in , , ,

UMEKUWA MSIMU WA MAFANIKIO MAKUBWA KWA SIMBA

Mabao ya Awadh Issa na Juma Abdul yaliwapa ushindi Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa VPL dhidi ya Azam uliopigwa Mei 2012. Bao la kufutia machozi la Azam liliwekwa wavuni na John Bocco na kuufanya mchezo huo uliokuwa ukitazamwa kwa ukaribu kumalizika kwa matokeo ya 2-1.

Mtibwa walikuwa wakishangiliwa kwa shangwe isivyo kawaida na mashabiki waliokuwemo ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam. Zilikuwa kelele za mashabiki wa Simba. Si Mtibwa Sugar, ni klabu yao ya Msimbazi waliokuwa washindi halisi wa mchezo huo.

Ushindi huo wa Mtibwa uliwahakikishia Simba taji la VPL kwenye msimu huo wa 2011/12. Uliwabakisha Azam Fc na alama 53 wakiwa kwenye nafasi ya pili wakati Simba walikuwa wameshavuna alama 59 na hivyo kuwafanya mabingwa kwa kuwa kila timu ilibakisha mchezo mmoja. Simba hawakuwa na cha kupoteza tena kwenye mchezo waliokuwa wamebakisha dhidi ya mahasimu wao Yanga.

Huo ulikuwa ubingwa wa mwisho wa VPL kwa Simba. Uliwapeleka vijana hao walionolewa na Mwalimu Milovan Cirkovic kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambapo walikutana na Recreativo do Libolo ya Angola kwenye mzunguko wa awali. Walipoteza nyumbani kwa 1-0 na kisha ugenini kwa 4-0 na hivyo kuondolewa mapema kwa jumla ya mabao 5-0.

Pengine kipigo hicho hakikuwa maumivu kuyazidi maumivu yaliyofuata. Kilichofuata ni mfululizo wa misimu mibaya mno kwa Simba. Msimu uliofuata wa 2012/13 waliukosa ubingwa wa VPL uliokwenda kwa watani wao Yanga. Tofauti kati yao na Yanga ilikuwa alama 15. Mbaya zaidi hawakuwemo hata kwenye nafasi ya pili iliyokwenda kwa Azam FC na hivyo wakakosa nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika.

Msimu wa 2013/14 ulikuja kuwa wa maumivu zaidi kwa Wekundu hao. Walimaliza kwenye nafasi ya nne nyuma ya Azam, Yanga na Mbeya City waliokamata nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu. Tofauti ya alama kati yao na mahasimu wao Yanga ikapanuka na kufikia 18. Kwa mara nyingine hawakupata nafasi ya kushiriki michuano ya CAF kwa kukosekana kwenye nafasi mbili za juu.

Tofauti ya alama kati yao na watani wao Yanga ikapungua kwenye msimu uliofuata wa 2014/15. Safari hii ni alama 8 pekee zilizowatenganisha na Yanga waliotwaa ubingwa. Hata hivyo haya hayakuwa mafanikio. Bado hawakupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa. Yanga na Azam waliendeleza ufalme wao kwenye nafasi mbili za juu.

Msimu wa 2015/16 uliishuhudia tofauti ya alama 11 kati ya watani hao wa jadi. Simba walibakia kwenye nafasi ya tatu huku Yanga wakishinda taji hilo la VPL na nafasi ya pili ikabakia kwa Azam. Safari hii mshindi wa pili hakuwa na nafasi ya kushiriki michuano ya CAF kutokana na mabadiliko ya kanuni kufuatia kuanzishwa kwa Kombe la Shirikisho la Azam.

Kwenye Kombe la Shirikisho la msimu huo Simba hawakuweza kutwaa ubingwa. Waliondolewa na Coastal Union kwenye hatua ya robo fainali kwa 2-1. Ni Yanga waliokuja kutwaa taji hilo kwa kuwafunga Azam 3-1 kwenye mchezo wa fainali. Nafasi ya kushiriki michuano ya CAF ikabaki kwa Yanga na Azam kwa msimu wa nne mfululizo.

Kwenye msimu wa 2016/17 uliomalizika siku kadhaa zilizopita Simba wamefanikiwa kufuta kabisa tofauti ya alama kati yao na Yanga. Wamemaliza na alama 68 sawa na mahasimu wao waliotwaa ubingwa kutokana na kuwa na tofauti kubwa ya mabao. Kutoka tofauti ya alama 18 msimu wa 2013/14 mbaka tofauti ya alama 0, tusiyaite haya mafanikio?

La maana zaidi ni kurejea kwenye michuano ya CAF ya mwakani baada ya kutwaa Kombe la Shirikisho Jumamosi kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbao. Lile jina la ‘Wa Kimataifa’ na wao linawafaa sasa sambamba na Yanga wanaojipamba kwa jina hilo. Licha ya kukosa ubingwa wa VPL kwa msimu wa tano mfululizo, msimu huu umekuwa wa mafanikio makubwa mno kwa Simba.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MAENEO YATAKAYOAMUA MECHI YA FAINALI YA FA KATI YA CHELSEA NA ARSENAL.

Tanzania Sports

PESA HAIKUWA CHOCHOTE KWENYE MSIMU WA EPL ULIOMALIZIKA