“All team in Tanzania, don’t talk again for final…they talk too much” …hiyo ni nukuu ndogo ya maneno aliyozungumza Fabrice Ngoma kwa furaha iliyochanganyika na jazba flani mara baada ya klabu ya Simba kuingia fainali ya CAFCC baada ya kufanikiwa kuwatoa wapinzani wao katika mchezo wa nusu fainali.
Maneno ya Ngoma ni majibu kwa watani zao Yanga ambao kwa muda mrefu msemaji wa klabu hiyo Ally Kamwe pamoja na mashabiki wa klabu hiyo ya jangwani, wamekuwa wakiwatambia wenzao kwa kufanikiwa kucheza fainali ya CAF CC msimu wa 2023 ambapo walipoteza kwa USM Alger kutoka Algeria.
Zimebaki dakika 180 kabla klabu mojawapo kati ya RS Berkane ya Morocco au Simba ya Tanzania kutangazwa rasmi kuwa bingwa wa kombe la Shirikisho (CAF CC) kwa vilabu vya Afrika kwa msimu huu wa 2025/2026. Ni mechi mbili za fainali zitakazopigwa tarehe 17 Mei 2025 huko Morocco kabla ya kumalizia fainali ya pili tarehe 25 mwezi Mei 2025 hapa Dar es Salaam, Tanzania.
Inatarajiwa kuwa mechi ngumu kwa vilabu vyote hasa ukizingatia kiwango cha hali ya juu kilichooneshwa na timu zote mbili tangu hatua za awali hadi mechi za mwisho za nusu fainali ambapo RS Berkane ilitupa nje CS Costantine wakati ambapo Simba iliwaondoa mashindanoni wajukuu wa Mzee Nelson Mandela, Stellebosch ya Afrika Kusini.
Kwa klabu ya Simba, hii itakuwa ni fainali ya pili ya mashindano yanayoandaliwa na CAF baada ya kufanya hivyo zaidi ya miaka 32 iliyopita mnamo mwaka 1993. Kwa wapinzani wao, RS Berkane, hii ni fainali yao ya tano katika kipindi cha miaka 7, katika fainali nne zilizopita, wameshinda mbili na kupoteza mbili!
…’they talk too much” hii ni sehemu ya kauli ya Ngoma, ni majibu ya moja kwa moja kwa Yanga. Itoshe kusema yale maneno ya msemaji wa Yanga, Ally Kamwe na kelele za wanazi wa jangwani zilikuwa haziishii tu kwa mashabiki wa Simba bali pia kwa wachezaji.
Zilikuwa haziwakeri mashabiki na wanazi wa Simba pekee, bali hata wachezaji nao walikuwa wanakereka. Ni bahati mbaya mshabiki hana lolote awezalo kufanya pale anaposhambuliwa kwa maneno ya utani pale timu yake inapofanya vibaya zaidi ya kuwa mpole.
Kwa wachezaji ni tofauti, wao wana nafasi ya kubadili kelele na dharau za mashabiki wa upande wa pili kuwa hamasa ya kufanya vizuri na kuongeza bidii. Itoshe kusema kauli ya Ngoma imethibitisha wazi wachezaji wa Simba na uongozi mzima wa klabu hiyo ya Msimbazi walikuwa na jambo lao moyoni la kulipa kisasi cha mafanikio yaliyofikiwa na Yanga msimu wa 2023.

Ndio, msikilize vizuri Fabrice Ngoma, anawakilisha wana Simba wote, anasema ‘all team in Tanzania don’t talk again for final…Simba they bring cup to Tanzania’, fainali ya Yanga vs USM Alger lilikuwa ni deni kwa wachezaji wa Simba. Wamelipa deni, sasa hivi upande wa pili upo kimya!
Ni wakati mzuri kwa klabu ya Yanga kupata faida ya Simba kuchukua ubingwa wa CAF CC siku ya tarehe 25 Mei 2025 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Wenye Yanga yao watanishangaa, YES…ni faida kubwa kwa Yanga iwapo Simba itatawazwa kuwa bingwa!
Ubingwa kwa Simba ni kichocheo tosha kwa Yanga hasa viongozi kuboresha kikosi ili kufikia mafanikio ya watani wao. Ubingwa wa Simba ni kichocheo kwa wachezaji wa Yanga kuonesha kwamba hata wao wanaweza kufanya kama watani zao!
Klabu hizi mbili za Kariakoo, zenyewe zina faida moja kubwa tofauti na klabu nyingine za hapa Tanzania, ambazo kwa uwezo wa kifedha hazijapishana sana. Kurwa na Dotto wana fursa ya adhimu ya shinikizo la ndani na shinikizo la nje jambo ambalo baadhi ya timu zinakosa.
Shinikizo la ndani kwa maana ya malengo binafsi ya klabu na shinikizo la nje kwa maana ya msukumo unaotokana na kutaka kufanya vizuri zaidi ya mpinzani wa jadi…hii ni silaha muhimu sana ambayo ndio inaweka utofauti na vilabu vinine hapa Tanzania.
Kila la kheri Simba, ubingwa wenu ni faida kwa Yanga!