in , ,

LUKAS PODOLSKI, UBAYA WA NAMBA HUHESABIKA KWENDA MBELE.

Ulikuwa usiku uliokuwa mkubwa sana kwa Podolski na wajerumani kwa
ujumla, usiku uliokuwa na hisia mbili , hisia ya furaha na hisia ya
majonzi.

Ilikuwa siku ya furaha kwa Wajerumani kumwangalia Lukas Podolski kwa
mara ya mwisho akitumikia timu yake ya taifa ya Ujerumani. Taifa
ambalo Lukas Podolski alilihusudu mpaka kufikia hatua ya kukataa
kuchezea taifa lake la asili yani Poland.

Wajerumani hawakuwa na choyo walimkaribisha Lukas Podolski na
kumnywesha damu ya kijerumani,damu ambayo ina maana kubwa sana. Wao
wanaamini ni watu pekee wenye akili duniani jeuri ambayo inawafanya
wawe na tabia ya kulipenda taifa lao,upendo unaopelekea wao kuwa
tayari kulipigania taifa lao katika hali yoyote.

Ni Ozil pekee ambaye alipata bahati mbaya ya kunywa damu chache sana
ya Kijerumani ndiyo maana ndani yake huwezi kuta ana asilimia kubwa ya
upiganaji na ukatili.

Haikuwa hivo kwa Lukas Podolski ,upiganaji na ukatili ulienea ipasavyo
kwenye mishipa yake ya damu. Akawa mtu asiyekuwa na huruma hata
chembe.

Katika ukuaji wake alionekana ni Daudi aliyetayari kwenda kwenye
uwanja wa vita bila kujali umri wake ulivyo mdogo. Mzaha haukuwa
umetengeza nyumba kwenye paji lake la uso kipindi alipokuwa vitani.

Hakuwa na nafasi ya kutafuta urafiki wakati wa vita, roho ya kikatili
ilikuwa imemvamia akawa anatembea nayo, anakula nayo na kuishi nayo
tangia akiwa kitoto kidogo cha FC Koln ndiye maana akiwa na umri wa
miaka 18 tu alifanikiwa kufunga magoli 10 katika michezo 19 katika
timu ya wakubwa ya FC Koln.

Wajerumani hawakutia mashaka juu ya ukatili uliokuwa ndani yake, wao
waliamini kwa muda aliofikia haikupaswa wao kumtilia mashaka na
wasiwasi, kilichokuwa kichwani kwao ni kumuona Adolf Hitler kwenye guu
la kushoto la Lukas Podolski.

Sumu ilikuwa inatembea kwa kasi mwilini mwake, ukatili uliongezeka
mwilini mwake akawa Simba asiye shiba vizuri, muda wote alitaka
kuonekana akiwinda kwa ajili ya tumbo lake. Akiwa na miaka 19 pekee
akafanikiwa kuwa mfungaji bora ya ligi ya Ujerumani kwa msimu wa mwaka
2004/2005 .

Chembechembe za damu ya ukatili zilikuwa zinaonekana kwake, kitu
ambacho kilikuwa kinazidi kuwapa furaha siku hadi siku Wajerumani.
Kwao ilikuwa ni furaha kuona jinsi mguu wa kushoto wa Lukas Podolski
ukitumika ipasavyo kuchinja watu bila huruma. Wingi wa damu na wingi
wa vichwa vilivyokuwa vimetenganishwa na vviwiliwili kwa kutumia kisu
cha mguu wa kushoto wa Lukas Podolski kwao ndiyo ilikuwa furaha.

Kushuhudia kifo cha adui ndiyo faraja ya Mjerumani, ndiyo maana hata
walipoandaa kombe la dunia la mwaka 2006 ilikuwa furaha kwao kumuona
muuaji wao mchanga akiwa anashindana kwenye mashindano ya uuaji na
wauaji wazoefu kama kina Ronaldo De Lima, Hernan Crespo, Zidane
,Miroslvan Klose na wengine wengi. Kwao kwa kipindi kile waliamini
wameshaanza kutengeneza jemedari mahili wa vita.

Jemedari ambaye angeweza kuibeba nchi yake na kwenda kuitetea mbele ya
adui yoyote.

Ni moto mmoja tu utakao waka milele, moto wa Jehanamu. Moto ambao huwa
tunausoma tu kwenye vitabu vya dini. Lakini moto wowote ule unaowashwa
na binadamu huzimwa na binadamu. Ndivyo ilivyokuwa kwa Lukas Podolski.

Moto wa Lukas Podolski ulianza kuzimwa taratibu, Mark Van Bommel
alikuwa mtu wa kwanza kuanza kutia maji kwenye moto wa Lukas Podolski.
Faulo yake ilimfanya Lukas Podolski akae nje ya uwanja akiuguza
majeruhi na hata aliporudi alikuta Luca Toni tayari ameshafukia ufalme
wake ndani ya kikosi cha Bayern Munich. Ikawa ngumu kuwatoa wabobezi
wa vita yani Miroslav Klose na Luca Toni.

Upande wa pili wa maisha akaanza kuuonja, majonzi yakavamia furaha
yake, ikawa ni wakati mgumu kuanza kuupitia katika maisha yake ya
soka. Nafsi yake iliamini Bayern Munich ndipo sehemu sahihi kwake yeye
kuweka ufalme wake lakini ikawa ngumu kwake kwa sababu siku zote ni
ngumu kukuta wafalme wawili ndani ya himaya moja.

Fc Koln ndiko alikokulia, siku zote mtoto hakuwi kwa wazazi na wala ni
ngumu kwa mtoto kufukuzwa nyumbani. Wajerumani wakampokea mpaka
ikafikia hatua kwenye website ya Klabu ya FC Koln kulitengenezwa picha
ya Lukas Podolski ambayo iliuzwa ili klabu ipate pesa za kuongezea
kumnunua kutoka Bayern Munich.

Imani ya Wajerumani kwa Podolski haikuwahi kutoweka hata siku, aliitwa
timu ya taifa hata kipindi ambacho alionekana hastahiri kuitwa.

Historia haitomkumbuka Lukas Podolski kama ambavyo itakavyomkumbuka
Gerd Muller ila atabaki kinywani mwa watu kama ni mmoja wa wachezaji
waliowahi kubeba kombe la dunia la mwaka 2014.

Kichwa huwa kinaniuma kila nikifikiria kwanini Lukas Podolski hakuwahi
kuwika na kikosi cha Arsenal, pengine kinachomkuta wajina wake Lucas
Perez ndicho kilichowahi kumkuta Lukas Podolski.

Goli lake alilofunga kwenye sekunde ya 9 dhidi ya Ecuador na kuwa goli
la mapema halitokuwa na kumbukumbu nzuri kama goli alilofunga usiku
huu. Goli ambalo hata Joe Hart alikuwa anatamani afungwe ili awemo
kwenye historia ya Lukas Podolski.

Tatizo la namba siku zote huhesabika kwa kwenda mbele ili kuzipa
nafasi namba zingine kuhesabiwa, ingekuwa inawezekana tungehesabu
namba kwa kurudi nyuma ili tumrudishe Lukaz Podolski.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KUNA HAJA RATIBA YA LIGI YETU IENDANE NA RATIBA YA CAF

Tanzania Sports

WAO NA SISI NI KAMA HESABU ZA KUJUMLISHA NA KUTOA