ARNE SLOTS ni bingwa wa Ligi Kuu England. Ujio wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 kwenye Ligi ya EPL haukutegemewa kama angeiibuka na taji hilo ndani ya msimu wa kwanza akiwa hana uzoefu nayo, na mara ya kwanza kufundisha timu kubwa kama Liverpool alirithi mikoba ya Jurgen Klopp. Slots aliingia Liverpool bila kuwa na mashabiki wengi wala kujulikana kwa umahiri wake katika soka nchini England.
Baada ya kushuhudia umahiri wa Arne Slots, sasa kizazi kipya cha makocha kipo tayari kuchukua hatamu na kutamba katika timu mbalimbali. Wapo makocha vijana ambao wameonesha ishara ya kuwa moto wa kuotea mbali.
TANZANIA SPORTS inachambua Kwa kina kuhusiana na kizazi kipya cha makocha ambao wanasifika Kwa Ufundi na umahiri wa ushawishi katika ufundishaji. Kwa mfano Arne Slots umahiri wake ulianza kuonekana katika klabu ya Feyenoord ya Uholanzi ambapo mabosi wa Liverpool waligundua namna alivyo na uwezo kwenye kazi yake na haikuchukua muda mrefu kumtangaza kama kocha wao ajaye baada ya Jurgen Klopp ingawa alikuwa mgeni machoni pa wadau na mashabiki wa Soka.
Naam, sasa inaonesha dhahiri mashabiki na wadau wa Soka Ulaya wanakwenda kushuhudia kizazi kipya cha makocha ambao watatamba katika timu mbalimbali. Ni makocha vijana ambao wapo tayari kuweka alama katika kazi zao. Wafuatao ni baadhi ya makocha wanaotarajiwa kufanya mambo makubwa kwenye kandanda batani Ulaya.
SEBASTIAN HOENESS

Pengine unaposoma jina hili kitu cha kwanza unakumbuka la mwisho Kwa sababu ni maarufu nchini Ujerumani. Umaarufu wa jina la Hoeness unatokana na mkongwe wa Soka kutoka klabu ya Bayern Munich, Uli Hoeness. Hata hivyo Sebastian Hoeness ni mpwa wa Uli Hoeness. Sebastian Hoeness ana umri wa miaka 42 na kazi yake inaonekana dhahiri. Alikuwa kocha wa kwanza kuongoza kikosi cha wachezaji wa akiba kutwaa ubingwa wa Ujerumani katika Ligi Daraja la tatu nchini Ujerumani wakati alipokuwa anakinoa kikosi cha vijana wa Bayern Munich katika msimu wa 2019/2020.
Raundi ya pili ya msimu wao ilikuwa imetawaliwa na matokeo mazuri ambapo walikusanya alama 43 kutoka 57 zilizotarajiwa na hapo ndipo klabu yake ilipoanza kuongeza ufuatiliaji wa kazi yake. Kutokana na mafanikio hayo, mabosi wa klabu ya Hoffenheim alibaini uwezo na kipaji cha kocha huyo na moja Kwa moja walimtangazia dau la kufundisha klabu yao katika Ligi Kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga. Tangu alipochukua jukumu la kufundisha klabu hiyo alifanikiwa kumaliza katika nafasi za katikati. Maarifa yake yalowavutia pia mabosi wengine wa klabu ya Stuttgart. Sebastian Hoeness alifanya kazi bora akiwa Stuttgart ambapo alimaliza Ligi akiwa nafasi ya pili nyuma ya Bayer Leverkusen ambao walitwaa ubingwa msimu uliopita. Stuttgart walionesha makali yao katika Bundesliga wakiwa na mshanbuliaji hatari Serhou Guirassy kabla hajahamia Borussia Dortmund.
Ufundishaji wa Sebastian Hoeness unafananishwa na Hansi Flick na anapenda kutumia mfumo 4-2-3-1, pamoja na mshambuliaji wa asili ambaye anafanya kazi ya kupachika mabao kwa mtindo wa aina yake. Kutokana na ubora wake ni suala la muda tu kwa vilabu vikubwa zaidi kumchukua kocha huyo.
THIAGO MOTTA
Usidanganyike na uamuzi wa klabu ya Juventus kumfukuza kazi kocha huyu. Motta ni miongoni .wa makocha ambao wanakuja juu katika kazi hiyo na anatazamwa kama kocha mtarajiwa wa Timu ya Taifa ya Italia.
