in

Yanga bado inaomba omba?

kikosi cha yanga

Kati ya kosa kubwa ambalo Yanga wanaruhusu kulifanya kila siku ni wao kusubiri wafanye mabadiliko ndiyo waendeshe timu yao kibiashara. Inawezekana pia hata neno timu ya wananchi inachangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wasifiirie zaidi.

Wanaitumia vibaya kauli mbiu ya timu ya wananchi. Kwanini nasema hivi ? Inavyoonekana viongozi wa Yanga wanaamini kutumia mbiu ya timu ya wananchi kwao wao ina maana ya kuwaomba pesa wananchi kwa ajili ya kuendesha timu .

Sikatai, sipingani na kitendo cha Yanga kuwaomba wananchi pesa kwa ajili ya timu yao pendwa. Tatizo langu na viongozi wa Yanga ni wao kuwaomba wananchi pesa bila kuwapa chochote wananchi.

Njia nzuri ya kuomba pesa kwa mashabiki wa mpira wa miguu ni ya kuwapa kitu mashabiki na wao kutoa pesa kwa ajili ya kukipata hicho kitu. Haya ndiyo mazingira rahisi na sahihi ya kibiashara na siyo kuomba pesa kwa njia ya kuomba kusaidiwa.

Tupo kwenye ulimwengu wa kipebari. Ulimwengu ambao hauruhusu kuomba omba. Ulimwengu huu unaruhusu kubadilishana huduma na fedha. Nilifikiri Yanga wangetumia muda huu kufikiria namna sahihi ya kutengeneza huduma ambazo zingewafanya wananchi watoe pesa kwa ajili ya kuzinunua.

Muda huu Yanga wapo kwenye wiki ya mwanachi.  Wiki ambayo ilitakiwa iingize pesa kwa Yanga kila siku mpaka siku ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya mwanachi. Tatizo ni kwamba  viongozi wa Yanga wanasubiri mpaka siku ya mwisho ya wiki ya mwanachi ndiyo waingize pesa.

Viongozi wa Yanga wamechelewa sana kuzindua jezi zao. Walitakiwa kuzitambulisha mwezi mmoja kabla ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya mwanachi. Mwezi ambao ungetoa nafasi kwa mashabiki wa Yanga kuzinunua jezi kwa wingi.

Kuzindua jezi siku chache kabla ya kilele cha wiki ya mwanachi hii haitoi nafasi kubwa kwa wananchi kununua jezi kwa wingi. Ilitakiwa jezi zitambulishwe mapema. Zinadiwe kwa nguvu. Kuwe na hamasa kubwa ya kuzinadi jezi hizi ili watu wanunue kwa wingi.

Ilitakiwa zitengenezwe bidhaa zingine ambazo zina nembo ya Yanga kwa ajili ya wananchi kuzinunua. Viongozi wangefikiria hata namna ya kutengeneza skafu kwa ajili ya mashabiki wa klabu ya Yanga kwa kuziuza kwa bei nafuu.

Tuko kwenye dunia ambayo watu wengi wanatumia simu za kisasa “smartphone” watu hawa wangetengenezewa makava ya simu zao yenye nembo ya klabu ya Yanga. Vyote hivi ni kwa ajili ya kutoa nafasi kwa Yanga kutengeneza pesa kibiashara na siyo kuomba omba kama anavyofanya mwenyekiti wa klabu hiyo.

Kuomba omba wakati una mtaji mkubwa wa mashabiki kunaleta picha mbaya kwa nembo ya Yanga. Yanga inaonekana ni timu ambayo haiko kibiashara . Hivo ni ngumu kwa mwekezaji kuja kuweka pesa zake sehemu ambayo haiendeshwi kibiashara.

Mtaji wa mashabiki ni kitu cha msingi sana. Na ndicho kitu ambacho Yanga wanatakiwa kukitumia sana kwa ajili ya kutengeneza pesa. Watengeneze bidhaa nyingi za kuwauzia mashabiki na siyo kuwaomba omba mashabiki wao.

Wafikirie hata kuanzisha Gala ambayo itafanyika usiku wa baada ya siku ya wananchi. Gala ambayo itakuwa na vitu ambavyo vitatoa nafasi kwa Yanga kuviuza na kupata pesa kutoka kwa makampuni na wageni waalikwa kwenye gala husika kuliko kukaa na kuomba omba.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
CL

Yaliyoshangaza zaidi katika fainali ya UEFA

Messi

Natamani MESSI acheze na RONALDO