakimtia presha afanye upendeleo kwao au kuwaadhibu wachezaji wa timu pinzani.

Wote wanakuwa wanamtazama mwamuzi. Mwamuzi anakuwa kiongozi wa dunia katikati ya presha kubwa. Kulia kwake anaye msaidizi. Kushoto kwake kuna msaidizi, halafu kuna mwamuzi wa akiba. Lakini maamuzi yote ya mchezo wa siku hiyo hubebwa na mwamuzi wa katikati ya dimba kwenye soka.

Fikiria  mwamuzi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia anatazamwa na mamilioni ya washabiki, wadau na viongozi wa soka. Ni kazi yake, lakini ngumu mno kuzimaliza dakika 90 bila kutukanwa matusi, kebehi, dharau na mengine kutoka kwa mashabiki, wachezaji au wadau wengine wa soka. Lakini dakika 90 si rahisi kwa waamuzi wa soka. 

Fikiria mwamuzi wa ndondi anapokabidhiwa pambano la Lennox Lewis dhidi ya Mike Tyson au Deontany Wilder dhidi ya Tyson Fury. Ama bondia Antony Joshua dhidi ya wapinzani wake katika mchezo huo.

Fikiria mwamuzi anayekabidhiwa pambano kati ya Real Madrid na Barcelona, au Manchester United dhidi ya Liverpool. Ama mwamuzi wa AC Milan dhidi ya Inter Milan, au mwamuzi wa River Plate dhidi ya Boca Junior. 

Au mwamuzi wa Sao Paulo na Corinthians. Mfikirie mwamuzi anayepewa pambano kati ya Brazil na Argentina, PSG dhidi ya Lille au Olympique Marseille. Mwamuzi wa pambano la Club Africain dhidi ya Esperance, au Enyima dhidi ya Enugu Rangers, au Nkana Rangers dhidi ya Zanaco.

Mtazame mwamuzi wa Misri dhidi ya Tunisia. Mfikirie mwamuzi wa Yanga na Simba, au AS Vita dhidi ya TP Mazembe. Mwangalie mwamuzi wa mpira wa Pete au Handball. 

Mwamuzi wa Tennis katika pambano la Serena Williams, Venus Williams, Andre Agassi, Pete Sampras, Rafael Nadal, Djokovic, Federer, na wengineo kwenye mchezo huo.

Wamuzi wote hao wana majukumu makubwa kuhakikisha mchezo unakwisha salama kwa pande zote kwa kusimamia sheria. 

Wote wanahakikisha mashabiki na timu zao zimemaliza salama na kwa kufuata sheria za mchezo. Hebu fikiria yule mwamuzi aliyepuliza kipyenga kwenye mchezo wa ufunguzi wa fainali za kombe la dunia mwaka 2002 Ufaransa dhidi Senegal. 

Mwangalie mwamuzi yeyote yule kwenye mchezo namna anavyokabiliwa na changamoto ndani na nje ya uwanja. 

Majibu tunayopata hapa ni kwamba mwamuzi ni mtu muhimu sana katika mchezo. Umuhimu wake ni pale haki inapotendeka kwa timu au mtu anayehusika na mchezo.

Adhabu anazotoa na haki anayosimamia ndani ya mchezo. Utaona kwamba waamuzi ni watu ambao wanaweza kuinuliwa na kupandishwa zaidi.

Tufikirie pamoja; kuna tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka duniani inayotolewa na FIFA. Kuna tuzo ya mchezaji bora duniani inayotolewa na Ballon D’or ya Ufaransa. 

Kuna tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya. Kuna tuzo  ya mchezaji bora wa mwaka ya CAF. Kwa CAF kuna tuzo ya mchezaji bora wa mwaka katika Ligi za ndani barani Afrika ambayo imewahi kunyakuliwa na Mbwana Samatta.

Zipo tuzo za wachezaji bora wa mwaka wa Amerika Kusini, Asia, Australia, CONCACAF na kadhalika. Sehemu zote hizo zinahusisha waamuzi ili mchezo kuwa salama. 

Ninatamani kuona matamasha ya kukabidhi tuzo kwa waamuzi bora kama wanavyofanya kwa wachezaji. CAF walikuwa na tuzo ya namna hiyo, lakini wameamua kuiweka kando.

FIFA hawana tuzo ya namna hiyo. Vipi kwa shirikisho letu la soka nchini Tanzania, TFF ama jirani zetu Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Rwanda na Burundi hawana namna ya kuwatuza waamuzi wetu wa michezo?

Mfano tuzo ya mwamuzi chipukizi, mwamuzi bora wa mwaka, mwamuzi bora wa Afrika, Ulaya, Amerika, Asia na kadhalika. Kama zipo tuzo za wachezaji bora chipukizi kwanini wasiwepo waamuzi bora chipukizi? 

Kama tuzo zinatolewa mfano Lyon au Paris, ni kwa vipi FIFA, CAF, UEFA na wengine washindwe kutoa tuzo kwa waamuzi? Na hii iwe hata kwenye ndondi, wamuzi wanastahili kupewa tuzo pia iwe chipukizi au wakongwe.

PierLuigi Collina amekuwa akisifiwa hadi leo. Collina anachukuliwa kuwa mwamuzi bora kabisa kuwahi kutokea katyika mchezo wa kandanda. Ni kipenzi cha waamuzi wengi duniani. Mashabiki wengi wanampenda Collina kwa sababu alikuwa mwamuzi bora. 

Ingekuwaje kama FIFA wanayo sherehe kukabidhi tuzo kwa waamuzi bora peke yao? Nadhani ni changamoto kwa waamuzi wenyewe katika kufanya kazi kwa ufanisi.

Ipo hoja kuwa tuzo ya mwamuzi bora inaweza kuharibika ikiwa atachezesha michezo mingine kwa kiwango cha chini yaani kuwa maamuzi mabovu na kuharibu.

Lakini swali hilo hilo linaweza kuuulizwa kwa wachezaji bora wanaopewa tuzo hizo, mbona wengi sana wanaboronga katika miaka inayofuatia? Je tuzo zimefutwa kwa sababu hiyo?

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Moro kaigharimu Yanga

Moro aigharimu Yanga VPL

Kikosi cha Simba Sports Club

Ibrahim Ajib, Jangwani inakuhitaji