Ni vigumu kusema hapana, pale timu kubwa zitakapotaka huduma yake ya ukocha baada ya kuongoza kikosi cha Bologna katika mafanikio mazuri msimu huu. Lakini timu iliyomfukuza yaani Juventus inapoteza mechi nyingi za Ligi Kuu Italia huku Thiago Motta akitamba katika kikosi kipya cha Bologna. Kwanza ni kocha kijana ambaye amepitia nyakati ngumu kuunda kikosi cha kumpa ushindi pamoja na kucheza katika falsafa yake. Matarajio makubwa yaliyokuwa kwake akiwa Juventus hayakuendana na uhalisu wa kikosi chenyewe. Lakini ndani ya klabu ya Bologna mambo yamekuwa mazuri na kuonesha nani alikosea kati ya mabosi wa Juventus waliomfukuza na Thiago Motta wa Bologna ambao wanapambana katika nafasi nne za juu katika msimamo wa Serie A.
Matokeo mabaya yalimfikuzisha kazi yake kwenye klabu ya Juventus mwanzoni mwa mwaka huu. Hadi sasa jina lake ni miongoni mwa yale yanayotajwa kuchukua nafasi ya ukocha kwenye klabu za Ligi Kuu England. Sifa yake kubwa ni msimamo wake katika falsafa ya ufundishaji, ambapo amekataa Katakata kubadilisha, na hivyo inaendana na msimamo wa makocha kama vile Pep Guardiola au Ange Postecoglou.
“Nilipokubali kuchukua kazi ya ukocha nikiwa na Ari na matumaini makubwa, nilifahamu ni mradi wa miaka mitatu, ambao unategemea Mapinduzi kwa wachezaji na timu itakayoundwa yenye shauku ya kutwaa mataji. Nilifahamu vyema kwamba klabu kama Juventus unapaswa kushinda mechi. Lakini mpango wenyewe haukuleta matokeo chanya niliyotarajia na kudhania.”
Licha ya kufukuzwa Juventus, Motta amefanya kazi nzuri akiwa kocha Kwa kuongoza kikosi cha Bologna. Kikosi chake kinasifika kwa ukabaji wa hali ya juu, mashambulizi mfululizo na Soka la Kasi. Pia amekuwa akichezesha wachezaji katika mzunguko kwa kuwapa nafasi wengi na kuinua viwango vyao. Naye anatajwa kuwa miongoni mwa wanaowindwa na matajiri wa Vilabu vya England.
EDIN TERZIC
Terzic ana leseni ya UEFA daraja sawa na ya Graham Potter, Nemanja Vidic na Nicky Butt.
Potter anaonekana kuwa bahati katika kazi yake kuliko Terzic. Mafanikio ya Edin Terzic ni kukiongoza kikosi cha Borussia Dortmund katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka Jana dhidi ya Real Madrid. Timu yake pia ilikosa ubingwa wa Ujerumani wa Bundesliga Kwa tofauti ya mabao katika mchezo wa mwisho wa kumaliza Ligi 2022/2023 mbele ya Bayern Munich.
Tangu alipojiuzulu katika klabu ya Dortmund msimu uliopita, hajachukua jukumu lingine hadi sasa. Terzic ana umri wa miaka 42, bado anayo nafasi kubwa ya kuonesha umahiri wake.
Moja ya matukio ya kukumbukwa msimu uliopita ni pale alipochukua jukumu la kujifanya mlinzi wa Uwanjani (Stewart) wakati alipoingia kwenye mazoezi ya Siri ya Real Madrid ili kuwajua wachezaji wao wa kupiga penalti endapo timu hizo zingefikia hatua huyo msimu uliopita.
Mbinu za timu yake ni kuhakikisha wanamiliki mpira zaidi ya wapinzani wao na mchezo wake unakuwa wa Kasi zaidi pamoja na kushambulia kwa kushtukiza. Terzic alianza kazi ya ukocha kama mchambuzi wa mifumo ya uchezaji wa timu pinzani.
