Wakati mshambuliaji wa Azam, Prince Dube alipopiga mkwaju mkali kuelekea langoni mwa Yanga na kuandika bao la kuongoza, maswali mawili yalinikabili; mosi, kwanini eneo la kiungo cha Yanga lilikuwa wazi na kumruhusu nyota huyo kujinafasi hatua tatu na nusu kwenye mchezo kama ule?
Pili, ukabaji wa beki wa Kati Abdallah Ninja ni mzuri sana, lakini nani anachukua au kumsaidia jukumu lake la kumfuata mpinzani kabla hajaleta madhara? Majibu yote haya yalikuwa na maana eneo la kiungo la Yanga liliwajibika kuhakikisha linadhibiti mpira. Lakini zaidi kabla ya mpira kumfikia Dube ulitokea pembeni kushoto ambako kulikuwa na Ditram Nchimbi na Kibwana Shomari, na pia eneo hilo hilo lilipaswa kuzibwa na viungo wao, nini kilichotokea?
Tanzaniasports inachambua mchezo huo kwa kina. Kwanza katika eneo la kiungo mpambano ulikuwa mkubwa kati ya Mudathir Yahya na viungo wa Yanga. Mudathir ndiye alikuwa kikwazo kikubwa cha safu ya kiungo ya Yanga.
Kiungo huyo si alikaba eneo kwa ufasaha bali ari na kasi viliifanya Yanga ijaribu mara nyingi kutumia pembeni mwao kupitia Deus Kaseke na Yacouba Sogne. Mudathir Yahna alikuwa anasaidiwa na Aaron Lyanga ambaye alikuwa akiingia eneo la katikati na kuelekea pembeni kushoto.
Uzuri wa Lyanga ana uwezo wa kukaa na mpira na ukokotaji wake ni hatari safu ya ulinzi. Mudathir hakuwa anapiga pasi kupitia kiungo bali alipiga ndefu kwenda upande wa kulia kwa asilimia takribani 80 ya mchezo mzima. Upande wa kulia alikopeleka pasi ndiko alikukowepo Lyanga. Mipango ya Azam ilipikwa kwa hawa wawili pamoja na Iddi Nado na Aggrey Moris. Tazama pasi nyingi alizopiga Aggrey Morris takrabani asilimia 70 zielekea upande wa Lyanga.
Pili, Yanga wamecheza na Azam wakiwa hawana mipango kitimu. Namna Yanga wanavyocheza, wanatoa pasi, wanavyoelekea lango, wanatengeneza mashambulizi yao utaona kabisa hakuna mpango madhubuti ambayo unaeleweka. Hakuna mkakati wa kitimu ambao unaona labda mchezaji fulani amewekwa mahususi kuwavuruga au kuwa mpishi wa ushindi wa Yanga. Hilo halipo, na kocha Mohammedd Nabi anatakiwa kufanya kazi upungufu huu.
Unaweza kushangaa Yanga uwezo wao wa kupiga pasi tano mfululizo ulikuwa hafifu. Amsha amsha bila utulivu, mipango na mikakati ya ushindi haiwezi kusiadia Yanga, kwa sababu mchezo mzima wameonesha kiwango hafifu cha kuwa na mfumo sahihi wa kutumia kupata matokeo mazuri.
Kwa ukubwa wa mechi ya Yanga na Azam mwalimu hakupaswa kutegemea kiungo mkabaji mmoja Tonombe Mukoko, ilibidi alinde kwanza timu kisha mpango wa pili ni kusaka ushindi.
Huwezi kuachia mapengo au mianya inayowapa adui nafasi ya kukushambulia kisha ukaendelea hivyo hadi dakika za lala salama ndipo unamsogea Feisal Salum ili awarudishe nyumba Azam kwa kuwashambulia zaidi, wakati wao walikuwa wanavusha mipira katikati kwenda mbele yaani ilipigwa juu juu kuwafuata walengwa. Pamoja na nia ya kuwarudisha Azam nyuma ya eneo lao, hakukuwa na mkakati mwingine kipindi cha pili kumdhibiti Mudahir Yahya, na Yanga walikufaa miguuni mwake.
