in , , , ,

Simba katika fainali kwa mkubwa mwenzake

KWA mara ya pili klabu ya Tanzania inatinga Fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya Simba kufanikiwa kuwatupa nje Stellenbosch FC ya Afrika kusini kwenye mchezo wa marudiano. Katika mchezo uliofanyika kwenye dimba la Moses Mabhida nchini Afrika kusini, Simba wakicheza soka la timu kubwa, utulivu na kuufanya mchezo uende wanavyotaka wao, ilikuwa silaha muhimu iliyowafakikisha kwenye ushindi na kutinga fainali. 

Kikosi cha kocha Fadlurahman Davids kiliingia katika mchezo huo wa ugenini kikiwa na faida ya bao moja waliloshinda kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye dimba la Amaan Complex visiwani Zanzibar. Katika mchezo huo Stellenbosch FC walitakiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ili kujihakikisha nafasi ya kutinga faiali lakini juhudi zao ziliishia miguuni mwa Simba. 

TANZANIASPORTS inachambua kwa kina mchezo huo na maana yake kwa Ligi Kuu Tanzania pamoja na wachezaji wenyewe. Lakini pia inaangalia namna kikosi cha Steve Barker kilivyoshindwa kuchachafya kwenye lango la Simba hadi kutolewa. 

Fadlu akitaka anaweza kukataa

Benchi la ufundi la Simba lina sifa moja muhimu; kuelewa mahitaji mchezo na namna ya kucheza na mpinzani wao. Kwenye mechi dhidi ya Stellenbosch, kocha Fadlu Davids hakuangaika kuwaagiza mengi wachezaji wao, lakini mar azote ishara zake na maelekezo ilikuwa ‘tulieni’. Angeweza kumitwa Hamza, na kumpa ishara ya mikononi “kuweni watulivu, tulieni”. Hapo hapo angeweza kumwita Kibu Dennis, “nenda pembeni” yaani akiwa anataka acheze eneo la winga pembeni ili kuwanyima nafasi wapinzani wao. 

Jambo la pili ambalo Fadlu Davids analifanya ni kuhakikisha anawachezesha wapinzani wake kadiri anavyotaka. Kwenye mchezo wa hatua ya awali dhidi ya Al Ahly Tripoli aliwawapelekesha kwa kasi kuanzia mchezo wa kwanza akiwa Libya hadi ule wa marudiano. Mechi zao zote walikuwa wakicheza kwa kasi mno kuanzia dakika ya kwanza hadi 90. 

Mechi dhidi ya Al Masry, Simba waliweka mchezo mzima mkononi mwao, lakini makosa madogo yaliwagharimu. Mwalimu aliyaona hayo, na katika mchezo wa marudiano akautaka mchezo huo kwa kucheza kwa kasi. Al Masry ya Misri walikutana na kasi kubwa ya mchezo na wakapigwa mabao 2-0 ndani ya dakika 90, kabla ya kwenda hatua ya matuta. Kwahiyo Fadlu Davids kuna muda anataka na muda mwingine hataki. Kila mechi ina mikakati ambayo inawapa ushindi kwa namna wanavyotaka.

Akiamua kutumia mawinga, basi anataka kuwarudisha nyuma wapinzani wao. Lakinidi dhidi ya Stellenbosch aliuweka mchezo katika boksi la nje ya 18 za adui. Mshambuliaji hakupaswa kwenda mbali na eneo la 18 na hakutakiwa kuingia kwenye boksi la 6 haraka badala yake alitakiwa kudhibiti mpira na kugawa kwa viungo au mawinga. Kazi Steven Mukwala aliifanya vyema Zanzibar na Afrika kusini, bahati mbaya nyavu hazikutikiswa ipasavyo. 

Ni sababu hii alimhitaji Mukwala kuliko Lionel Ateba. Kama unamhitaji Ateba maana yake unataka kukimbizana na mabeki wa timu pinzani. Lakini ukiwa na Mukwala unahitaji kudhibiti mpira na kuwavuta viungo wako wasogelee eneo hilo. Ni sababu hii washambuliaji wa Simba licha ya kukosa nafasi nyingi, lakini viungo ndio walikuwa na fursa ya kufunga kuliko washambuliaji.

Ukuta wa kiungo

Tanzania Sports
Wachezaji wa Simba Sc, wakimbeba kwa furaha kocha wao Fadlu Davids

Unaweza kuwasifia mabeki wa Simba kwa ushirikiano na uwezo mkubwa wa kuwadhibiti washambuliaji. Lakini kabla ya hapo unapaswa kuwaangalia watu wawili wa katikati ya dimba wanaotengeneza ukuta katika kikosi cha Simba. Ni Fabrice Ngoma na Yusuf Kagoma. Viungo hawa wameifanya safu ya ulinzi ya Simba iwe inamalizia kazi ngumu wanayofanya. Kwa asili wao si wapishi wa mashambulizi, bali walinzi wa walinzi, yaani kazi yao kuwalinda walinzi wa Simba. Hivyo mbele yao wanahitaji kiungo atakayewapa utamu washambuliaji, na ndipo anapocheza Jean Ahoua au Fernandez. Ukuta huu umekuwa ukizuia mipango na kutibua mbinu nyingi za wapinzani, na ndiyo silaha muhimu ya Simba. Wapewe heko.

