KUNA Majina makubwa sana yaliyovaa jezi namba 9 pale Liverpool. Miongoni mwa magwiji waliovaa jezi namba 9 ya Liverpool ni kama Ian Rush, Robbie Fowler, Fernando Torres, na Roberto Firmino. Magwiji hao wanasifiwa kwa umahiri wao kwenye soka, walipachika mabao mengi, walileta raha kwenye dimba la Anfiedl, waliwafanya mashabiki waamini wachezaji wazuri wanapatikana Liverpool tu. Baada ya kuondoka Roberto Firmino mchezaji mwingine aliyevaa jezi namba 9 ya Liverpool ni Darwin Nunez, nyota aliyesajiliwa kutoka Benfica ya Ureno. Maisha ya Darwin Nunez hayakuwa mazuri katika klabu ya Liverpool tofauti na alivyokuwa kwenye Ligi Kuu Ureno wakati akichezea klabu ya Benfica. Baada ya msuguano wa muda mrefu, Alexander Isak alijiunga na Liverpool na kuwaaga mashabiki na viongozi wa Newcastle United. Sasa ameanza maisha maisha mapya katika klabu ya Liverpool.
Ni mambo gani yaliyomwondoa Alexander Isak na kujiunga na Liverpool? TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu ambayo yamechangia nyota huyo kukimbilia Liverpool na nini ambacho anaweza kukipa kwenye klabu yake mpya.
Medali za Makombe
Hakuna ubishi kwamba kila mchezaji anataka kutwaa ubingwa. Kila mchezaji anatamani kuvaa medali ya ubingwa fulani. Lakini maisha ya Newcastle United hayakumpa uhakika wa kutwaa ubingwa tena baada ya kuchukua ule wa Carabao. Mafanikio kwa mchezaji yeyote ni kutwaa ubingwa fulani. Hili Liverpool wanaweza kumhakikishia kwa vile wao tayari ni mabingwa watetezi. Mpango wa Liverpool ni kuvunja rekodi ya kutwaa ubingwa inayoshikiliwa na Manchester United. Kwahiyo wanataka kuhakikisha wanakuwa na silaha zao za kuvunja rekodi hii. Mchezaji wao wanayemtegemea ni Alexander Isak.
Mabao langoni mwa adui
Bila hata kuangalia takwimu unaweza kuona kabisa safu ya ushambuliaji ya Liverpool haikufunga mabao mengi. Badala yake mabao yalikuwa yanafungwa kwa mchanganyiko miongoni mwa viungo na washambuliaji. Kwa maana hiyo Liverpool ya Arne Slot ilihitaji mshambuliaji mmoja ambao atawapa uhakika wa mabao angala 40 kwa upande wa Ligi Kuu. Kila walipotazama kwenye kikosi chao, hawakuwa na uhakika kama wangeweza kupata mabao hayo. Ikawalazimu waingie sokoni. Ili wachukue ubingwa msimu huu lazima wabadilike, kuwa na mbinu mbadala kuliko msimu uliopita. Arne Slots amesomwa na wapinzani wake, kwahiyo kubaki na Darwin Nunez ingekuwa kujimaliza kabisa. Alexander Isak anatambua kuwa ni mabao yake ndiyo yatampa thamani zaidi Liverpool, kwa sababu ni mahali ambapo magwiji wameweka rekodi mbalimbali. Kwahiyo lazima asimame imara kuhakikisha anaweka rekodi yake kwa kupachika mabao mengi. Arne Slots amewekeza kwa wachezaji wawili Hugo Ekietike na Alexander Isak, Kwahiyo mabao ndicho kitu cha kwanza kinachohitajika kutoka kwa washambuliaji hao. Jukumu hili ndilo linaotakiwa kubebwa na Isak.
Ubingwa wa EPL
Akizungumzia tangu mwanzoni mwa tetesi za usajili wa Alexander Isak nyota wa zamani Zlatan Ibrahimovic alisisitiza kuwa ili kutwaa ubingwa ni lazima Msweden mwenzake huyo aondoke Newcastle United. Zlatan alikaririwa na vyombo vya habari kuwa kombe la Carabao halina heshima kwa mchezaji mwenye ndoto kubwa, na alitaka kumwona Isak akijiunga na klabu kubwa ikiwemo Liverpool. Hicho ndicho kilichotokea, na kwamba Isak alijiunga na Liverpool. Kwa namna suala hilo lilivyotokea, unabaini kuwa Alexander Isak hakutaka tena maisha ya Newcastle, na ndoto zake zilikuwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England. Huwezi kufirikia kutwaa ubingwa wa EPL na Newcastle United. Kwa Liverpool, Isak atapewa ubingwa kwa sababu ni timu inayofukuzia taji hilo. Endapo msimu uliopita kocha Arne Slot angekuwa na Alexander Isak basi nyota huyo bila shaka angekuwa mfungaji bora wa EPL.
Hamu ya Ligi ya Mabingwa
Kucheza Ligi ya Mabingwa ni ndoto ya kila mchezaji. Pia kila mchezaji anayeshiriki Ligi ya Mabingwa anafahamu kuna faida za kiuchumi pia kupitia marupurupu wanayopata kwa timu kushiriki ama kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alexander Isak kama mchezaji mwenye ubora wa hali ya juu aliangalia malisho mapya na Liverpool ni sehemu sahihi ambayo inaweza kumpa vyote viwili.
Liverpool wanao mwelekeo mzuri chini ya kocha Arne Slot. Nafasi ya Isak kupangwa kikosi cha kwanza ipo kwa sababu wanahitaji mshambuliaji mwenye uwezo wa kuwapatia mabao ya kutosha.
Heshima ya Klabu
Kuchezea timu inayofukuzia ubingwa na ile ambayo inataka kumaliza nafasi nne za juu ni tofauti. Liverpool wana heshima ya kufukuzia ubingwa, wakati alikotoka kulikuwa na mpango wa kutafuta nafasi nne za juu. Alexander Isak kuchezea Liverpool ni suala linalompa heshima pia kwani ni klabu ambayo inasifika Kimataifa. Heshima ya kuchezea timu kubwa inapendwa na kila mchezaji, hicho ndicho pia anachokitaka Alexander Isak.

