Historia inatuambia kwenye miaka ya 1800 kabla ya mapinduzi ya viwanda
kila nchi ilikuwa masikini na watu wengi walikuwa masikini.
Hadithi ilibadilika baada ya mapinduzi ya viwanda kwenye karne ya 19
kuelekea karne 20. Hali iliyowapa nafasi ya watu mbalimbali kufanya
wawezalo kulingana na walichokuwa na uwezo nacho.
Wenye akili walikimbia, waliokuwa wamepungukiwa na akili kipindi kile
walibaki wamelala hata muda wa kukaa hawakuwa nao na hii ilitokana na
wale walioonekana wana akili mpaka wakapata nafasi ya kukimbia,
walikimbia na mali pamoja na akili za wale waliokuwa wamebaki
wamelala.
Akili za wao kukimbia tena hazikuwepo, kwao waliona kulala ni kitu
bora kuliko kukimbia kwa sababu kwenye kulala hakuna jasho lolote
ambalo walikuwa wanalipata ukilinganisha na kukimbia.
Hata kizazi chao walikipata wakiwa wamelala, na kujikuta wanatengeneza
kizazi kilicholala mpaka leo. Kizazi kinachopingana na maana halisi ya
kuwa jasho ndiyo mafuta pekee yanayotumika kwenye gari la maendeleo.
Ni ngumu kwa gari la maendeleo kwenda bila kuwekewa mafuta ambayo ni
jasho, wingi wa jasho kwenye gari lako ndiyo ukubwa wa thamani ya
maendeleo yako. Na ndiyo maana napenda kusema vipimo vyote vya
maendeleo ya mtu hupimwa kulingana na wingi wa jasho linalomtoka
mwilini mwake.
Ndiyo maana huwezi shangaa huku kwetu wachezaji wetu wanakufa masikini
kipindi ambacho jarida la forbes la nchini marekani likiwatangaza
wanamichezo wanaoingiza pesa nyingi duniani.
Hii haitoi maana ya kwamba wanamichezo wetu wanatakiwa wawepo kwenye
orodha ya hao wachezaji kumi wanaoingiza pesa nyingi, lakini kuna kitu
cha kujifunza kupitia vyanzo vyao vya mapato.
Kama huwezi kutengeneza kitu kizuri basi unatakiwa ukifanye kionekane
kizuri, ni ngumu kwa mchezaji wa Tanzania kushindana kipesa na
Cristiano Ronaldo ila ni vyepesi sana kwa mchezaji kuishi kwenye njia
za Cristiano Ronaldo.
Mchezaji kuelewa marupurupu, matangazo ya biashara na kuwa balozi wa
makampuni ya kibiashara ni njia sahihi ya kwake kupita kwenye njia za
Cristiano Ronaldo, kutegemea mshahara pekee ni kwenda kinyume na njia
za Cristiano Ronaldo.
Unaweza ukashindwa kufanya kitu kizuri maishani mwako, lakini unaweza
ukatengeneza kitu kikaonekana kizuri, ndiyo maana wakati mwingine
unaweza ukashindwa kuuza hisa za Klabu ili iendeshwe kibiashara kama
jambo zuri lakini ukatengeneza kitu ambacho kikaonekana kizuri mbele
ya macho ya jamii bila kuuza hisa za klabu.
Yanga ina wanachama milioni tano na kuendelea, huu ni mtaji mzuri sana
kwa viongozi wao kufanya kitu kionekane kizuri baada ya wao kushindwa
kufanya kitu kizuri.
Ukiachana na kwamba Yanga inaweza ikatumia wingi wa wanachama hawa
kuuza vifaa vyenye nembo ya klabu kama saa, viatu, jezi, kofia, skafu,
perfume na kadhalika ila pia wanachama hawa ni mtaji mkubwa sana kwao
kupata wadhamini watakao rahisisha shughuli zao ndani ya klabu.
Miaka ya 90 Pamba iifanikiwa kupata ndege kutokana na udhamini wa
mgodi wa mwadui, kwanini leo hii ambapo tuna utitiri wa mashirika ya
ndege ndani na nje ya nchi wakose ndege itakayokuwa inawadhamini
safari zao za nje na ndani?
