in , , ,

Ulivyo uwezekano wa Leicester ama Tottenham kutwaa taji la EPL

Zimesalia raundi 9 pekee kuelekea mwishoni wa msimu huu wa EPL. Ukiwatoa Manchester City, Liverpool, Everton na Newcastle United waliocheza michezo 28, timu nyingine zote zimeshacheza michezo 29 kila moja.

Leicester City chini ya Claudio Ranieri ndio wanaoongoza kwenye msimamo wa EPL wakiwa na alama 60. Tottenham Hotspur wanashikilia nafasi ya pili na alama zao 55.

Washika Bunduki wa London wanazo alama 52 zinazowaweka kwenye nafasi ya tatu huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Manchester City wenye alama 50 na mchezo mmoja mkononi.

Kwenye makala hii tunatazama uwezekano wa kutwaa taji la EPL kwa timu mbili za juu kwenye msimamo wa EPL ambazo ni Leicester City na Tottenham Hotspur.

Vinara Leicester City mbaka sasa tayari wameshamshawishi karibu kila mshabiki wa soka la England kuwa wanao uwezo mkubwa wa kushinda taji hilo. Wanawazidi Spurs walio kwenye nafasi ya pili kwa alama 5.

Uwepo wa vipaji kama Riyad Mahrez, Jamie Vardy, N’Golo Kante na wapiganaji kama Chistian Fuchs na nahodha Wes Morgan na wengine ndio ulioifikisha Leicester ilipo na ndio ambao unaweza kuifanya imalize kwenye nafasi yake.

Bahati yao nzuri ya kutoandamwa na majeruhi ni moja kati ya vitu vinavyoweza kuwafanya wapinzani washindwe kuwashusha pale walipo.

Matokeo yao ya karibuni pia yanawapa nafasi ya kunyanyua taji. Kwenye michezo yao tisa ya mwisho wamekusanya alama 20. Ikiwa watakusanya idadi hiyo hiyo ya alama kwenye michezo 9 iliyosalia watamaliza na alama 80.

Alama hizo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ikiwa timu hiyo husika pia itakusanya alama sawa na ilizokusanya kwenye michezo tisa ya mwisho iliyocheza. Lakini si jambo rahisi kwao kukusanya alama hizo kwenye michezo iliyobaki.

Hugo Lloris
Hugo Lloris

Changamoto kubwa ambayo inawakabili vijana hawa dhidi ya dhamira yao ya kunyanyua ndoo ni uwepo wa mechi ngumu kwenye michezo ya mwishoni.

Kwenye michezo yao mitatu ya mwisho watakuwa na kibarua ndani ya Old Trafford, kisha kucheza nyumbani dhidi ya Everton na kumalizia Stamford Bridge. Kuna uwezekano mkubwa wa kudondosha alama za kutosha kwenye michezo hiyo mitatu.

Kwangu uwezekano wa Leicester kutwaa taji la EPL ni 7/10. Ninaamini vijana hawa wa Ranieri watadondosha alama za kutosha kwenye michezo iliyosalia na hivyo kukaribisha ushindani mkali kutoka kwa wapinzani hasa Spurs.

Spurs wao pia wanao uwezekano wa kutosha wa kutwaa taji hili. Wao ndio timu bora ya EPL linapokuja suala la ulinzi msimu huu. Wamerushusu mabao 24 pekee mbaka sasa ambayo ni machache kuliko timu yoyote.

Hawako nyuma pia kwenye suala la ushambuliaji. Ni Leicester City na Manchester City pekee zenye magoli 52 kila moja zinazowazidi Spurs kwa magoli, ambapo wao wamefunga magoli 51.

Viwango vinavyooneshwa na Mousa Dembele, Hary Kane, Dele Alli, Christian Eriksen, Toby Alderweireld na wengine vitawatoa Spurs kimasomaso endapo watakaza buti na kupigana zaidi kwenye michezo yao 9 iliyosalia.

Vijana hawa wa Mauricio Pochettino wamekusanya alama 19 kwenye michezo yao tisa iliyopita. Ikiwa watakusanya alama kama hizo kwenye michezo tisa iliyobaki watamaliza na alama 74.

Hapa watahitaji kuomba dua Leicester wafungwe angalau michezo minne na kutoa sare moja kati ya michezo tisa iliyosalia ndipo wamalize juu yao. Hilo si rahisi hata kidogo kutokea.

Changamoto ya michezo migumu pia inawakabili Tottenham. Wana safari ya kutembelea Anfield na Stamford Bridge. Hata hivyo mchezo wa Anfield upo nje ya michezo sita ya mwisho.

Spurs nawaona wakiwa na uwezekano wa 6/10 wa kunyanyua taji la EPL. Ninaamini watakusanya alama nyingi zaidi ya zile zitakazokusanywa na Leicester kwenye michezo iliyosalia. Ila tofauti ya alama 5 iliyopo sasa inaweza kuwanyima ubingwa.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Chelsea nje Ulaya

Tanzania Sports

Ulivyo uwezekano wa Arsenal ama Man City kutwaa taji la EPL