Tatu, Michael Sarpong halishwi ipasavyo, akiwa mshambuliaji mwenye jukumu la kupachika mabao amekosa huduma ya kulishwa mipira ya kupachika magoli. Pasi nyingi anazopata Sarpong ni zile za juu za kugombania na mabeki wa timu pinzani, si Azam pekee bali mechi nyingi imekuwa namna hiyo. Ni Calinhos alijaribu kupiga pasi mpenyezo lakini hazikufika hata asilimia 40. Sarpong amekuwa ni mshambuliaji ambaye hapati huduma sahihi na hajiweki katika nafasi ya kupata huduma kwa sababu wakati wote amekuwa akiondoka katika nafasi yake.
Upande mbaya wa Sarpong unaochangia kushindwa kupachika mabao ni namna anavyojiweka au kujipanga katika eneo la hatari kila siku katika mechii nalo ni tatizo.
Nne, Yanga wana ari lakini hawana mipango ya kupika mabao. Deus Kaseke haeleweki, sijui anacheza namna gani, mbinu gani, anachangia nini kikosini kwa sababu hata kukokota mipira hakuna ni tatizo, hakupiga krosi, hakupiga pasi za mwisho na zaidi hakuwa tishio mbele ya beki mkongwe Morris na Bruce Kangwa.
Tano, kwa mchezo wao dhidi ya Azam unaona kama vile Yanga wameishiwa makali ya mawinga. Nafasi ya mawinga ni changamoto, hakuna winga tereza mwenye kasi, ari,maarifa na viwango. Kwa asili Yanga ni mabingwa wa kuzalisha mawinga wakali na wenye maarifa ya hali ya juu akina Akida Makunda, Said Maulid,Edibily Lunyamila,Mrisho Ngassa, Simon Msuva na wengineo, lakini sijui ni nani atamudu kuwapa huduma kwa wachezaji waliopo.
Sita, Yacouba Sogne pekee ndiye anamudu kukaa na mpira muda mrefu katika safu ya ushambuliaji na uwezo wa kukokota unamfanya kuwa mshambuliaji wa pili zaidi yaani nambari 10 au yule wa kucheza huru kuliko mshambuliaji kamili wa kuongoza jahazi la safu ya ushambuliaji. Kwa Michael Sarpong hamudu kazi ya Yacoube ni changamoto, hapigi mashuti bali purukushani ambazo mabeki wenye akili kam Aggrey Moris ni rahisi kudhibiti ushambuliaji wa aina hiyo.
Saba, Yanga dhidi ya Azam kiungo kiliyumba, mabeki wa pembeni Kibwana Shomari na Adeyum Saleh waliyumba. Eneo pekee ambalo Yanga naona pana uhakika na umadhubuti ni mabeki wa kati; Abdalla Ninja, Dickson Job, Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto. Angalau eneo hilo mabeki wanafanya kazi nzuri, lakini kama timu haifungi mabao maana yake wanajiweka katika shinikizo la wapinzani wao
Nane, mwishowe Tanzaniasports ilimtafuta kocha mmoja mkongwe ambaye amefundisha soka Tanzania Bara na Zanzibar katika vilabu vya Ligi Kuu amesema, “Niliwahi kukueleza hili jambo, na jana limejirudia tena dhidi ya Azam. Yanga si kwamba wana wachezaji wabaya lakini wanakosa benchi la ufundi lenye kiwango cha kutengeneza mikakati na mbinu za ushindi. Wao ndio wanachagua wachezaji wa kutekeleza mikakati yao, sasa mchezaji akifeli maana yake ule mkakati haumfai aondoshe mara moja, kinyume cha hapo tatizo litakuwa lilelile na makocha watafukuzwa tu, kwa sababu hawaangaliwi kama wana viwango vya kutosha kiufundi kabla ya kuajiriwa kufundisha Yanga,”
Comments
Loading…