in

Simon Msuva ‘atishia’ ndoto za ubingwa wa Simba CAF

Simon Msuva

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika limetoa  ratiba ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa wikiendi iliyopita inaonesha kuwa mechi za kwanza za robo fainali zitachezwa Mei 14 na marudiano yatakuwa Mei  21, ambapo Simba ni miongoni mwa timu 8 zilizotinga hatua ya robo fainali ikiwa imepangwa kuanza mchezo wake ugenini.

Ratiba ya mechi za kwanza za CAF zinaonesha kuwa Simba itamenyana na miamba ya Kaizer Chiefs ya Afrika kusini wakati Al Ahly watawakaribisha Mamelodi Sundowns  nchini Misri kabla ya wiki moja baadaye kwenda Johannesburg kurudiana na miamba hiyo ya zamani ya kocha wa Al Ahly Pitso Mosimane.

Nyota wa Tanzania Simon Msuva atakiongoza kikosi cha Waydad Casablanca ya Morocco kumenyana na miamba ya Algeria ya MC Alger, wakati CD Belouzidad wenyewe watakuwa wenyeji wa kigogo wa Tunisia, Esperance.

Katika hatua ya nusu fainali mshindi kati ya Simba na Kaizer Chiefs atakumbana na kati ya MC Alger na Waydad Casablanca. Hiyo ina maana kuwa endapo Simba watawatoa Kaizer Chiefs kisha Wydad Casablanca wakaitoa MC Alger itakuwa wazi kuwa nyota wa Tanzania Simon Msuva atakumbana na miamba ya nyumbani Tanzania yaani Simba.

Ikumbukwe Simon Msuva alikuwa nyota wa klabu ya Yanga kabla ya kujiunga na Difaa El Jadida ya Morocco na baadaye akasajiliwa na miamba hiyo ya Wydad Casablanca ambayo ina uwezekano kukutana na Simba kama timu hizo zitashinda mechi zao za robo fainali.

Vilevile mshindi kati ya Al Ahly na Mamdelodi Sundowns atachuana na mshindi kati ya Esperance ya Tunisia na CD Belouzidad ya Algeria.

Mechi kati ya Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundwons inatarajiwa kuwa ya kusisimua kutokana na ubabe wa timu hizo mbili, huku Mamelodi wakiwa wanajivunia kuizaba mabao 5-1 miamba hiyo ya Misiri.

Vuilevile mchezo kati ya Mamelodi Sundowns na A Ahly utakutanisha timu zinazofahamiana vema ambapo Pitso Mosimame anayeinoa Al Ahly kwa sasa atafanya kila mbinu kuwaonesha mabosi wake wa zamani kuwa yeye ni kocha bora kuliko walipo sasa.

Hata hivyo kibarua kigumu kilichopo ni kile Al Ahly kudhihirisha ubora wao mbele ya kikosi bora cha Mamelodi Sundwons kinachocheza soka la Kibrazil ndio maana ikuwa klabu maarufu barani Afrika ambayo ina jina la utani la Brazilians kutokana na aina ya kandanda lao, pasi nyingi na kutawala mchezo.

Kwa upande mwingine mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wanatangaza uhondo uliopo Ligi Kuu nchini kutokana na mkafanikio waliyopata hadi sasa.

Simba walikuwa kundi A pamoja na mabingwa watetezi Al Ahly(Misri), El Merreikh (Sudan), AS Vita (DR Congo) ambako waliibuka kuwa vinara kwa kujikusanyia pointi 13.

Jambo bora zaidi CAF wameitaja Simba kuwa timu kabambe na yenye mafanikio ikiwa inashika nafasi ya 13 msimu huu. Hayo ni mafanikio makubwa sana.

Simba ilianza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya AS Vota ambako ilishinda 1-0, kabla ya kulazimisha sare 0-0 dhidi ya El Merreikh ynchini Sudan. Katika mecho wa marudiano Simba waliwachapa El Merreikh mabao 3-0.

Aidha, Simba waliwachapa mabingwa watetezi Al Ahly bao1-0, kisha kuisambaratisha AS Vita mabao 4-1, na baadaye kukubali kipigo cha bao 1-0 nchini Misri.

NINI MAANA YA MAFANIKIO YA SIMBA?

SIMBA SC
SIMBA SC

Katika kandanda Afrika mashariki kwa nyakati tofauti timu zimekuwa zikibuka na kupotea. Simba imekuwa na rekodi nzuri ya mashindano ya kimataifa, lakini msimu huu wanaonekana kujivunia uzoefu waliopata kwenye mashindano hayo.