DOMENICO TEDESCO
Huyu ni kocha wa kipekee kwani anatajwa kuwa na mbinu tofauti na makocha wengine. Tedesco anaeleza kuwa, “Daima nataka timu yangu ijigawe katika maeneo mawili. Napenda kujilinganisha na bondia, ambaye hayupo tayari kuangushwa. Zaidi ya hapo, nataka kushinda vita vya kumiliki mpira haraka kwa sababu napenda kushambulia, hasa kwa kuangalia uwiano wa kutawala mchezo na kufungua njia za wapinzani ili kuwafunga,”
Heshima ya Tedesco imekuwa kubwa kwa miaka ya karibuni, lakini ndiyo kwanza ana umri wa miaka 39 na tayari anaonekana kuwa na uzoefu Fulani katika ufundishaji kulinganisha na umri wake. Kocha huyo wa zamani wa Ubelgiji alikiongoza kikosi cha Spartak Moscow kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kujiunga na RB Leipzig ambako alitwaa taji la German Cup msimu uliopita.
Bahati mbaya msimu uliofuata hakupata matokeo mazuri hivyo mabosi wake wakaamua kumpa mechi za kuokoa kibarua chake. Hata hivyo mwaka 2023 alikubali kuchukua kibarua ya kuinoa Ubelgiji. Akiwa na kikosi cha dhahabu ambacho umri ulikuwa unawatupa mkono, hakufanikiwa kupata taji la Euro mwaka 2024 kutokana na kiwango kibovu cha nchi hiyo kwenye mashindano na mechi za kirafiki. Matokeo mabovu yalisababisha golikipa namba moja Thibaut Courtois kukataa kuchezea timu ya Taifa ya Ublegiji kabla ya kufanya mazungumzo na kocha wake huyo mapema Januari mwaka 2025 ili arudi kuchezea timu ya Taifa ya Ublegiji.
Licha ya matokeo mabovu, Tedesco anawindwa na vilabu mbalimbali ambavyo vinahitaji huduma yake.
MATTHIAS JAISSLE
Kwanza ni kijana na pili ni kocha mwenye uwezo mzuri na tumaini katika mchezo wa Soka. Yupo katika orodha ya makocha wanaotarajiwa kufanya vizuri akiwa anaonesha cheche zake huko Saudi Arabia. Viongozi wa klabu mbalimbali wamekuwa wakijaribu kumtafuta na kumvutia kwa mikataba minono lakini Jaissle amekuwa mtulivu na anaelewa umuhimu wa kujitengenezea wasifu bora kwenye mchezo unaopendwa zaidi duniani wa Soka.
Jaissle alianza safari yake ya soka katika mazingira magumu kwenye klabu ya Liefering huko Austria, ambapo alifanikiwa kuipeleka Ligi Kuu toka daraja la kwanza na kumaliza msimu akiwa katika nafasi nzuri.
RB Salzburg walimwajiri na akakiongoza kikosi Chao katika Ligi Kuu na mashindano ya Europa League katika hatua ya makundi kabla ya kuondoka klabuni hapo siku moja kabla ya kuanza msimu mpya. Taarifa ya klabu hiyo kutangaza kuondoka Kwa kocha wao ilisema “Tunaamini kwamba tunataka kuanza msimu mpya tukiwa kamili Kwa nguvu, maarifa na ari isiyotiliwa mashaka. Ili kufanikiwa hilo ni lazima tukiri kuanza kusimamia eneo la kocha ambaye atakuwa tayari kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya timu. Anayeshindwa basi hapawezi kuwa mahali pake pa kazi.”
Baada ya hapo kocha huyo alijiunga na klabu ya Al-Ahli, ambayo ilikuwa imewasajili Roberto Firmino na Ivan Toney na kuzua mjadala ni nafasi ipi ingefaa kwao na kocha angechukua uamuzi gani katika kuwapanga mastaa hao.
Kana Kwamba haitoshi
Jaissle alikiongoza kikosi hicho kumaliza msimu wakiwa nafasi ya tatu katika msimu wake wa kwanza. Kwa sasa ana umri wa miaka 37 na dalili njema za kuwa kocha mahiri zaidi Ulaya zinaonekana, kwani uwezekano wa yeye kutodumu katika Ligi ya Saudi Arabia ni Mkubwa.
FRANCESCO FARIOLI
Ni makocha wangapi wamesomea falsafa katika chuo cha Florence? Kwa hakika ni safari ya aina yake Kwa kocha huyu mwenye umri wa miaka 36 ambaye sasa anainoa klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Farioli aliachana na masomo yake ya falsafa Chuo kikuu ili kuwa kocha wa Soka. Farioli haijawahi kucheza mpira wa miguu katika ngazi yoyote , lakini amedhihirisha kuwa anaweza kuwadhihirishia wadau wa Soka kuwa anamudu kazi hiyo. Alianza safari ya ukocha akiwa kocha wa makipa kwenye klabu ya Margine Coperta, ambayo ni ndogo huko nchini Italia, kabla ya kujiunga na klabu ya Lucchese ya daraja la tatu. Malengo ya kuwa kocha mahiri yalimpeleka nchini Qatar kufundisha kama kocha wa makipa wa watoto chini ya umri wa miaka 16 na huko ndiko alikutana na kocha Roberto de Zerbi. Haukutegemewa kuwa kukutana na kocha huyo kama kungeleta matokeo mazuri na safari yake ya ukocha hadi kuwa miongoni mwa wale wanaodhaniwa kuwa makocha bora vijana barani Ulaya.