Stellenbosch ni mtoto mbele ya wakubwa

Simba ulikuwa ni mloima mrefu sana kwa Stellenbosch fc. Kihistoria Simba walikuwa wkaubwa mno na vijana wa Stev Barker walikosa kile walichokuwa nacho Simba; uzoefu. Vijana wengi wa Stellenbosch walikuwa wana hamu ya kufunga au kuishambulia huku wakisahau kuwa wanacheza dhidi ya timu inayoelewa namna ya kuwatupa nje ‘watoto wa namna hiyo’. 

Mawinga wa Stellebosch na mshambuliaji wao De Jong walikuwa na kazi moja tu kupambana na Simba kwa kutumia kasi na nguvu. Bahati mbaya kwa mawinga hao hawakuwa na muono mzuri kuhusiana na upigaji wa krosi au pasi mpenyezo kuingia eneo la hatari la Simba. Stellenbosch hawana ujuzi wa kuvuruga wapinzani (mind games). Mbinu zao za kutegemea krosi na mipira ya kurushwa ilikuwa ya kizamani. Unapocheza na timu kama Simba ambayo haiogopi lolote ni dhahiri unahitaji zaidi ya mbio na krosi.

Ushindi wa Simba umeonesha pia ni sahihi kwa klabu hiyo kutinga fainali kuliko Stellenbosch. Sababu ni kwamba RS Berkane walikuwa mbele kwa mabao 3 dhidi ya Constantine ya Algeria, ni timu imara na ndiye bingwa mtetezi. Kiuchezaji Stellenbosch wasingekuwa wapinzani wazuri kwa RS Berkane. Simba wana uwezo wa kupambana na RS Berkane katika mchezo wa fainali kuliko Stellenbosch kutokana na ina ya uchezaji, uzoefu na uwezo  wa mchezaji mmoja mmoja.

Wakubwa wanakutana

Katika mchezo wa fainali bila shaka yoyote wakubwa wanakutana. RS Berkane watakuwa wametazama mechi za Simba ili kuelewa uchezaji wao. Fadlu Davids si mgeni wa Berkane kwa sababu anafahamu soka la Morocco vyema tangu alipokuwa msaidizi katika klabu aya Raja Casablanca. Kwahiyo mchezo wa fainali unakutanisha wakubwa watupu. Simba wana uzoefu na wamekutana na timu nyingi toka Afrika kaskazini, na pia wanaanza fainali hii wakiwa ugenini na mechi ya marudiano itachezwa jijini Dar Es Salaam. Hii ni fainali ya wakubwa. 

Je wapi Steve Barker alipokosea?

Kikosi cha Stellenbosch kilikosa maarifa ya kupenya safu ya ulinzi ya Simba. Jambo la pili Stellenbosch inaonekana kuundwa na viungo na mawinga kuliko washambuliaji. Aina ya wachezaji wao sio wale wa kupambana na mabeki, sio wale ambao wanaweza kulielewa lango lilivyo ndio maana ushindi wao mwingine ulikuwa mwembamba kwenye mechi nyingi. Faida ya aina ya wachezaji hao ni pale unapokutana na timu isiyojua kulinda lango lake na kuzidiwa na presha. 

Wachezaji wake ni wenye kasi bila muono wa mbali wa namna timu inavyoweza kupachika mabao. Mbaya zaidi timu yenerywe inategemea adhabu ndogo kama vile kona, mipira ya kurusha nafaulo kupata ushindi. Pia ni timu inayoundwa kuachiwa uhuru wa kucheza yaani wapewe uhuru bila kutibuliwa mipango yao. kama kitu wanapaswa kufanya ni usajili wa washambuliaji angalau watatu kuimarisha timu yao katika ufungaji na upatikanaji wa mabao.

Pia, kipindi cha pili aliwarudisha kwenye msingi wa kupiga pasi fupi kuelekea lango la Simba, ambapo mtindo huo hufanywa na Simba mara nyingi. 

Simba ya Fadlu ukitaka kubutua wanaweza, ukitaka pasi fupi wanazijua, kwahiyo hatua ya kwanza ni kutibua mbinu za mawinga na viungo. Viungo wa Stellenbosch ni watengenezaji sio wafungaji. Kwahiyo pale kwenye safu ya ushambuliaji yao hakuna mshambuliaji w akuitisha Simba. Walifia hapo.

Nyayo za Yanga

Ni dhahiri soka la Tanzania ngazi ya vilabu linazidi kuongeza chachu na kujitanagza zaidi baada ya klabu ya Simba kufuata nyayo za watani wao wa jadi Yanga ambao wamewahi kutinga fainali ya Kombe hilo kabla ya kufungwa na USM Alger ya Algeria. Yanga walikuwa wakiwatania watani wao hao kuwa hawana mafanikio kwenye mashindano ya CAF, lakini sasa tayari Simba wamefikia rekodi ya Yanga na hakuna tena kutambiana.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

67 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Bahati iko mbali ya ubora wa Rhulani Mokwena? 

Tanzania Sports

Je, Arsenal watapindua matokeo mbele ya PSG?