Asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe…”, hii ni rejea maarufu kutoka kwenye Biblia, katika kitabu cha Yohana 8:7. Hii ni sehemu ya hadithi ya mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi na kuletwa mbele ya Yesu na viongozi wa dini wakitaka arushiwe mawe, kulingana na sheria ya Musa.
Sakata la Yanga, TFF na Bodi ya Ligi imenikumbusha huo mstari wa kwenye Biblia. Kwa wapenda soka, sote tunafahamu chanzo cha sakata hilo… ni pale klabu ya Simba ilipodai haitopeleka timu uwanjani kutokana na figisu za wanaodaiwa kuwa makomandoo wa Yanga kuwazuia kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo na Bodi ya Ligi kubariki msimamo huo na kuahirisha mechi ya derby iliyopangwa kufanyika Machi 2025.
Baada ya kuahirisha mchezo huo klabu ya Yanga ilitoa tamko kwamba haitashiriki mchezo mwingine wa derby msimu huu kwani wanatambua mechi yao ilitakiwa kuchezwa tarehe 8 Machi mwaka huu na wanastahili kupata pointi tatu.
Kufupisha story…baada ya CAS kutoa taarifa ya kuitaka Yanga kutumia vyombo vilivyopo nchini kudai haki yake kabla ya kwenda kwao (CAS), bodi ya Ligi imepokea taarifa ya CAS kwa kutangaza tarehe mpya ya derby. Yanga wanasema hawachezi…yes, hawatapeleka timu, kisa TFF na Bodi ya Ligi wanaendesha ligi kwa ‘upendeleo’ kwa maana nyingine Yanga wanadai wanaonewa.
Itoshe kusema kilichotokea kwenye mpira wetu, ni kwamba kuna mmoja wa wadau muhimu kwenye soka letu amekamatwa ‘akizini’, ila ni ukweli ulio wazi kwamba wanaodai kumkamata aliyezini nao hayo ndio mambo yao, nao ni ‘wazinifu’ wazuri tu ila hawajafumaniwa bado au wanafichiwa siri!
Mpira wetu bado upo kwenye kipindi cha mpito, haujawahi kuwa safi 100%, kumekuwa na figisu figisu, sio tu kwenye shirikisho, bali pia kwa viongozi wa vilabu, wachezaji, marefa na hata waandishi wa habari za michezo (watangazaji, wachambuzi) wamekuwa vituko na agenda zao ambazo hazina maslahi kwa mpira wetu.
Kwa wale watu wazima kidogo watakumbuka kuna kipindi matokeo ya mechi za ligi yalifutwa na Waziri wa Michezo wa wakati huo, Mh. Fatma Said Ali baada ya baadhi ya timu kufungana magoli mengi (mfano 5-5) katika mechi za kufunga msimu – kwa kifupi matokeo yalipangwa!
Tunakumbuka tuliwahi kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya timu za Taifa kwa vijana baada ya mchezaji wetu mmoja kubainika alidanganya umri (ukifikiri vizuri utaona hiyo chain ya kutengeneza huo uongo ilivyo kubwa – mchezaji anahusika, shirikisho linahusika, hadi mamlaka iliyompa hati ya kusafiria).
Suala la kudanganya umri bado ni mtihani mkubwa kwenye soka letu, jambo ambalo tunalikana hadharani lakini kwenye kificho sote tunakubaliana kwamba tunadanganya umri wa wachezaji wa timu za vijana. Kuna suala la kupanga matokeo, mengi yamesemwa kuhusu hilo jambo, zipo taarifa pia baadhi ya wachezaji wanacheza kamari tena kuhusu mechi za vilabu vyao.
Inasemekana marefa nao hawapo nyuma kwenye betting, tena wana bet mechi ambazo wao ndio wanachezesha. Zipo taarifa pia wamiliki wa vilabu pia wanacheza kamari, tena kwa mechi zinazohusu vilabu vyao.
Ukiwa na shirikisho linaloweza kushiriki kwenye mchezo wa kudanganya umri, ukiwa na viongozi wa vilabu wanaoweza kushiriki mchezo mchafu wa kupanga matokeo (rejea mechi zilizofutwa na Waziri wa Michezo enzi za ligi daraja la kwanza – naamini zipo nyingi ila hatuzijui!), ukiwa na waandishi/watangazaji/wachambuzi wa soka wanaoweza kupotosha kwa maslahi binafsi.
Ukiwa na ligi ambayo kuna tuhuma kwamba wachezaji wana bet mechi wanazozicheza wao, marefa pia wanafanya hivyo hivyo kwenye mechi wanazochezesha, wamiliki wa vilabu nao wanaweka mikeka kwa mechi zinazohusu klabu wanazozimiliki, tunashangaa nini mechi kuahirishwa na Bodi ya Ligi kwa shinikizo la moja ya vilabu?!
Uamuzi wa Bodi ya Ligi kutangaza tarehe mpya ya derby na taarifa rasmi ya klabu ya Yanga kwamba hawatapeleka timu ni hatua nzuri sana. Nasema tumefika patamu, wanapogombana watu wanaojuana na waliofichiana siri zao kwa muda mrefu ni jambo zuri kwa watu baki.
Ni faida kwa mpira wa Tanzania, ni wakati wa kujua madhaifu ya viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza vilabu na taasisi za mpira wa miguu Tanzania. Hofu yangu ni moja tu, je wanamanisha kweli?? Bodi ya Ligi itasimamia msimamo wake wa mechi kuchezwa kama ilivyosema? Je Yanga nao watasimamia msimamo wao wa kutokupeleka timu uwanjani?
Chaguo ni lao, aidha Bodi na Yanga wasimamie maamuzi yao tuanze upya kwenye soka letu au mmoja aamue kutumia ‘busara’, tuendelee na business as usual!
Yesu aliwajibu kwa kusema: “Yeyote aliye miongoni mwenu asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”
Alamsiki.
Comments
Loading…