Misimu mitatu iliyopita Simba imekuwa ni timu ambayo ina kikosi imara. Kikosi ambacho kimeisaidia Simba kuchukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara mara tatu mfululizo.
Moja ya kitu kikubwa ambacho kiliwasaidia Simba kuwa bora zaidi ndani ya misimu mitatu iliyopita ni wao kutengeneza kikosi imara chenye wachezaji bora na imara.
Walisajili wachezaji wazuri ndani ya kikosi chao. Kila nafasi ndani ya uwanja ilikuwa na wachezaji wawili ambao walikuwa na viwango ambavyo vinalingana.
Jana wakati natazama kikosi cha Yanga kilichokuwa kimeanza , nikatazama na wachezaji ambao walikuwa kwenye benchi niliona kitu tofauti kabisa.
Niliona Yanga ambayo siyo Yanga ya misimu mitatu iliyopita. Benchi la Yanga lilikuwa limesheheni wachezaji wenye majina makubwa ambao walikuwa na uwezo wa kubadilisha matokeo.
Kitu hiki hakikuwepo kwa Yanga ndani ya misimu mitatu iliyopita. Yanga ilikuwa na kikosi kifiyu sana. Kikosi ambacho kilikuwa kinawapa wakati mgumu wao kufanya vyema.
Kwa sasa Yanga ina wachezaji wawili kwenye kila eneo ndani ya uwanja. Wachezaji ambao wana kiwango kinachofanana kwa kiasi kikubwa. Kiwango ambacho ni kikubwa.
Pamoja na kwamba haikufanikiwa kushinda mechi dhidi ya Tanzania Prisons lakini ilikuwa na kikosi kizuri ambacho hakijazoeana. Yanga inahitaji kukaa pamoja kwa muda ambao utawapa nafasi ya wao kujijenga vyema.
Simba kilichowapa nafasi ya wao kuwa timu bora ni wao kuwa na wachezaji wenye viwango vikubwa kwenye kila eneo ndani ya uwanja.
Yanga kwa msimu huu wana kikosi cha hivo. Kila eneo ndani ya timu ina wachezaji wawili wenye viwango vikubwa kuanzia kwa golikipa mpaka kwa washambuliaji.
Magolikipa wa Yanga, Metacha Mnata na Farouk Shikalo wana viwango vikubwa wote. Mabeki wa pembeni na mabeki wa kati wana viwango vikubwa.
Eneo la kiungo cha Yanga kina wachezaji wenye viwango vikubwa sana mpaka eneo la ushambuliaji. Wachezaji hawa hawajapata muda wa wao kukaa pamoja na kujijenga kitimu. Wakijijenga vyema Yanga itatoa ushindani mkubwa sana kwa Simba tofauti na msimu uliopita.
Comments
Loading…