in

Ibrahim Ajib, Jangwani inakuhitaji

Kikosi cha Simba Sports Club

Lile jina la Ibrahim Ajib “Migomba” bado lipo jangwani. Kumbukumbu zako zimekuwa chemichemi ambazo hazijawahi kukauka katika jangwa lenye udongo wa njano na kijani. Natumaini unaendelea vizuri.

Nina amini unaendelea vizuri, unaendelea vizuri kwa sababu upo kwenye timu ambayo haina matatizo ya kuchelewesha mishahara kama ambavyo ulivyokuwa jangwani.

Pamoja na kwamba Jangwani ulikuwa unacheleweshewa mshahara, lakini ulikuwa unashawishiwa nafasi ya kucheza uwanjani. Akili yako ilikuwa haiwazi namna ya kupata nafasi ya kucheza kama ambavyo ulivyo kwenye mto wa msimbazi.

Akili yako ilikuwa inaweza namna ya kupika magoli peke yake, kitu ambacho kilikufanya ufikishe pasi 20 za mwisho za magoli. Pasi ambazo zilikufanya uwe mpishi bora wa magoli kuwahi kutokea kwenye ligi kuu ya Tanzania bara.

Tumekukumbuka sana Ibrahim Ajib, mwili wako ulikuwa unapendeza zaidi ulipokuwa unavishwa rangi ya njano na kijani. Picha yako haijawahi kufutika kwenye akili za wana Jangwani wengi.

Tanzania Sports
Ibrahim Ajib

Hata ile jezi namba kumi anayoivaa Tariq Seif tunaikumbuka kila tukimuona akiwa amevaa.  Jezi ile ilikuwa inakustahili na ilikuwa imekuvaa sana na ulikuwa unaitendea haki jezi ile.

Ile dhana ya namba 10 huvaliwa na mtu mwenye kipaji kikubwa na mwenye uwezo wa kuibeba timu, dhana hiyo ilikuwa kwako. Ulikuwa na uwezo wa kuufanya mpira utakavyo wewe.

Miguu yako ilikuwa ni amri jeshi mkuu  na mpira ulikuwa ndiyo mwanajeshi wako, sauti yako ilisema kwa amri mguu pande, mpira ulikaa mguu pande.  Sauti yako iliposema mguu sawa mpira ulitii.

Hata wakati ambao ulitaka mpira uende nyuma geuka, mpira uligeuka kwa adabu kweli kweli. Miguu yako iliposema mbele tembea mpira ulienda mbele bila kusita. Miguu yako ilikuwa na sauti.

Kumbuka pia miguu yako iliitwa yenye dhahabu kipindi kile upo jangwani. Kwa bahati mbaya ulipo ni pagumu kwako. Kila ukiamka unawaza namna ya kuwaweka benchi kina Francis Kahata,  Deo Kanda,  Miraji Athumani na wengine.

Kabla hujaja Simba ulikuwa mfalme Jangwani , ulitakiwa kuwepo sehemu ambayo ungezidi kuonesha ufalme wako. Jangwani panakuhitaji sana, jangwani panahitaji ufalme wako.

Siumesikia juzi pia kuwa wanampango wa kukuletea na Bernard Morrison hapo msimbazi upambanaye naye? Tafakuri ya ziada inahitaji kuchukua nafasi kubwa sana kwenye akili yako.

Jangwani panakutazama, jangwani panakuhitaji, jangwani panahitaji kuwekewa sanamu yako ya heshima. Fikiria namna ya kukumbukwa kama mmoja ya watu mahiri na hodari kuwahi kutokea Jangwani kwa sababu huko unaweza ukapata nafasi kubwa ya kucheza.

Hii ni barua ya wema, barua ambayo wana jangwani wameniambia nikuandikie. Bado wanakupenda, bado wanaona una nafasi kubwa sana ya kutengeneza magoli mengi. Wewe ndiye mfalme wa “Assist” ufalme ambao utakuwa imara kama utapata sehemu ya kucheza mara kwa mara.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Mwamuzi wa mpira wa wavu

Yupo wapi refa bora wa dunia apewe tuzo yake?

Mchezaji wa Azam FC

Yanga, Azam FC utamu wake uko hapa