in , , ,

Watumwa’ waandaa Kombe la Dunia Qatar

‘*Wapokonywa pasipoti, wanyimwa mishahara
*Watu 44 wadaiwa kufariki kwa mateso hayo
*Wananyimwa maji ya kunywa, Fifa yaonya

 
 
Waandaaji wa Kombe la Dunia 2022, Qatar wametupiwa shutuma nzito za kuwafanyika kazi watu mfano wa enzi za utumwa.

Hili ni kombora jingine linalozidi kuwaweka pabaya nchi hiyo ambayo ni ya kwanza kupewa uenyeji wa mashindano hayo miongoni mwa nchi za Mashariki ya Kati na za Kiislamu.

Waangalizi wamesema wameshitushwa na kusikitishwa sana na mazingira ya kazi, ambapo uchunguzi huru umeonesha kwamba wahamiaji wanafanyishwa kazi kitumwa.

Qatar ina wahamiaji wengi, ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wafanyakazi huko pia ni wahamiaji, taarifa zinasema kwamba raia wa Nepal wanahenyeshwa sana kwenye kile kilichoelezwa kuwa utumwa wa zama mpya.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limesema linasikitishwa na habari hizo ambapo Serikali ya Qatar imetangaza kuanza uchunguzi kwenye suala hilo na kulishughulikia.

“Hakuna sababu yoyote wala hatutakubali kuona wafanyakazi walio ndani ya Qatar wakifanyishwa kazi kama watumwa,” serikali imesema katika tamko lake.

Uchunguzi unaonesha kwamba walau watu 44 walipoteza maisha kati ya Juni 4 na Agosti 8 mwaka huu kutokana na ajali kwenye kazi za kuandaa miundombinu ya mashindano hayo na magonjwa ya moyo yanayohusiana nayo.

Inadaiwa kwamba baadhi ya wahamiaji wanalazimishwa kufanya kazi hizo ngumu za ujenzi kwa ajili ya Kombe la Dunia, ambapo wanaume wengi wa Nepal licha ya kufanya kazi hawajalipwa kwa miezi kadhaa, huku pasi zao za kusafiria zikitaifishwa ili kuwazuia kusafiri.

Inadaiwa pia kwamba wafanyakazi wanazuiwa kupata maji ya kutosha ya bure kwenye maeneo ya ujenzi, hivyo kuwaletea matatizo ya kiafya.

Bodi inayosimamia Kombe la Dunia imesema kwamba lazima Qatar wazingatie sheria na kanuni za afya na usalama kazini, utu wao kuzingatiwa na pia ustawi wao.

Wakuu wa Qatar wamesita kukanusha au kukubali juu ya hali hizo lakini wamesema watahakikisha wafanyakazi wote wanapata haki zao na utu kuzingatiwa.

Mambo mengi yameibuka dhidi ya mashindano hayo kufanyika Qatar, ambapo wadau wanasema haitawezekana kuchezwa majira ya joto, kwani jotoridi hufikia hadi nyuzijoto 56 au zaidi.

Fifa inafikiria kuhamishia mashindano hayo wakati wa majira ya baridi, lakini pia upo uwezekano wa wadau, ikiwa ni pamoja na wadhamini kushitaki.

Nchi zilizonyimwa uandaaji nazo zinapanga kushitaki iwapo ratiba itabadilishwa. Wazo jingine lililotolewa ni kubakisha mashindano wakati wa majira ya joto lakini yahamishiwe katika nchi nyingine itakayokuwa na jotoridi la kufaa.

Qatar inadai imeshabuni na inawekeza teknolojia ya kupoza hewa kwenye viwanja vyote wakati wa mashindano hayo, lakini tatizo ni kwamba teknolojia hiyo haijajaribiwa na kukubaliwa na mamlaka husika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

KAMATI YA MAADILI TFF YATANGAZA MAAMUZI YAKE

KOMBE LA LIGI ENGLAND, MZUNGUKO WA NNE….