*Pepe Reina aenda Napoli, Jovetic Man City
*Benteke abaki Villa, Terry akosa uhakika

Klabu ya Barcelona inaingia katika kipindi cha mpito, baada ya kocha wake, Tito Vilanova kujiuzulu kwa ajili ya kuendelea na matibabu yake ya saratani.
Vilanova (44) alikuwa na uvimbe katika koo lake na liliondolewa Noveba 2011, lakini mwaka jana alipata matatizo zaidi yanayohusiana na ugonjwa huo.
Vilanova alikuwa msaidizi wa Joseph ‘Pep’ Guardiola ambaye zaidi ya mwaka mmoja uliopita aliachia ngazi akisema anahitaji kupumzika na kuona akili yake upya, ambapo sasa amejiunga na mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich.
Kocha huyo alianzia kwenye timu ya vijana ya Barca 1988, kabla ya kujiunga na Celta Vigo na baadaye na klabu nyingine.
Amepata kuwa mkurugenzi wa ufundi kwenye klabu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Terrassa, na baadaye kuwa kocha msaidizi wa timu ya pili ya Barca, akifanya kazi chini ya Guardiola, kabla ya 2008 kuwa msaidizi wa kocha huyo.
Vilanova alikaa New York, Marekani kwa wiki 10 kwa ajili ya matibabu yake hayo na alirejea Hispania Machi, ambapo aliiongoza klabu yake kutwaa ubingwa wa nchi hiyo.
Rais wa Barca, Sandro Rosell na mkurugenzi wa soka, Andoni Zubizarreta ndio waliotangaza habari hizo mbele ya waandishi wa habari, wakisema Vilanova anaendelea na matibabu, hivyo hataweza kuendelea na majukumu hayo, wakisema ni pigo kubwa kwa klabu.
Klabu hiyo imekuwa na Jordi Roura kama kaimu kocha wakati Vilanova akiwa kwenye matibabu na mapumziko.

MANCHESTER CITY WAMCHUKUA JOVETIC

Baada ya danadala za hapa na pale, akiwaniwa na klabu mbalimbali, hatimaye Stevan Jovetic ametua Manchester City kwa kitita cha pauni milioni 22 kutoka Fiorentina.
Jovetic (23) alikuwa akiwindwa na Manchester United na Arsenal, lakini sasa amemalizia safari yake City baada ya kumaliza vipimo vya afya na kusaini mkataba.
Bosi mpya wa City, Manuel Pellegrini ameshafanikisha usajili wa Alvaro Negredo na winga Jesus Navas kutoka Sevilla na kiungo Mbrazili, Fernandinho.

PEPE REINA ANAKWENDA NAPOLI

Golikipa wa Liverpool, Pepe Reina (30) amejiunga na Napoli kwa mkopo wa msimu mmoja.
Anajiunga huko baada ya klabu hiyo kubwa kumsajili Simon Mignolet aliyekuwa Sunderland, atakayekuwa kipa namba moja na anayechukuliwa kuwa kipa aliyecheza zaidi na kuokoa mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita.
Reina anaungana na kocha wake wa zamani, Rafa Benitez aliyemaliza kibarua cha muda mfupi Chelsea. Benitez alikuwa akiwania kumsajili golikipa wa QPR, Julio Cesar anayewaniwa na Arsenal. Reina alikuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa zaidi Liverpool na ni mmoja wa wachezaji waliomwezesha Benitez kuwa na mafanikio Anfield.

BENTEKE ANABAKI MTOTO WA VILLA

Hatimaye mpachika mabao wa Aston Villa, Christian Benteke amekacha mpango wake wa kuihama klabu hiyo na kutia saini mkataba mpya utakaomfunga Villa Park hadi 2017.
Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji aliyeingia Villa kutoka Genk ya huko kwa pauni milioni saba mwaka jana, alikuwa anahusishwa na Tottenham na Chelsea pia.
Benteke alipata kusema awali kwamba angebaki Villa kwa ajili ya kumuenzi Kocha Paul Lambert aliyemwamini na kumpa kazi hapo, lakini baadaye akabadilika, akisema anataka kuondoka, licha ya kuwa mkataba wake haujaisha.

JOHN TERRY HAIHAI

Kocha mpya wa Chelsea, Jose Mourinho amesema kwamba nahodha wake, John Terry hayuko salama katika suala la kupata namba, hivyo atatakiwa ajitahidi kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.
Terry (32) alikuwa nahodha kwenye kikosi cha Mourinho katika ajira yake ya kwanza Chelsea, na amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, hivyo akishindwa kuonesha uwezo anaweza kupoteza nafasi kwenye timu hiyo na kutoongezewa mkataba.
“Hayupo salama, na anajua hana uhakika wa namba au hata kuongezewa mkataba. Kitu pekee kikubwa kati yetu ni urafiki tulio nao, lakini kikazi hakuna uhakika wowote…najua ni mchezaji mzuri lakini anatakiwa apambane kama wengine,” akasema Mourinho.
Chelsea sasa inaundwa na nyota wengi, ambapo hata msimu uliopita chini ya Benitez, nahodha huyo alikuwa akipangwa kwenye mechi chache, tena zisizokuwa za muhimu, kiasi cha kuzusha uvumi kwamba waligombana naye.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

CAF yateua waamuzi wa Taifa Stars dhidi ya The Cranes

Barcelona watamchukua nani