Kumekucha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), ambapo vigogo wanaendelea
kuoneshana kazi, huku vibao vikigeuka na timu nyingine zikishika kasi.
Mabingwa watetezi, Real Madrid walienda sare ya 3-3 na Legia Warsaw wa Poland.
Mechi yao ilichezwa bila washabiki kuhudhuria, kutokana na washabiki
kufanya fujo kwenye mechi baina ya Legia na Borussia Dortmund ambapo
Legia walilimwa mabao 6-0. Walipigwa faini ya pauni 69,000 na marufuku
ya washabiki.
Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Legia wanatolewa nje kwenye michuano
hiyo, kwani wamepata alama moja tu katika mechi nne za kundi lao.
Dinamo Zagreb na Club Brugge nao wataondoka baada ya kufungwa mechi
nne mfululizo kwenye michuano hiyo.
Borussia Dortmund wamejihakikishia kuvuka kwenda hatua ya 16 bora
baada ya ushindi wao dhidi ya Sporting Lisbon. Monaco waliwapiga 3-0
CSKA Moscow.
Lyon kutoka Ufaransa walikwenda sare na Juventus wakati Leicester,
mabingwa wa England walishikilia rekodi ya kutopoteza mchezo kwenye
UCL kwa kwenda sare tasa ugenini kwa FC Copenhagen.
Tottenham Hotspur walifanya vibaya baada ya kupoteza mechi muhimu kwa
0-1 dhidi ya Bayer Leverkusen wakiwa nyumbani Wembley. Wanaonekana
kutokuwa na bahati na uwanja huo unaochukuliwa kuwa wa taifa kwa
England.
Manchester City walifanikiwa kulipiza kisasi baada ya kuwafunga
Barcelona 3-1 jijini Manchester na kumweka Pep Guardiola roho kwatu.
Arsenal wamefuzu kwa hatua ya 16 bora baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya
Ludogorets Razgrad, wakitoka kufungwa 2-0 hadi ushindi, likiwamo goli
zuri sana la kiungo Mesut Ozil.
Mjerumani huyo alimvuka kipa aliyekuja kutaka kuokoa, kisha akawapiga
chenga za maudhi walinzi wawili wakaenda chini kabla hajaweka kitu
nyavuni.
Kwenye mechi ya kwanza Arsenal waliwafunga wapinzani wao hawa mabao
6-0 Emirates, lakini mechi ya marudio ilionekana kuwa mwiba baada ya
kuanza kulala kwa 2-0.
Mabao mengine ya Arsenal yalifungwa na Granit Xhaka na Olivier Giroud,
ambapo golini kama ada alikuwapo kipa David Ospina aliyepewa majukumu
ya UCL.