Ulitazama tamasha la Wiki ya Mwananchi? Moja ya tamasha bora la kimpira kuwahi kutokea nchini. Hongera kwa Yanga kwenye hili. Wanahitaji pongezi sana kwa sababu mbalimbali.
Yanga ilikuwa na sura ambayo kwa haraka haraka ni ngumu kuwakaribisha wadhamini kuja kuwekeza pesa zao kwa sababu hawakuwa na bidhaa nyingi za kuwauza wadhamini.
Wiki ya mwananchi ilikuwa ni njia nzuri ya kuwaonesha wadhamini kuwa wao ni sehemu sahihi kwa mtu kuja kuweka pesa yake na bidhaa yake ikafanikiwa vyema.
Wiki ya mwananchi ilikuwa ni siku ambayo ilionesha Chapa ya Yanga ina ushawishi mkubwa kwa kukusanya wafuasi mbalimbali wa klabu yao. Wafuasi ambao ni wengi.
Wiki ya Wananchi ilionesha namna ambavyo Yanga ina mashabiki wengi Tanzania. Kitu ambacho ni mtaji mkubwa wa kibiashara kwa Yanga.
Wiki ya wananchi ilikuwa ni siku ambayo Yanga ilijisafisha kibiashara kwa kuonesha Yanga ni sehemu sahihi ya kuwekeza na ni sehemu sahihi inayoaminika.
Tuanzie hapa kwenye kuaminika. Chapa yoyote ili ipata wadhamini wa kufanya nao biashara lazima ijenge mazingira mazuri ya kuaminika ndani na nje ya klabu.
Lazima kuwe na mipango mikakati mbalimbali ya kuonesha kuwa Chapa hii inaaminika sana kwa watu wa nje na ndani ya hiyo Chapa.
Wakati jana namsikiliza Mwinyi Zahera kuhusu madai yake kwa Yanga. Neno kuaminika lilikuja kwenye kichwa changu. Yanga imejitahidi ndani ya wiki ya mwanachi kujitengenezea mazingira ya kuaminika.
Imejitengenezea mazingira mazuri kuonesha kuwa ina aminika. Mazingira ambayo ni rafiki mkubwa wa mfanyabiashara yoyote kuja kuwekeza pesa zake.
Lakini linapokuja kwa madai ya wafanyakazi wao kudai mishahara ile picha ya wao kuaminika inafutika. Taasisi yoyote ya kibiashara haiwezi kuwekeza pesa zake sehemu ambayo haijali maslahi ya wafanyakazi wao.
Kwenye hili suala la madai ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi waliopo wa Yanga na wafanyakazi waliopita wa Yanga ni kujitengenezea picha mbaya kibiashara kwa wadhamini.
Comments
Loading…