Mwaka 1998 Yanga wakiwa na kocha Tito Mwaluvanda na Raul Shungu walifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Simba wanaweza kuweka rekodi ya kuwa timu pekee ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kuweza kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tangu mfumo wa mashindano hayo ulipobadilika mwaka 2017 ambapo kuliwekwa hatua moja ya mtoano badala ya ile ya makundi kumalizika ikawa ya robo fainali, ikifuatiwa na nusu fainali na kisha fainali.

Hadi sasa mafanikio ya Simba ni jambo la kujivunia kwa Watanzania na Afrika Mashariki. Ikumbukwe Simba ndiyo klabu ya kwanza Tanzania kutoa mchezaji ambaye alikuwa miongoni mwa wafungaji bora wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2019. Emmanuel Okwi alikuwa alikuwa mchezaji aliyewakilisha Simba wakati huo na Ligi Kuu Tanzania bara.

Hatua ya mchezaji kutoka Afrika mashariki kuwa miongoni mwa wafungaji bora ulikuwa ujumbe juu ya kuinuka kwa soka Afrika mashariki.

Ukanda wa Afrika Mashariki haujawahi kuwa na rekodi kubwa za kandanda kama kanda za Afrika magharibi,kusini na kaskazini. Lakini sasa Simba wamebeba matumaini makubwa ya washabiki wa ukanda huo.

Klabu nyingi za Afrika mashariki hazina nguvu kama zile za Al Ahly, Esperance, CR Belouzdad, Wydad Casablanca, Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns, Raja Casablanca, Zamaleki,Ismailia,Orlando Pirates, Club Africain na nyinginezo.

Gor Mahia wamewahi kutinga hatua ya robo fainali katika Kombe la Shirikisho mara mbili 2017/2028 na 2018/2019). Yanga  walitinga hatua ya robo fainali mara moja sawa na Rayon Sports ya Rwanda (2018) lakini pia KCCA ya Uganda imefanya hivyo mara moja (2018)

PESA ZA LIGI YA TANZANIA

TFF HQ
TFF HQ

Wachezaji wa kigeni wamezidi kumiminika katika Ligi Kuu Tanzania.  katika kikosi cha Simba kilichoanza dhidi ya El Merreikh kilikuwa na wageni Francis Kahata (Kenya), Joash Onyango (Kenya) Taddeo Lwanga (Uganda), Chris Mugalu (DR Congo), Clatous Chama (Zambia), Larry Bwalya (Zambia), Luis Miquissone (Msumbiji) Lokosa (Nigeria) na Pascal Wawa (Ivory Coast) ni miongoni mwa nyota wanaowika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wachezaji wengine wa kigeni waliko katika klabu ya Yanga ni Carlos Calinhos (Angola), Michael Sarpong(Ghana), Lamine Moro (Ivory Coast), Farouk Shikalo (Kenya), Yacouba (Togo).

Mwingine ni mshambuliaji nyota wa Namungo FC Stephen Sey raia wa Ghana ambaye amekuwa maarufu Ligi Kuu Tanzania Bara na kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika ambako mabao yake yameiwezesha Namungo kutinga hatua ya makundi.

Nyota hao watachagiza ongezeko la idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali ambao bila shaka watakuwa chachu ya kuimarisha viwango vya wachezaji wazawa.

Kimsingi mafanikio hayo yatavutia nyota wa kigeni kucheza Ligi Kuu Tanzania, watavutia idadi kubwa ya wadhamini ambao watawekeza fedha zitakazosaidia klabu kujiendesha na kuboresha viwango vya wachezaji.

Mashindano ya CAF yanasaidia kuwaweka sokoni wachezaji wa klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara pamoja na kufuatiliwa vipaji vilivyoko nchini na kununuliwa moja kwa moja.

Jambo hilo linaweza kuwa na faida kubwa kwao kuimarisha vipato vyao lakini pia kuongeza pato la nchi na hata klabu ambazo zinaweza kuongeza makusanyo yao kutokana na mauzo ya wachezaji husika kwenda katika klabu nyingine za nje ama ndani ya bara la Afrika.

Kwa sasa Ligi Kuu Tanzania ndio inaongoza kwa klabu kulipa mishahara mikubwa kwa wachezaji Afrika mashariki jambo ambalo limekuwa likivutia nyota wengi kukimbilia klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi hii.

Ushiriki wa Simba maana yake unatangaza mazuri ya Ligi ya Tanzania. vilevile wachezaji wake wengi ambao wanaitwa timu za taifa hivyo itawavutia makocha wengi kutaka kujua maendeleo ya wachezaji wao.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Utamu mwingi wa Yanga unakosa makocha

Tanzania Sports

Man U wameonesha udhaifu