De Zerbi alimchukua Farioli na kwenda naye kwenye kikosi cha Benevento na baadaye Sassuolo. Alibadili mwelekeo kutoka kuwa kocha wa makipa hadi kuwa kocha msaidizi wa Klabu ya Alanyaspor huko Uturuki, kisha alijiunga klabu ya kwanza kama kocha mkuu Fatih Karagümrük, akiwa na umri wa miaka 31.
Farioli alifanya vizuri katika klabu hiyo na ikawa sababu ya kuajiriwa katika klabu yake ya zamani Alanyaspor kabla ya kwenda klabu ya Nice ya Ufaransa. Akiwa klabu ya Nice walifuzu mashindano ya Europa League. Mwezi Mei mwaka Jana aliajiriwa rasmi kama kocha wa Ajax Amsterdam ya Uholanzi. Akiwa kocha wa kwanza toka Italia kufundisha klabu hiyo.
Mfumo wake wa ufundishaji unafanana na kocha Roberto De Zerbi lakini sehemu Kuu ya falsafa yake ni namna anavyounganisha timu, kushambulia, kutafuta mabao kwenye boksi la adui pamoja na kucheza jwa Kasi, pasi fupi, kufungua nafasi, haraka na mabadiliko ya nafasi ndani ya mchezo. Hizo ni mbinu zilizomoa taji la Uholanzi. Farioli amekuwa akihusishwa na timu mbalimbali kama vile Roma.
CESC FABREGAS
Ni maarufu zaidi duniani kwa uchezaji wake alipokuwa Arsenal, Barcelona na baadaye Chelsea. Huyu ni maarufu zaidi kuliko makocha wengine katika orodha hii Kwa sababu alikuwa mmoja wa viungo bora katika mchezo wa Soka akiwa ametamba katika Ligi za England na Hispania. Pia ni mshindi wa Kombe la Dunia. Lakini nini hasa kilichomfanya awe kocha?
Mwaka 2023, alichukua jukumu la kuwa kocha wa kikosi cha pili cha klabu ya Como na kile chini ya miaka 19. Baadaye aliajiriwa kama kocha wa muda timu ya wakubwa ya Como. Hata hivyo haluruhusiwa kufundisha timu hiyo kwa sababu hakuwa na cheti cha ukocha cha UEFA, hivyo alibaki kuwa kocha msaidizi wa Como hadi alipoteuliwa rasmi kuwa kocha mkuu mwaka 2023 Kwa Maktaba wa miaka minne.
Fabregas amekulia katika mfumo wa 4-3-3 akiwa Barcelona, ni sababu hiyo hadi katika kazi ya ukocha anatumia mfumo huo. Anataka kuona viungo watatu katikati ya dimba ambao wanabadilishana majukumu ndani ya mchezo kuliko kuwa na viungo wa asili wa Namba 6, 8 na 10.
Akizungumzia mfumo humo, Fabregas aliliambia gazeti la The Guardian alisema “Najaribu kuwapigia simu watu waliokuwa kwenye nafasi hiyo Kwa muda mrefu. Malengo yangu ni kuimarisha timu, kwahiyo nataka kuzungumza na kujadiliana kupata suluhisho. Nataka kuchota mawazo ya kiufundi kutoka kwa watu wanaonizunguka, hiki ni kitu ninachokifanya Kila siku. nilipokuwa mchezaji chini ya Arsene Wenger , José Mourinho, Antonio Conte, Luis Aragonés na Vicente del Bosque nimepata bahati ya kujifunza mengi.”
Licha ya Como kumaliza msimu wakiwa nafasi za katikati, Cesc Fabregas anahusishwa na kibarua cha kufundisha Roma akiwa na umri wa miaka 37 tu, huku timu zingine za EPL zinamtazama kama mtu sahihi wa klabu zao.
Comments
Loading…