Ni ngumu sana kuruka kama hujaamua kuagana na nyoga, inawezekana
kabisa bado hatujaamua kuruka na sababu kubwa ni kwamba hatujaagana na
nyoga.
Utaaganaje na nyoga wakati bado umelala? Wazee wetu walipokuwa
wamelalia ndipo tulipoamkia na hatutaki kuamka ndiyo maana hatutaki
hata kutazama uwakala kama ni biashara moja wapo kubwa. Tanzania ni
moja ya nchi ambayo haina mawakala wa soka wasiozidi kumi na mwisho wa
siku tutabaki kumtolea mfano Msuva kuwa hakuwahi kwenda kucheza soka
la kulipwa kwa sababu ya ujinga wake, wakati hata sisi ujinga wetu
ulichangia kumbakisha nchini.
Roho haituumi tunavyomuona Mendez anavyotengeneza pesa nyingi kupitia
simu na ndiyo maana hutoshangaa kuona tusivyo na wivu wa maendeleo na
majirani zetu wa Kenya wanavyojinyakulia medali za dhahabu katika
mashindano makubwa ya riadha duniani. Hatutaki kujifunza ni njia zipi
wanazotumia kuzalisha mashujaa wapya kila siku, vichwa vyetu
havikuniki kisawasawa namna ya kuwatengeneza wakina Nyambui wapya ,
wenzetu kwenye riadha wameshafika na wanaendelea kwenda pasipofikika
na wamehamia kwenye mchezo wa Raga.
Hatua ni hatua lakini cha muhimu ni kupiga hatua ya uhakika katika
maisha yako. Ni ngumu kwa hatua ya uhakika kupatikana gizani hata siku
moja. Mwanga hutoa mwelekeo wa uhakika wa hatua zako unazopiga . Ndiyo
maana mimi napata mashaka na hatua ya uandaaji wa kombe la Afrika kwa
vijana wa chini ya umri wa miaka 17 tuliopata mwaka 2019. Ni hatua
nzuri ila uhakika wa hatua hii ni kutufikisha wapi? Kuandaa na
kushinda michuano hii kisha tukawakilishe Afrika kwenye kombe la dunia
la vijana?
Mimi nahisi siyo jambo la busara kupendezesha nyumba kutokana na ugeni
wa ghafla, maana utatumia muda mwingi wa usafi wako sebuleni.
Michuano hii ya vijana tutakayoiandaa itatumia uwanja wa taifa na wa
Azam Complex pekee baada ya michuano hii tutabaki na makaratasi yetu
ofisini kuwa tuliwahi kuandaa michuano ya Afrika kwa vijana.
Serikali yetu haitotumia hii fursa kama fursa ya kuandaa michuano
mikubwa zaidi ya hii kwa kukarabati viwanja tulivyonavo. Tuna utajiri
wa viwanja vibovu, vinavyohitajika marekebisho pekee. Usishangae
kumuona raisi wa Zambia akitangaza nia ya kuandaa Afcon mwaka 2025
anajua faida ambazo nchi itapata kiuchumi, kiutalii na sekta
mbalimbali kukua kama sekta ya uwekezaji.
Mpira wa kikabu umetiwa kapuni, hauna sehemu ya kutokea ndiyo maana
vijana wengi wanaishia kuwa mashabiki wa kina Steve Cury, James lebron
na Kevin Durrant. Wamebaki wakishereheka na kushujudu ufalme wa hawa
watu baada ya nyie kuuweka mchezo wao kwenye kapu na kuamua kuutupa
mtoni, kuna siku mke wa Farao ataokota kapu la mtoto kikapu na atamlea
kisha atakuja kututoa utumwani.
Kuna kipindi ngumu ilionekana kama mchezo ambao utakuja kutupa sifa
kwa miaka ya mbeleni, lakini viongozi wake bado wamelala hawajui kipi
wafanye kuendeleza mchezo huu.
Hapo ndipo tofauti ya kwetu sisi na wao inapokuja, sisi kila siku
tunajifunza hesabu za kutoa kwenye kila kitu tulichonacho, wakati wao
hufanya hesabu za kujumlisha kwenye kila walichonacho. Ni ngumu
kukimbia pamoja kwenye mbio zinazokinzana hata siku moja.