in , , ,

KUNA HAJA RATIBA YA LIGI YETU IENDANE NA RATIBA YA CAF

Msukuma hujivunia zaidi anapokuwa na idadi kubwa ya ng’ombe dume
katika zizi lake, yeye hupenda kuwaita “Nzangamba”. Ufahari wa kuwa na
idadi kubwa ya ng’ombe dume kwake huwa ni msingi kuliko kujua
upatikanaji wa hao ng’ombe dume.

Kwake yeye huona faida kubwa sana kwa ng’ombe dume zinapokwenda
shambani kulima, au kutumika katika usafirishaji wa mazao kutoka
shambani mpaka nyumbani.

Thamani ya ng’ombe dume huwa kubwa hata kwenye utoaji wa mahali pindi
mtoto wa kiume anapotaka kuvuta jiko lake.

Furaha hii ya msukuma dhidi ya ng’ombe dume huja bila wao kukumbuka ni
wapi ufahari wa ng’ombe dume huanza kujengwa.

Thamani ya ng’ombe jike hushushwa mbele ya ng’ombe dume bila kukumbuka
ng’ombe jike ndiye matunda ya ng’ombe dume bora, imara na yenye nguvu.

Ni ngumu sana kupata ng’ombe dume lenye sifa za kifahari bila ng’ombe
jike lenye matunzo mazuri.

Matunzo mazuri ya ng’ombe jike ndiyo matokeo ya kupata dume bora
.Maziwa hupatikana kwa ng’ombe dume, maziwa ambayo huwa na faida kubwa
kwenye ukuaji wa ndama. Pia ng’ombe jike ndiye huelekeza malisho
sahihi kwa ndama wake.

Kama ilivyo kwa ng’ombe jike kuhitaji matunzo mazuri kwa ajili ya
kukuza ng’ombe dume bora, imara na yenye nguvu ,ndivyo hivo hata ligi
yetu inahitaji matunzo mengi sana ili kupata timu imara za kushindana
kwenye michuano ya kimataifa.
Ligi yetu ni mama mzazi na mlezi wa vilabu vyote vya ligi kuu. Malezi
yake ndiyo yatakayoleta matokeo sahihi kwa vilabu vyetu.

Yani ni aina gani ya mtoto tutakaye mpata kwenye ligi zetu,tutampata
kulingana na matokeo ya malezi ya ligi yetu.

Ligi yetu ikitulea vibaya ndivyo hivo tutapata vilabu ambavyo havina
ushindani katika mechi za kimataifa.

Pamoja na ushindani hafifu uliopo ndani ya ligi yetu unaosababishwa na
sababu mbalimbali kama upungufu wa wadhamini pia ratiba ya ligi yetu
huchangia kwa kiasi kikubwa kwa timu zetu kutokufanya vizuri kwenye
mechi za kimataifa ikiwa ni sababu mojawapo kati ya nyingi zilizopo.

Ligi yetu huanza mwezi wa nane na kumalizika mwezi wa tano, wakati
michuano ya vilabu vya CAF huanza mwezi wa pili mpaka mwezi wa kumi na
moja.

Ukiangalia ratiba ya ligi yetu na ratiba ya mashindano ya vilabu
barani Afrika zinapishana, na hii inakuwa na hasara kubwa sana kwa
vilabu vyetu kuliko faida.

Kwanza kwa klabu ambayo hufanikiwa kuvuka na kwenda hatua ya makundi
ya michuano hii ya vilabu barani ulaya huwa havipati muda mwingi wa
kupumzika. Kama ligi yetu inamalizika mwezi wa tano na kuanza mwezi wa
nane au wa tisa kama msimu mpya, na mashindano ya vilabu barani Afrika
huanza mwezi wa pili mpaka wa kumi na moja, hii inatoa taswira halisi
kuwa timu haiwezi kupata muda mzuri wa kupumzika.

Mfano,msimu uliopita Yanga walifanikiwa kuingia hatua ya robo fainali
ya kombe là shirikisho barani Afrika.
Uwakilishi wao umeanza mwezi wa pili mwaka 2016 ligi imeisha mwezi wa
tano mwaka 2016. Ligi imeisha wao wakabaki kwenye michuano ya kombe la
shirikisho Afrika.

Msimu mpya wa ligi kuu wa 2016/2017 umeanza mwezi wa tisa kipindi
ambacho Yanga ilikuwa inamaliza michezo yake ya hatua ya makundi ya
kombe là shirikisho.

Hawakuwa na muda wa kupumzika wakaingia kwenye ligi, mpaka sasa wapo
kwenye ligi na wapo kwenye michuano ya kimataifa, na hii itakuwa na
maana kuwa kama wakifanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi ya kombe
là shirikisho hawatopata muda wa kupumzika.

Na hii italeta uchovu mkubwa sana kwa wachezaji. Hata ukiangalia
viwango vya baadhi ya wachezaji msimu huu wa klabu ya Yanga vimeshuka
kwa sababu ya uchovu.
Pia majeraha yamekuwa mengi kwa baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga
kama Ngoma, Kamusoko, Tambwe na wengine kwa sababu ya uchovu.
Hii ilipelekea kwa Yanga kutotoa upinzani dhabiti kwenye mechi dhidi
ya Zanako hasa hasa kwenye mechi ya nyumbani.

Pia tumekuwa tukililia kila siku timu zetu zijijenge kiuchumi kwa
kutafuta njia mbadala za mapato ndani ya timu.

Na moja ya njia nzuri ya kuingiza pesa kwa mpira wa kileo wa
kibiashara ni kucheza pre -season matches ( mechi za maandalizi ya
msimu mpya ).

Mechi hizi huambatana na timu kwenda sehemu mbalimbali kulipo na
mashabiki wao ili wacheze mechi na timu za mkoa husika ili wao
kunufaika na viingilio, kuuza bidhaa zenye nembo za vilabu kama jezi,
skafu na kofia.

Na ili ufanikiwe kwa hili unatakiwa uwe na mtaji wa mashabiki, na
vilabu vinavyofanikiwa kupata nafasi ya kuwakilisha nchi yetu ni vile
ambavyo vina mashabiki wengi. Hivo ratiba kwao huwabana sana na
kutowapa nafasi ya kupata muda wa kucheza mechi za maandalizi ya msimu
mpya kwa sababu muda huo wao huwa wanawakilisha nchi kwenye mechi za
kimataifa hivo hujikuta wanapoteza baadhi ya mapato.

Kuna haja kwa TFF kuangalia upya tena upangaji wa ratiba ya ligi kuu
ili iendane na ratiba ya CAF.

Tuige mfano wa timu za Ulaya, Msimu wa ligi zao nyingi huanza mwezi wa
nane na michuano ya ligi ya ulaya ( UEFA na EUROPA) huanza mwezi wa
tisa hatua ya mtoano, na kumalizika mwezi wa tano sambamba na ligi kuu
za nchi mbalimbali.

Hii huvipa nafasi vilabu kupumzika vizuri na kupata pèsa za ziada
kupitia mechi za maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Kama tunataka tuwe na idadi kubwa ya ng’ombe dume ambao watatufanya
tujivunie tunatakiwa tumtunze vizuri mama yake na kumboresha ( ligi
kuu) kisha tuwape muda wa kupumzika ng’ombe dume ( vilabu
vinavyowakilisha nchi) .

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Hans Van Der Pluijm-Tumechoka na muziki wa Msondo na Sikinde

Tanzania Sports

LUKAS PODOLSKI, UBAYA WA NAMBA HUHESABIKA KWENDA MBELE.