Klabu za England zimetupiwa lawama kwamba huajiri makocha kwa ubaguzi, wakiwaacha wenye rangi nyeusi hata kama wana uwezo.
Taasisi inayopambana na ubaguzi wa rangi michezoni, Kick It Out imesema kwamba mfumo uliopo si wa haki, unalenga baadhi ya watu na kutupa wengine nje, ambapo wenyeviti au wamiliki wa klabu wamebainika kuajiri makocha kwa kutozingatia vigezo.
Taarifa kutoka kwa asasi hiyo imesema kwamba kuna makocha wengi wazuri, lakini ama hawapewi nafasi au hufukuzwa kazi kirahisi kwa sababu ya rangi yao tu, wazo linalopingwa na mmiliki wa Wigan, Dave Whelan na Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho.
Whelan ambaye timu yake ilishuka daraja msimu uliopita anasema rangi au dini haviwezi kutumiwa katika kujadili mustakabali wa mtu kwenye michezo, hasa katika soka, akisema kila mmoja ni sawa duniani, hivyo mwenye uwezo apewe nafasi.
Mourinho kwa upande wake alisema kwamba watu wa soka si wapumbavu hivyo kwamba wafikie mahali kuwafungia milango watu fulani, akasisitiza hakuna ubaguzi kwenye soka. “Ukiwa na vigezo utapewa kazi, ukiwa juu upo juu tu,” akasema Mreno huyo.
Hata hivyo, mchambuzi wa soka wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Jason Robert ambaye ni mwanasoka wa kulipwa wa zamani na ni mweusi, alitoa mrejesho kwa mchango wa kocha huyo aliyepata kufundisha soka Ureno na Hispania akisema: “Mourinho – eti hakuna ubaguzi kwenye soka – kuna namna moja tu ya kutoa mrejesho katika hilo. Ni ya kizamani kidogo lakini; hahahahahahahahahahahahaha.”
Pamekuwa na mapendekezo kwamba kila klabu yenye nafasi wazi ya ukocha ilazimishwe kumfanyia mahojiano walau kocha mmoja mweusi au mwenye asili ya makundi yenye watu wachache, lakini Mourinho na Whelan wamepinga.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), Gordon Taylor aliiambia BBC wiki jana kwamba kulikuwa na upinzani wa siri miongoni mwa klabu za England katika kuajiri makocha weusi.
Kwa sasa, miongoni mwa klabu 92 zinazoshiriki Ligi Kuu ya England na ligi nyingine za soka chini yake, kuna makocha wawili tu weusi, nao ni Keith Curle wa Carlisle na yule wa Huddersfield, Chris Powell. Latika Ligi Kuu hakuna hata mmoja, waliokuwapo wamefukuzwa.
Walau asilimia 25 ya wachezaji kwenye soka hapa ni weusi au kutoka makundi madogo na nahodha wa zamani wa England, Paul Ince ametaka suala hilo lishughulikiwe haraka badala ya kuacha baadhi ya watu wakilisukumiza chini ya zulia kupotezea.
Mtu aliyeingiza sheria kama hiyo ya kuhakikisha weusi na walio wachache wanapewa nafasi mwaka 2003, Dan Rooney, amesema ingependeza kwa sheria hiyo kupokewa na kutumiwa katika soka ya England.
Takwimu zinaonesha kwamba kuna wachezaji palikuwa na makocha watano weusi kwenye soka ya kulipwa England, ambapo ukiacha wawili wanaoendelea na kazi zao, wengine walikuwa ni Chris Hughton, Paul Ince, Chris Kiwomya na Edgar Davids.
Comments
Loading…