in , ,

Ulivyo uwezekano wa Arsenal ama Man City kutwaa taji la EPL

 

 

Zimesalia raundi 9 pekee kuelekea mwishoni wa msimu huu wa EPL. Ukiwatoa Manchester City, Liverpool, Everton na Newcastle United waliocheza michezo 28, timu nyingine zote zimeshacheza michezo 29 kila moja.

Leicester City chini ya Claudio Ranieri ndio wanaoongoza kwenye msimamo wa EPL wakiwa na alama 60. Tottenham Hotspur wanashikilia nafasi ya pili na alama zao 55.

Washika Bunduki wa London wanazo alama 52 zinazowaweka kwenye nafasi ya tatu huku nafasi ya nne ikishikiliwa na Manchester City wenye alama 50 na mchezo mmoja mkononi.

Kwenye makala hii tunatazama uwezekano wa kutwaa taji la EPL kwa timu mbili zilizo kwenye nafasi ya tatu na ya nne. Hizo ni Arsenal na Manchester City.

Arsenal wana alama 52. Kuna tofauti ya alama 8 kati yao na vinara Leicester City. Inapozingatiwa kuwa imebaki michezo 9 pekee tofauti hiyo ya alama ni kubwa mno.

Washika Bunduki hawa wamekusanya alama 10 pekee kwenye michezo tisa ya mwisho ya Ligi Kuu ya England.

Ikiwa watakuwa na uwiano huo huo wa matokeo kwenye michezo tisa iliyosalia watamaliza na alama 62 pekee hivyo hawataweza kutwaa taji na pengine watashindwa hata kuwemo kwenye timu nne za juu.

Michezo tisa waliyobakisha Arsenal ni dhidi ya West Bromwich, Everton, Watford, West Ham, Crystal Palace, Sunderland, Norwich, Manchester City na Aston Villa. Kiuhalisia vijana hawa wa Wenger wamebakisha michezo michache migumu.

Pengine hilo linaweza kuwafanya wakusanye alama nyingi kwenye michezo iliyobaki zaidi ya zile watakazokusanya vinara Leicester kwenye idadi hiyo ya michezo.

 Manuel Pellegrini na Kevin De Bruyne
Manuel Pellegrini na Kevin De Bruyne

Changamoto kubwa inayowakabili Arsenal ni kuandamwa na majeruhi ya kutisha. Kwenye mchezo wa FA ambao Arsenal walicheza dhidi ya Hull City wiki ilyopita Ramsey, Mertesacker na Gabriel waliongezeka kwenye orodha ya majeruhi.

Majeruhi wengine ni Jack Wilshere, Santi Cazorla, Oxlade-Chamberlain, Thomas Rosicky na Laurent Koscielny anayetarajia kurudi kwenye mchezo ujao.

Uwezekano wa Arsenal kutwaa taji ni 3/10. Tofauti ya alama 8 iliyopo, matokeo yao ya karibuni na orodha pana ya majeruhi inaninyima chaguo zaidi ya kuhitimisha kuwa wanao uwezekano kiduchu mno wa kumaliza juu ya Leicester.

Manchester City walio kwenye nafasi ya nne wana kiporo dhidi ya Newcastle walio kwenye nafasi ya 19. Huo ni mchezo rahisi mno hivyo wana uwezekano mkubwa wa kushinda.

Kwa sasa vijana hao wa Etihad wana alama 50 ambazo ni 10 pungufu ya vinara Leicester City. Wao ni moja kati ya timu bora kwenye upande wa ushambuliaji. Wamefunga mabao 52 sawa na Leicester.

Pia wao ni moja kati ya timu zinazoaminika kuwa na wachezaji wenye vipaji binafsi vya juu. Kevin De Bruyne, Sergio Aguero na David Silva ni mifano mizuri kwenye hilo.

Viwango vilivyozoeleka vya wachezaji wa Manchester City vinaweza kumshawishi mshabiki yeyote wa soka la England kuwa timu hiyo inaweza kukusanya alama zaidi ya 25 kwenye michezo 10 waliobakisha.

Hata hivyo matokeo ya michezo ya karibuni ya vijana hao wa Manuel Pellegrini yanaleta picha tofauti. Wamekusanya alama 15 pekee kwenye michezo yao kumi ya mwisho.

Ikiwa watakusanya idadi hiyo hiyo ya alama kwenye michezo yao kumi iliyosalia watamaliza na alama 65. Hawataweza kushinda taji na alama hizi.

Kitu kilichowafanya Manchester City kushindwa kuwepo kwenye nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa EPL kwenye wakati kama huu ndicho kinachoelekea kuwakosesha ubingwa.

Kitu hicho ni morali ya upiganaji. Wachezaji wa Man City wanakosa morali ya upiganaji waliyo nayo vinara Leicester. Uwezekano wao wa kushinda EPL ni 4/10.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Ulivyo uwezekano wa Leicester ama Tottenham kutwaa taji la EPL

Tanzania Sports

YANGA YAWANYOOSHA APR JIJINI KIGALI