in , , ,

PESA HAIKUWA CHOCHOTE KWENYE MSIMU WA EPL ULIOMALIZIKA

Zaidi ya paundi bilioni 1.19 zilitumika na klabu za EPL kwa ajili ya usajili kwenye kipindi cha dirisha kubwa la usajili la msimu uliopita lililoishia Septemba 1 2016. Kwa fedha ya Tanzania kiasi kilichotumika kilikuwa zaidi ya shilingi trilioni 3.4. Hiyo ilkikuwa mara ya kwanza jumla ya fedha za usajili kwa klabu zote za EPL kuvuka paundi bilioni 1 ndani ya dirisha 1 la usajili.

Manchester City na jirani zao Manchester United ndio walikokuwa vinara kwenye matumizi ya pesa za usajili kwa ajili ya kujiandaa na msimu wa EPL na mashindano mengine. Manchester City walitumia jumla ya paundi milioni 174 wakati Manchester United waliteketeza kiasi cha takribani paundi milioni 150 huku wakivunja rekodi ya ada ya uhamisho kwa kutumia paundi milioni 89 kwa ajili ya Pogba.

Mabingwa Chelsea hawakufua dafu kwenye matumizi ya pesa kuzizidi klabu hizo mbili kutoka jiji la Manchester. Wao walikuwa kwenye nafasi ya tatu baada ya kutumia paundi milioni 123.4 zilizowashusha Darajani N’Golo Kante, David Luiz, Michy Batshuayi na wengine. Walikuwa nyuma kwenye matumizi lakini wakawa vinara kwenye EPL.

Tottenham Hotspur wao walitumia kiasi cha paundi milioni 70.6 pekee kuwasajili Mkenya Victor Wanyama na wengine. Manchester City na Manchester United kila moja ilitumia zaidi ya mara mbili ya kiasi hiki. Vijana hao wa Mauricio Pochettino walimaliza kwenye nafasi ya pili kwenye EPL wakiwa mbele kwa nafasi moja dhidi ya Manchester City na kwa nafasi tatu dhidi ya Manchester United.

Liverpool wao chini ya Meneja Jurgen Klopp walitumia kiasi cha paundi milioni 69.9. Sadio Mane, Georginio Wijnaldum na Joel Matip ni baadhi ya wachezaji waliosajiliwa. Klabu hiyo kutoka Merseyside ilimaliza kwenye nafasi ya nne na kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Arsenal walitumia zaidi ya paundi milioni 90 lakini hawakuweza kukata tiketi hiyo yenye hadhi.

Kiasi cha paundi milioni 22.5 ndicho pekee kilichotumika na West Bromwich Albion. Walimaliza kwenye nafasi ya 1o. Walikuwa mbele kwa nafasi mbili dhidi ya Leicester City waliotumia zaidi ya mara tatu ya kiasi hicho. Watford na Crystal Palace kila moja ilitumia zaidi ya paundi milioni 50 lakini ziliachwa mbali na West Brom kwenye msimamo wa EPL. Hata Sunderland walioshuka daraja walitumia pesa nyingi zaidi ya West Brom.

Kwenye mafanikio binafsi pia kwenye msimu uliomalizika tunapata picha ile ile. Kati ya wachezaji wote waliosajiliwa kwenye majira ya joto mwaka jana ni N’Golo Kante, David Luiz na Sadio Mane walioingia kwenye timu bora ya mwaka ya EPL inayofahamika kama ‘Premier League PFA Team of The Year’. Jumla ya kiasi kilichotumika kuwasajili wachezaji hao watatu wa Chelsea na Liverpool ni karibu sawa na paundi milioni 89 zilizotumika na Manchester United kumsajili Paul Pogba ambaye hakuonesha makali yaliyotarajiwa.

N’Golo Kante aliyesajiliwa na Chelsea kwa paundi miloni 30 alifanya vizuri mno na kuibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa EPL inayotambulika kwa jina la ‘PFA Player of The Year Award’. Amewaacha mbali mno Paul Pogba, John Stones, Leroy Sane na Michy Batshuayi ambao kila mmoja alisajiliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa kumzidi yeye.

Fernando Llorente aliyesajiliwa na Swansea kwa ada ya uhamisho inayoaminiwa kuwa takribani paundi milioni 5 pekee amemaliza msimu akiwa na mabao 15. Batshuayi alisajiliwa na Chelsea kwa zaidi ya mara sita ya kiasi hicho. Haya yote yanaashiria kuwa pesa haikuwa chochote kwenye msimu wa EPL uliomalizika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

UMEKUWA MSIMU WA MAFANIKIO MAKUBWA KWA SIMBA

Tanzania Sports

AZAM WAMEMCHOMA KISU JICHONI BOCCO, HUKU WAKIWA WAMEMTUMBULIA JICHO.