MASHINDANO ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yamefika hatua ya nusu fainali. Katika mechi za kwanza za nusu fainali, Arsenal walifungua dimba dhidi ya miamba ya Ufaransa, PSG. Mchezo wa pili ulikutanisha miamba ya Italia, Inter Milan na Barcelona ya Hispania ambapo mchezo huo ulimalizika 3-3.
Katika mchezo kati ya PSG na Arsenal, vijana wa Mikel Arteta walicharazwa 1-0 lililofungwa na Ousmane Dembele kunako dakika 4 ya mchezo.
Kwa ushindi huo PSG wapo mguu mmoja ndani kuelekea fainali ya UEFA ambayo mwaka huu inatarajiwa kufanyika jijini Munich nchini Ujerumani.
TANZANIA SPORTS inachambua Kwa kina namna Arsenal inavyoweza kupindua matokeo ya kutoka kufungwa hadi kuibuka kinara na kutinga fainali. Ikumbukwe Arsenal na PSG zote hazijawahi kutwaa taji la UEFA na msimu huu zipo katika nafasi nzuri ya kuandika rekodi zao. Je ni namna gani Arsenal wanaweza kuibuka na ushindi huko Ufaransa?
KUWATAZAMA LIVERPOOL
Arsenal kwa namna yoyote Ile wanatakiwa kuwatazama Liverpool walivyocheza dhidi ya PSG jijini Paris. Liverpool waliibuka na ushindi 1-0 dhidi ya PSG wakiwa ugenini. Ingawaje PSG waliishinda Liverpool katika mchezo wa marudiano baada ya kupachika bao la mapema na kwenda katika hatua ya matuta.
Liverpool waliimudu PSG Kwa kushambulia muda wote wa mchezo. Safu ya ushambuliaji ilikuwa na wachezaji watatu ambao walikuwa na kazi moja tu; kuhakikisha walinzi wa PSG hawatulii na hawapati nafasi ya kupanda mbele. Mabeki wa PSG wanapopanda mbele wanawapa mwanya viungo wao kuwa wazalishaji zaidi na Kwa mchezo wao wa Kasi wanaweza kuleta madhara langoni mwa Arsenal. Hivyo basi njia ya kwanza ya Arsenal ni kutazama mechi zote mbili za PSG na kuridia tena jinsi walivyofungwa na walivyoshinda.
VITA YA KIUNGO
Hili ni eneo ambalo limebeba Siri nyingi za PSG. Viungo wao watatu wanafanya kazi ya kuziba eneo la kulia la Arsenal na pia huwa wanakwenda kuziba eneo la kushoto la Arsenal. Ukiangalia mtiririko wa timu ya PSG katika mchezo wa kwanza unabaini kuwa walichofanya na kuwazuia Arsenal ni jinsi ya kujilinda na kutawala mchezo walivyotaka wao. Eneo la Ulinzi wa kati halikuwa limepata mashambulizi mengi lakini nafasi kadhaa zilitengenezwa na Arsenal. Vijana wa Mikel Arteta walizidiwa maarifa katika eneo la kiungo hasa Vintiha ambaye alikuwa anapoozesha mchezo na kuifanya timu icheze itakavyo kuliko kuathiriwa na uchezaji wa Arsenal.
GOLI LA MATUMAINI
Arsenal walikosa kitu kimoja tu; goli. Laiti wangekuwa na mshanbuliaji mwenye uwezo wa kupachika mabao katika mazingira magumu ama tuseme ya aina yoyote bila shaka wangekuwa na magoli mengi ya matumaini ya ushindi. Timu yao inatengeneza nafasi nyingi za kufunga. Viungo wao Martin Odegaard, Gabriel Matinelli, Bukayo Saka, Trossand ni wachezaji ambao wanahitaji mtu mmoja anayejua kucheka na nyavu. Mtu huyo sio Kai Havertz Kwa sababu hana uwezo wa kupachika mabao angalau 25 Kwa msimu.

Mechi nyingi za EPL na UEFA Arsenal wanajikuta katika mazingira magumu Kwa sababu upachikaji wao wa mambo ni hafifu. Ikumbukwe si suala la kukosekana Gabriel Jesus bali hata kupata huduma ya mshanbuliaji ambayo inihalikishia timu kupata mabao muhimu na kutosha.
MKAKATI WA ULINZI
PSG wanajivunia Ubunifu wa wachezaji wao katika eneo la kushambulia. Goncalo Ramos ndiye anaonekana kuwa mshanbuliaji ambaye anafaa kucheza eneo la namba 9. Lakini PSG wana wachezaji wa aina ya Arsenal, tofauti yao ni kwamba Wana Kasi kuwazidi vijana wa Mikel Arteta. Safu ushambuliaji ya PSG imejaa wabunifu na mawinga ambao wanatumika kucheza kama washambuliaji Kwa sababu wa muono mzuri wa kupachika mabao.
Mkakati wa kwanza wa Arsenal lazima uwe kuzuia kufungwa magoli ya mapema. PSG waliitoa Liverpool kwa mkakati wa goli la mapema. Wamekwenda kucheza na Arsenal wamefanya kitu kilekile; kufunga goli la mapema Kisha kuanza kujilinda. Hii Ina maana safu ya ulinzi ya Arsenal inapaswa kutengenezwa kiakili kuelewa mazingira ya dakika 15 za kwanza ambazo zinakuwa hatari zaidi.
LANGO LA PSG
Wamefika nusu fainali kwa mchango wa uhodari wa Idara la golikipa. Arsenal licha ya kutengeneza nafasi nyingi lakini walikwama Kwa golikipa wa PSG, Donnarumma. Golikipa huyo si wa kumwendea na mashuti kuelekea langoni, badala yake unahitajika mkakati maalumu ambao utawezesha timu hiyo kupenya kwenye lango la PSG. Umahiri wa safu ya ulinzi unajengwa na Donnarumma mbali ya mchango wa mabeki wake. Kwahiyo ili Arsenal angalau wapate bao ni lazima wachezaji watatu wawe kwenye boksi la adui huku watatu wakiwa nje ya 18. La pili, ni lazima Arsenal wahakikishe wanaweza kufanya mabadiliko ya kimbinu ikiwemo kuachana na mipira ya krosi, badala yake wachezeshwe Kwa pasi nyingi wanapokuwa nje ya 18 ya PSG.
KASI YA MCHEZO
Arsenal watarajie kukutana na Kasi kubwa ya mchezo katika mechi ya marudiano. PSG watajivunia bao lao na hivyo watalitafuta jingine haraka sana. Kwahiyo Kasi ya mchezo inatarajiwa kuonekana kuanzia mwanzoni na 4-1-4-1 ndiyo inayopa nafasi nyingi za kuwashinda maadui wao. Kwa mfumo huo wanaweza kushambulia kwa Kasi na kushtukiza wakiwa watano kuelekea lango la adui huku wakijilinda Kwa wachezaji wanne nyuma, huku mbele yao anakuwa mmoja Kwa lengo la kulinda eneo lao linapotoka shambulizi la haraka la maadui.
Kila Idara, winga, viungo na safu ya ushambuliaji lazima zifanye kazi ya ziada katika mchezo wa mkondo wa pili.
ReplyReply allForward |
Comments
Loading…