in , , ,

Arsenal wachomoa kwa Man U

Manchester United dhidi ya Arsenal

*Liverpool wabaki kileleni, City safi

*Mabingwa watetezi hali ni ngumu

Mechi kubwa iliyofuatiwa na wengi kutoka pembe mbalimbali za dunia
baina ya Manchester United na Arsenal imemalizika kwa sare ya 1-1.

Wenyeji, Man U walionekana kana kwamba wangeibuka na ushindi kutokana
na kasi yao, japokuwa Arsenal walitawala zaidi mchezo kwa asilimia
kiujumla, wenyeji wakaongoza hadi dakika mbili kabla ya kipenga cha
mwisho wageni waliposawazisha.

Alikuwa ni mshambuliaji Mfaransa, Olivier Giroud aliyeingizwa akitoka
benchi kuokoa jahazi aliyefanya kweli, akitumia kipaji na uwezo wake
mkubwa zaidi wa mipira ya juu, akatia mpira kimiani dakika ya 88 kwa
kichwa kufuatia majalo la Alex Oxlade-Chamberlain. Bao la United
lilifungwa na Juan Mata dakika ya 68.

Arsene Wenger alionesha kuridhishwa na ushindi huo ambapo kikosi chake
kilikosa huduma muhimu ya beki wa kulia anayepanda na kushuka, Hector
Bellerin ambaye aliumizwa na Danny Rose wa Tottenham Hotspur kwenye
mechi iliyotangulia ambapo walitoka 0-0. Pengo lake lilizibwa na beki
aliyekuwa kwa mkopo West Ham msimu jana, Carl Jenkinson.

Mata akifunga goli la kuongoza dhidi ya Arsenal
Mata akifunga goli la kuongoza dhidi ya Arsenal

Hadi mapumziko Arsenal hawakuwa wamepiga mpira wowote uliolenga lango
la United na kumfanya kipa wao, David de Gea kuwa likizo lakini kipa
wa Arsenal, Petr Cech alikuwa na kibarua kizito na aliokoa mabao mengi
ya wazi kutokana na uzoefu wake. Kocha wa Man U, Jose Mourinho
alilalamika kwamba walinyimwa penati na kusema sare hiyo kwao
inaonekana kama wamefungwa.

Arsenal wamebaki kwenye nafasi yao ya nne baada ya kufikisha pointi
25, mbili nyuma ya Liverpool wanaoongoza ligi na ambao jana walibanwa
na Southampton kwa kwenda suluhu. Manchester United wao wapo nafasi ya
sita wakiwa wamejikusanyia pointi 19 sawa na Everton walio nafasi ya
saba.

Manchester City walikuwa vyema jana kwani walipata ushindi wa 2-1
dhidi ya Crystal Palace, ambapo Yaya Toure alifunga yote mawili. Huyu
ni kiungo aliyerejeshwa kundini baada ya majibizano ya wakala wake na
kocha Pep Guardiola kutokana na mchezaji huyo kuwekwa kando tangu
mwanzo wa msimu na wakati mwingine kufikiria kuondoka. Hii ilikuwa
mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England (EPL) kucheza msimu huu.

Heka heka uwanjani
Heka heka uwanjani

Bao la Palace liliwekwa kimiani na Connor Wickham dakika ya 66, likiwa
ni la kusawazisha dhidi ya lile la Toure la dakika ya 39. Toure
alimaliza kazi dakika saba kabla ya mechi kumalizika, akitia kimiani
mpira wa kona wa Kevin de Bruyne. City wana pointi na mabao sawa na
Liverpool lakini Liver wanakuwa juu kutokana na alfabeti yao ya kwanza
‘L’ kuwa mbele kimpangilio kuliko ‘M’ ya City.

Matokeo mengine ni Everton kwenda sare ya 1-1 na Swansea, Stoke kulala
nyumbani 1-0 dhidi ya Bournemouth, Sunderland kushangaza kwa kupata
ushindi wa kwanza wa 3-0 dhidi ya Hull, Watford kuwatandika mabingwa
watetezi – Leicester 2-1 na Spurs kuwazidi nguvu West Ham kwa 3-2.

Chelsea ambao Jumapili hii wanazuru Middlesbrough kukamilisha mzunguko
wa 12, wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 25 sawa na Arsenal
wakati Spurs wamefikisha pointi 24. Mkiani wamo Swansea wenye pointi
sita, Sunderland wenye nane na Hull wakiwa na 10. Timu tatu zina
pointi 11 nazo ni West Ham, Palace na Middlesbrough wakati mabingwa
watetezi wanazo 12 kutokana na mechi 12 wakiwa nafasi ya 14.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Ulaya kuchele!

Tanzania Sports

CR7 awabomoa Atletico